Home » » Serikali yatenga siku ya usafi Geita

Serikali yatenga siku ya usafi Geita


Na David Azaria,Geita Yetu
SERIKIALI wilayani Geita katika Mkoa wa Geita imetenga siku maalum kwa ajili ya shughuli za usafi,ili kuufanya mji wa huo na vitongoji vyake kuondokana na uchafu na kuwa mfano wa kuigwa nchini.
Mkuu wa wilaya ya Geita Manzie Mangochie alisema serikali imefikia hatua ya kutenga siku ya Alhamisi kuwa siku maalum ya usafi katika maeneo mbalimbali ya mji huo,na kwamba siku hiyo shughuli za biashara pamoja na ufunguzi wa maduka itakuwa ni kuanzia saa 4 asubuhi badala ya saa 12 au saa 1 asubuhi.
Mwandishi wa gazeti hili ambaye alizunguka na kuongea na wananchi na wafanyabiashara walisema kuwa suala la usafi wamelipokea kwa moyo mkunjufu na wamelifurahia kwakua uchafu ulizidi na hakukuwa na mtu au kiongozi wa kuwahimiza kutunza mazingira baada ya kila mtu kujenga mazoea ya kusafisha mazingira majumbani kwao pekee.
Mmoja wa wafanyabiashara hao Suzana Zabron wa soko kuu la Geita alisema pamoja na suala la usafi Bwana afya wa wilaya anatakiwa ahakikishe kuwa kunakuwa na sehemu maalum ya kutupa uchafu kwani kwa sasa wanatupa katika eneo la soko jambo ambalo ni hatari kwa afya na pia eneo wanalofanyia  biashara hakuna vyoo.
Kwa upande wake mmoja wa Maofisa Afya katika mji wa Geita Japhet Masesa kuanzia sasa kila mfanyabiashara anatakiwa awe na chombo cha kuhifadhia taka na na kwamba kutakuwa na trekta ambalo litakuwa likipita asubuhi na kuzikusanya kupeleka eneo husika.
Pia alisema shughuli ya usafi ambayo imefanywa katika eneo la mji kama mfano na  wananchi wakiongozwa na Mkuu wa wilaya hiyo,umewatia moyo kuwa wanaweza kuifanya Geita kuwa safi kama mikoa migine inayosifika kwa usafi na kuongeza kuwa kwa sasa kuna changamoto nyingi ambazo wanajitahidi kuzifanyia kazi na kwa kampeni hii ya usafi endelevu itasaidi kuzitatua.
“Hii kampeni ya usafi kwakweli imetekelezwa ipasavyo na wananchi nao walikuwa wanauchukia uchafu na hii ni kazi ya wote si tu Mabwana afya kwa hiyo tuendeleze kampeni hii kwa pamoja”alisema Masesa
Kwa upande wa mkuu wa Wilaya Mangochie  ambye alitembela maeneo ya masoko kuangalia hali ya usafi aliwataka wananchi na wafanyabiashara kutilia mkazo suala la usafi kwani si jukumu la serikali pekee kwani nao wana nafasi katika hilo.
Alisema kuwa changamoto walizozipokea kutoka kwao zitashughulikiwa na uongozi wa soko utimize wajibu wao kwa kujua matatizo ya wafanyabiashara na kuyafikisha eneo husika ili yatatuliwe.
Aliongeza kuwa mwezi huu utatangazwa rasm mkoa huu kuwa na Halmashauri ya mji na kuna bajeti imetengwa kuhakikisha miundo mbinu inaboreshwa na pia ifikapo mwaka 2015 basi iwe manispaa.
“Unajua kwa sasa jamani tusikae kama ilivyokuwa wilaya huu ni mkoa lazima tuhakikishe mji wetu unakua msafi kwani kuna wageni watakuja na kukuta mzingira machafu watatuelewaje?”alihoji mkuu huyo
Kampeni hii ya usafi ni endelevu ambapo imepangwa kwa wiki kila alhamisi saa moja hadi saa nne itakuwa siku ya kusafisha mazingira na kazi za kufungua biashara itakua baada ya suala la usafi kukamilika.
Hivi karibuni Mkuu wa Mkoa wa Geita Said Magalula alimuagiza mkuu wa wilaya hiyo kuhakikisha kwamba kuhakikisha kwamba mji wa Geita Pamoja na vitongoji vyake unakuwa msafi kwa kuwa mji huo ndipo yalipo Makao makuu ya Mkoa huo.

0 comments:

Post a Comment

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Geita Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa