Home » » Waendesha bodaboda wamkamata polisi

Waendesha bodaboda wamkamata polisi


na Victor Eliud, Geita
MWENYEKITI wa waendesha pikipiki mkoani Geita, Mashamba Tulende, ameonyesha kukerwa na baadhi ya askari polisi wanaobeba watu zaidi ya mmoja kwenye pikipiki (mishikaki) na kumuweka chini ya ulinzi askari aliyetenda kosa hilo.
Mbali ya kumweka chini ya ulinzi, alimwamuru askari huyo kuimba wimbo unaoonyesha udhaifu wake na kumchezesha kwata, kabla ya kulipa faini na kuruhusiwa kuondoka.
Mwenyekiti huyo wa waendesha pikipiki alisema alilazimika kufanya hivyo kutokana na kukerwa na kitendo hicho hasa ikizingatiwa kuwa wao wenyewe ndio wamekuwa wakiwakamata watu wanaofanya kosa hilo na kuwafikisha kwenye vyombo vya dola.
Akizungumza kwenye kikao kilichoandaliwa kati yao na Mkuu wa Polisi wa Usalama Barabarani, mkoani Geita, John Mfinanga, kikiwa na lengo la kuwaelimisha waendesha bodaboda sheria za usalama barabarani, alisema suala la ‘mishikaki’ kwao limekuwa historia, ila juzi walimkamata askari akiwa amebeba ‘mishikaki’.
“Nilipopewa taarifa na kufika huweziamini bila kuchelewa na kujali ni askari nilimuweka chini ya ulinzi na kumwamuru aimbe wimbo wa kukiri udhaifu wake huo naye alitii na kufanya hivyo wakati mimi nikifanya utaratibu wa kumfikisha kituoni,” alisema.
“Askari wako huyo aliposikia nataka kumfikisha kituoni alikuwa mpole na kuomba apewe adhabu yoyote, ili nisimfikishe na nadhani alihofia kumwaga unga wake hivyo nilimtaka alipe faini ya sh 20,000 na baadaye nilimruhusu kuondoka,” alisema Tulende.
Alisema aliamua kufanya hivyo ili kuonyesha hasira zake dhidi ya baadhi ya askari polisi wenye tabia hiyo.
Alimhakikishia mkuu huyo wa usalama barabarani kuwa ataendelea kuwakamata askari wake iwapo watatenda kosa hilo huku akimtahadharisha kumkamata hata yeye, ili kujenga imani kwa waendesha bodaboda.
Mkuu huyo wa usalama barabarani aliunga mkono kauli hiyo na kuahidi kumpa ushirikiano katika suala hilo hasa kutokana na ukweli kwamba ajali nyingi katika mkoa huo zilikuwa zinaongozwa na magari madogo ya abiria maarufu michomoko ambazo zimepigwa marufuku hivi karibuni.
“Nakuomba usilegeze hata mimi nikikosea nikamate maana bila hivyo ajali zitaendelea kupoteza roho za Watanzania wasio na hatia,” alisema Mfinanga.
Chanzo: Tanzania Daima

0 comments:

Post a Comment

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Geita Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa