Home » » WANAOSADIKIWA KUUA VIKONGWE WAKAMATWA GEITA

WANAOSADIKIWA KUUA VIKONGWE WAKAMATWA GEITA



Na Victor Bariety, Geita
JESHI la Polisi limefanikiwa kuwakamata watu mbalimbali wanaosadikiwa kujihusisha na mauaji ya vikongwe kwa imani za kishirikina na majambazi sugu, wanaotumia silaha za moto.

Kukamatwa kwa watu hao kulikuja baada ya jeshi hilo kufanya msako mkali kwa kushirikiana na wananchi katika operesheni kata mapanga, inayoendelea kufanyika kimkoa na katika kila wilaya.

Matukio hayo yalitokea kwa nyakati tofauti Julai 23 hadi 28, mwaka huu, kuanzia saa saba usiku hadi saa 10 usiku.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Geita, Leonard Paul, aliwataja majambazi waliokamatwa kuwa ni Victor Joseph (18), Emmanuel Jacob (20), Emmanuel Paul (25), Simeo Petro (27), Yunu Kasase (21), Legea Nicholaus (23), Lutae Magala (25), wote wakiwa ni wakazi wa Geita.

Aliwataja majambazi sugu kuwa ni Msafiri Kiselehelo (37), aliyekutwa na kivuli cha hati ya Nolle Proseque ya kesi ya mauaji P12/2006 ya Kibondo mkoani Kigoma iliyotolewa mwaka 2008 na Benedict Paul (27), mkazi wa Kisiwa cha Ikuza.

Alizitaja mali zilizookolewa katika msako huo ni pamoja na kamera aina ya Yashika yenye thamani ya Sh 50,000, sigara pakiti tano, simu 14 za mkononi, laini za Airtel na betri mbili za simu.

Alisema katika msako huo, jambazi mmoja ambaye jina lake halijafahamika, aliuawa kwa kupigwa sehemu mbalimbali za mwili wake na wanachuo wenye hasira kali, baada ya kuvunja duka la mwananchi mmoja na kupora Sh 900,000 na wenzake wamekamatwa.

Aidha, alisema walifanikiwa kuwakamata majambazi waliotaka kumuua askari katika Kata ya Katoro, Tarafa ya Butundwe, ambapo majambazi wapatao watano wakiwa na silaha waliingia katika Baa ya Twiga na wakafyatua risasi kadhaa dhidi ya askari mwenye namba E.9421 D/S/SGT Thomas, kwa lengo la kumuua.

Alisema askari huyo kwa ujasiri alikwepa shambulio hilo na kukimbia ambapo mwezi uliopita polisi walipata taarifa ya kuwapo majambazi hao katika eneo la Katoro na kufuatilia na kufanikiwa kuwakamata.

Alisema kuna matukio yalitokea hivi karibuni ambapo mwezi huu katika Kijiji cha Shabaka, Tarafa na Wilaya ya Nyang’wale, waliokuwa katika msako walifanikiwa kukamata gobole na watu wanaozimiliki bila kibali ambao ni Yuda Malimi (48) na Faida Julius (32) wote wakazi wa Shabaka, mkoani Geita.

Chanzo: Mtanzania

0 comments:

Post a Comment

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Geita Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa