na Stella Ibengwe, Geita
MKUU wa Mkoa wa Geita, Said Magalula, amesema serikali haitasita kuwachukulia hatua watu watakaovuruga zoezi la Sensa ya Watu na Makazi.
Magalula alitoa onyo hilo mwishoni mwa wiki alipokuwa akifungua mafunzo ya siku 12 kwa wakufunzi 135 wa sensa kutoka wilaya tano za mkoa huo.
Alisema kuna baadhi ya watu wanaotaka kuhujumu sensa hiyo kwa manufaa yao na kuwataka kuacha tabia hiyo, kwani serikali haitawavumilia.
Pamoja na hilo, aliwataka viongozi wa dini na vyama vya siasa kuendelea kutoa ushirikiano, ili kuwezesha kazi hiyo kufanyika kwa amani na utulivu kwa kuiasa jamii kuacha kuwaficha watu wenye ulemavu, kwani kila mtu ana haki ya kuhesabiwa.
Kwa upande wake, Mratibu wa Sensa Mkoa wa Geita, Erasmus Rugarabamu, alisema mafunzo hayo yanatolewa kwa wakufunzi na makarani kutoa elimu kwa jamii iache kuwaficha watu wenye ulemavu majumbani.
“Serikali imetoa kipaumbele kwa kutoa mafunzo maalumu kwa wakufunzi hawa, ili wapate takwimu sahihi za watu zitakazoisaidia serikali kupanga mipango vizuri ya maendeleo,” alisema Rugarabamu.
Alisisitiza kuwa sensa haihusu imani walizonazo, pia watahakikisha taarifa watakazozitoa wakati wa kujibu maswali ya sensa zitakuwa siri na zitatumika kwa masuala ya takwimu pekee.
Chanzo: Tanzania Daima
0 comments:
Post a Comment