Home » » CCM YADAIWA KUIHUJUMU CHADEMA GEITA

CCM YADAIWA KUIHUJUMU CHADEMA GEITA

Na Victor Bariety, Geita
BAADHI ya viongozi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) mkoani Geita, wanadaiwa kupanga njama za kukidhoofisha Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA).

Chama hicho kinadaiwa kufanya hivyo kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi, kuihujumu Chadema katika kampeni za uchaguzi mdogo wa udiwani wa Kata ya Lwezera zinazoanza Oktoba 6 mwaka huu.

Tayari Jeshi la Polisi wilayani hapa, linamsaka aliyekuwa Diwani wa Kata ya Sombetini, kupitia CCM, kabla ya kuhamia Chadema, Alphonce Mawazo.

Mawazo ambaye anafanya mikutano ya Chadema chini ya kaulimbiu ya Vuguvugu la Mabadiliko (M4C), anatafutwa kwa tuhuma za uchochezi.

Baadhi ya viongozi wa Chadema wilayani hapa wameeleza kuwa, kutafutwa kwa Mawazo ni sehemu ya mkakati huo wenye lengo la kuwatisha wafuasi wa chama hicho.

Wamesema kuwa, mkakati huo unalenga kuzuia viongozi wa kitaifa wa Chadema walioletwa wilayani hapa, kuongeza nguvu katika kampeni hizo.

Taarifa hizo zinasema, katika mpango huo, baadhi ya viongozi wa CCM wamepanga kuwakamata na kuwafungulia kesi viongozi wa Chadema waliokuja Geita, kuhakikisha kata ya Lwezera ambayo awali ilikuwa ya CCM inarudi mikononi mwa Chadema.

Mawazo anadaiwa kuchochea vurugu katika mkutano wa uzinduzi wa M4C uliofanyika juzi katika viwanja vya magereza, uliohutubiwa na Mbunge wa Nyamagana Ezekiel Wenje (CHADEMA).

Kwa mujibu wa taarifa kutoka Jeshi la Polisi wilayani hapa, Mawazo anatafutwa kwa tuhuma za uchochezi, ambapo wakati akihutubia katika mkutano huo, aliwahamasisha wananchi kutokubali kunyanyaswa na jeshi hilo na kusema kuwa jeshi hilo linatumika vibaya.

Tuhuma nyingine ni kwamba, katika mkutano huo Mawazo alidai kuwa, Mkuu wa Wilaya ya Geita (DC) alipata wadhifa huo kwa hisani ya Rais Jakaya Kikwete.
Chanzo: Mtanzania

0 comments:

Post a Comment

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Geita Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa