By Daniel Limbe, Geita
Askari Polisi wa Kituo cha Wilaya ya Geita, amekamatwa na kutozwa faini ya Sh. 20,000 kwa kosa la kubeba abiria wawili kwenye pikipiki maarufu kama mishikaki.
Askari huyo alakamatwa na baadhi ya waendesha pikipiki wilayani humu baada ya kumuona mlinzi huyo wa amani akivunja sheria mbele yao.
Akizungumza kwenye kikao cha majadiliano baina ya waendesha pikipiki na Jeshi la Polisi mkoani humu, Mwenyekiti wa waendeshaji wa bodaboda, Mashamba Tulende, alisema walifikia uamuzi huo baada ya kuona askari huyo amevunja sheria za usafirishaji na kukiuka makubaliano halali ya vikao vyao vilivyoagiza kusitishwa kwa ubebaji wa `mishikaki'.
Kwa mjibu wa mwenyekiti huyo, taratibu hizo walijiwekea wenyewe ili kudhibiti wimbi la ongezeko la ajali za barabarani ambazo zimekuwa zikitokea mara kwa mara na kusababisha vifo vya watu wengi kila mara.
Alifafanua kuwa baada ya makubaliano hayo, wamekuwa wakikamatana wao wenyewe na kufikishana kwenye vyombo vya dola kwa anayekiuka.
Alisema hayo juzi kwenye kikao kilichoandaliwa baina yao na Mkuu wa Polisi Usalama Barabarani mkoani Geita, John Mfinanga.
Kikao hicho kililenga kuwaelimisha waendesha bodaboda sheria za usalama barabarani ili kuepuka ongezeko la vifo vinavyotokana na ajali za bodaboda.
Chanzo: Nipashe
0 comments:
Post a Comment