Home » » BAADA YA AJALI GEITA SERIKALI YAPIGA MARUFUKU USAFIRI WA MICHOMOKO

BAADA YA AJALI GEITA SERIKALI YAPIGA MARUFUKU USAFIRI WA MICHOMOKO



Na David Azaria Geita Yetu BLOG
SIKU moja baada ya watu 11 kupoteza maisha papo hapo kutokana na ajali mbaya ya magari mawili madogo ya abiria kugongana uso kwa uso na gari lingine Mkoani Geita,Serikali Mkoani Geita imepiga Marufuku magari madogo maarufu kama “Mchomoko” kufanya biashara ya kusafirisha abiria Mkoani hapa.
Marufuku hiyo imepigwa na Mkuu wa Mkoa huo Magalula Said Magalula wakati akizungumza na mamia ya wananchi waliokuwa wamefurika katika viwanja vya hospitali ya wilaya ya Geita,kwa ajil;I ya kushuhudia na kutambua miili ya watu waliokufa katika ajali hiyo.
Kwa mujibu wa mkuu huyo wa mkoa amri hiyo imeanza kutekelezwa tangu juzi ilipotokea ajali,huku akitoa wito kwa wafanyabiashara mbalimbali wa ndani na nje ya Mkoa wa Geita kupeleka magari makubwa kwa ajili ya kusafirisha abiria katika maeneo ambayo magari hayo madogo yalikuwa yakifanya biashara hiyo.
“Agizo hili linaanza kutekelezwa leo hii hii (Jumapili),na kuanzia sasa hivi haya magari (Mchomoko) kazi yake kuu itakuwa ni kufanya kazi za kawaida,na hata kama yakibeba abiria itakuwa ni mmoja ama watatu lakini si kwa mtindo huu wa sasa ambapo badala ya kubeba abiria watano kwa mujibu wa muundo wake yanabeba zaidi ya abiria 12……’’ alisema Mkuu wa Mkoa.
Pia Mkuu huyo wa Mkoa amemuagiza kamanda wa polisi Mkoani hapa kuwaweka ndani na kisha kuwashughulikia mara moja askari polisi waliokuwa wakilinda katika beria ya Nyankumbu,ambao wanadaiwa kuwa waliamua kuyaachia magari hayo kuendelea na safari pamoja na kwamba yalikuwa yamejaza abiria kupita kiasi.
Amedai kuwa katika uchunguzi wake tangu alipowasili Mkoani hapa miezi kadhaa iliyopita amebaini kuwa magari hayo ambayo mengi hufanya safari zake kati ya Mji wa Geita na Katoro ukiachilia mbali wilaya nyingine za Mkoa huo,yamekuwa yakipita katikakatika kizuizi cha polisi kilichopo Nyankumbu Mjini Geita ambapo kuna askari wengi huku yakiwa yamejaza abiria kupita kiasi.
“Nimetoa maelekezo kwa jeshi la polisi kwanza kuwaweka ndani askari wpte waliokuwa wakilinda kwenye Kizuizi cha Nayankumbu kwa sababu tumepata taarifa kwamba pamoja na magari hayo kupita yakiwa yamejaza abiria kupita kiasi,lakini bado wao waliyaachia sasa hii inaonekana kwamba kuna jambo hapo……’’ alisema mkuu huyo wa Mkoa.
Kwa mujibu wa Mkuu huyo wa Mkoa tayari ofisi yake imetoa maelekezo kwa Kamanda wa Usalama Barabarani Mkoani Geita,kuhakikisha kwamba amri hiyo inatekelezwa ipasavyo katika maeneo yote ya Mkoa huo na kwamba askari yeyote wa usalama ambaye itabainika kwamba gari aina ya mchomoko limepita katika eneo lake likiwa na abiria atafukuzwa kazi mara moja.
Huku akionekana mwenye uso uliokunjamana Mkuu wa Mkoa alisema wiki mbili zilizopita allitoa maelekezo kwa askari polisi juu ya kuzuia magari hayo kufanya kazi ya kusafirisha abiria,kwa vile yamekuwa yakihatarisha usalama wa abiria na mali zao kutokana na kujaza kupita kiasi pamoja na kwenda kwa mwendo kasi.
“Wiki mbili zilizopita nililiagiza jeshi la polisi kuyapiga magari haya marufuku kufanya kazi hii ya kusafirisha abiria,lakini inavyoonekana agizo hili halikufanyiwa kazi na ndiyo maana leo hii mnaona tuko kwenye viwanja hivi vya hospitali ya wilaya tunatokwa na machozi kutokana na kupoteza wapendwa wetu……’’ alisema Mkuu wa Mkoa na kuongeza.
“Sasa nasema hivi ni marufuku haya magari kufanya biashara ya kusafirisha abiria kuanzia leo(Jumapili),hili ni agizo katika mkoa Mzima wa Geita,najua kwamba kuna watu na hasa askari polisi ambao hawapendi kutekeleza maelekezo ya serikali,nitafuatuilia suala hili mimi mwenyewe na askari anayejijua kwamba hataweza kutekeleza amri hii,ni vyema akajiondoa mapema……’’.
Usafiri wa Mchomoko uliingia Mkoani Geita mwaka 2009 mara baada ya kukamilika kwa ujenzi wa barabara ya Geita hadi Bukomba kwa lami,ambapo magari hayo yamekuwa maarufu kwa usafirishaji wa abiria katika wilaya za Bukombe,Biharamulo,Chato,Geita na Sengerema.

0 comments:

Post a Comment

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Geita Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa