Home » » MAJAMBAZI YATEKA KIJIJI GEITA

MAJAMBAZI YATEKA KIJIJI GEITA



KAMANDA wa Polisi Mkoani Geita Kamishna Msaidizi wa polisi (ACP) Leonard Paul Akizungumza na Blog Hii.(Picha na David Azaria yetu blog)


Na David Azaria wa Geita Yetu Blog
KUNDI la watu wanaosadikiwa kuwa ni majambazi waliokuwa na silaha za kivita,mapanga na marungu wameteka kijiji cha Kibehe kata ya kigongo wilayani chato mkoani Geita na kufanikiwa kupora fedha,simu za mkononi na kujeruhi baadhi ya wananchi.

Tukio hilo limetokea usiku wa kuamkia jana majira ya saa 6;30 usiku baada ya majambazi hao kuteka kaya zaidi ya tano kabla ya kurusha risasi kadhaa hewani hatua iliyosababisha wananchi kushindwa kutoka ndani ya nyumba zao.

Wakizungumza na Blog hii baadhi ya mashuhuda wa tukio hilo Mussa Limbe na Inocent Moshi wamesema majambazi hao baada ya kuanza uvamizi huo uliodumu kwa zaidi ya saa 2 walimteka na kumweka chini ya ulinzi mwalimu wa shule ya msingi Kibehe Nyalusule Kungula na kumuamuru kuwatembeza kwenye kaya za watu wenye fedha.

Baada ya uvamizi huo,majambazi hao walitumia silaha za jadi(Mapanga na Marungu) kuwajeruhi baadhi ya wananchi kwa lengo la kuwashinikiza kutoa fedha na simu za mkononi hatua iliyopelekea kujeruhiwa vibaya katika maeneo mbalimbali ya miili yao.

"Baada ya kuvamia majambazi hayo yalianza kuwapiga kwa kutumia marungu na mapanga huku yakiwashinikiza kutoa fedha zote walizo nazo na baada ya kuchukua fedha na simu yalianza kufyatua risasi hewani ili kuwatishia wananchi"alisema Moshi

Aidha wamedai kuwa majambazi hao wanaokadiriwa kufikia kuwa 11 walianza kupiga yowe wakati wakiondoka na wananchi walipojitokeza kwa lengo la kusaidia huku wakifuata mwelekeo waliokuwa wakikimbilia na kupia yowe walikutana na majambazi hao na kuwashambulia kwa mapanga hatua iliyopelekea baadhi ya wananchi kujeruhiwa vibaya.

Wamewataja baadhi ya waliojeruhiwa vibaya kuwa ni pamoja na Paschal Magoma,Mwalimu wa shule ya msingi Bukamila Edwin Mponela na Mtu mmoja ambaye hajafahamika jina lake lakini anadaiwa kuwa fundi wa pikipiki katika kijiji hicho ambao wote wamelazwa kwenye hospitali ya wilaya ya chato kwaajili ya matibabu.

Kamanda wa polisi mkoani Geita Kamishna Msaidizi wa Polisi Leonard Paul amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kwamba jeshi la polisi linaendelea kuwasaka watu wote wanaodaiwa kuhusika katika tukio hilo na kwamba watakapo bainika watafikishwa mahakamani.

Aidha Kamanda Paul amewataka wananchi Mkoani hapa kujenga tabia ya kutoa taarifa mapema kwa jeshi la polisi pindi wanapowahisi baadhi ya watu wasiowafahamu ili iwe rahisi kwa jeshi hilo kukabiliana na matukio kama hayo kabla ya kutokea uvunjifu wa amani.

Kamanda huyo amedai kuwa mbali na polisi kuwahi kwenye eneo la tukio hakuna mtu aliyekamwatwa kuhusika na uvamizi huo,lakini ameapa kuwa waliohusika katika tukio hilo ni lazima watatiwa mbaroni.

“Kwa mahati nzuri tunafanya kazi kwa ukaribu sana na wananchi……naamini kwamba wote waliohusika katika tukio hili tutawakamata na kuwafikisha kenye vyombo vya sheria,wananchi wanatuamini,na ni lazima tuaminiane ili tuweze kuujenga mkoa wetu ambao bado ni mchanga na hasa ukizingatia kwamba umeanzishwa hivi karibuni……’’ alisema na kusisitiza Kamanda huyo.

Hili ni tukio la pili la ujambazi kutokea katika kipindi cha mwezi mmoja ambapo tukio la kwanza lilitokea mwishoni mwa mwezi juni wakati ambapo watu wanaosadikiwa kuwa ni majambazi walipomvamia aliyekuwa mkuu wa kituo cha polisi Katoro Inspekta msaidizi wa Polisi Thomas Mboya wakati akiwa baa kwa lengo la kumuua.

Hata hivyo ilimlazimu Mkuu huyo wa kituo kutumia mbinu za kivita zaidi katika kukabiliana na majambazi hayo ambapo alifanikiwa kunyanyuka na meza iliyokuwa imejaa vinyaji na kummwagia mmoja wa majambazi hao aliyekuwa na Bunduki,na kisha kukimbia huku wakimmiminia risasi.

Siku chache baadaye baada ya msako mkali wa polisi walifanikiwa kuwatia mbaroni majambazi hao wakiwemo watatu kutoka nchini Burundi,ambapo mmoja aliuawa kwa kupigwa risasi baada ya kujaribu kumpora Askari Bunduki.



0 comments:

Post a Comment

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Geita Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa