na Victor Eliud, Geita
WARSHA ya sensa iliyoanza mapema mwezi huu ambayo ilikuwa ifungwe leo imeingia dosari baada ya washiriki kugoma kuendelea na mafunzo wakidai posho yao imechakachuliwa.
Washiriki hao kutoka wilaya tano za mkoa wa Geita walisusia mafunzo hayo jana kwa kuondoka ndani ya ukumbi yalipokuwa yakifanyika mafunzo hayo huku wawezeshaji wakibaki wasijue la kufanya.
Tukio hilo lilitokea majira ya saa nane mchana muda mfupi baada ya washiriki hao kupata chakula cha mchana kwa lengo la kujiandaa kurudi ukumbini kuendelea na mafunzo hayo.
Sakata hilo lilianza pale mhasibu alipowataka washiriki hao 135 kuchukua posho zao kabla ya kuendelea na mafunzo hayo na ndipo alipojikuta akisusiwa posho.
“Utatulipaje pesa pungufu...acheni uchakachuwaji..siku ya kwanza mmetulipa sawa leo utatulipaje posho ya namna hii hatukubali,” alisikika mmoja wa washiriki hao akimfokea mhasibu.
Kwa mujibu wa washiriki hao posho imeshuka kutoka sh 65,000 hadi 45,000 kinyume cha makubaliano ya awali.
Kutokana na hali hiyo, Mratibu wa Sensa Mkoa wa Geita, Erasmus Rugalabamu, alijikuta kwenye wakati mgumu kuokoa jahazi hilo, lakini aligonga mwamba baada ya washiriki hao kugoma kumsikiliza na kutawanyika.
Akizungumza na Tanzania Daima kuhusu tukio hilo, Mratibu wa Sensa Mkoa, mbali na kuthibitisha kususiwa ukumbi na washiriki hao alidai wanatarajiwa kukaa kikao na viongozi wa sensa wilaya na mkoa, ili kujua namna ya kutatua tatizo hilo.
Mafunzo hayo yalifunguliwa hivi karibuni na Mkuu wa Mkoa wa Geita, Magalula Magalula huku akiwataka wawezeshaji wa mafunzo hayo kutowaonea aibu walevi na wanalala kwenye mafunzo hayo.
Wakati huohuo, Sitta Tumma kutoka Mwanza, anaripoti kuwa serikali imewaonya watu watakaodiriki kukwamisha zoezi la sensa watachukuliwa hatua kali za kisheria ikiwamo kushtakiwa mahakamani.
Onyo hilo lilitolewa juzi na Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana, Baraka Konisaga, alipozungumza na waandishi wa habari ofisini kwake kuhusiana na maandalizi ya sensa.
Alisema serikali na vyombo vyake vya dola vimejipanga kuwashughulikia kikamilifu watu wote watakaovuruga zoezi hilo, hivyo ni vema raia wote wakashiriki kikamilifu katika kufanikisha azma hiyo ya serikali.
Chanzo: Tanzania Daima
0 comments:
Post a Comment