Home » » MAKALA : KAMANDA PAUL KARIBU, LAKINI UMEJIANDAAJE KUTOKOMEZA UHALIFU GEITA?

MAKALA : KAMANDA PAUL KARIBU, LAKINI UMEJIANDAAJE KUTOKOMEZA UHALIFU GEITA?



Kamanda wa polisi Mkoa wa Geita Kamishna Msaidizi wa Polisi Leonard Paul



Na:David Azaria Geita yetu
“HUWEZI kutokomeza uhalifu mahali popote pale bila kushirikisha jamii katika eneo husika,kwa sababu Jamii ndiyo inayofahamu nani ni mhalifu?, anakaa wapi?, anapatikana wapi na kwa wakati gani……’’. 
Haya ni maneno ya Kamanda wa polisi wa Mkoa wa Geita Kamishna Msaidizi wa polisi Leonard Paul aliyoyatoa wakati wa mahojiano maalum na Mwandishi wa Makala haya Ofisini kwake juu ya mikakati iliyowekwa na Jeshi hilo katika kupambana na wahalifu mkoani hapa. 
Kamanda Paul ambaye anakuwa Kamanda wa Kwanza wa Polisi wa Mkoa wa Geita baada ya Serikali kuanzisha rasmi Mkoa huo pamoja na mingine Mitatu ya Simiyu, Katavi na Njombe, anasema ni vigumu mahali popote pale duniani askari polisi kupata mafanikio katika suala la ulinzi na usalama wa raia na mali zao bila kushirikisha jamii. 
 “Unadhani bila kuwashirikisha wananchi unawezaje kuwapata wahalifu na kuwashughulikia kikamilifu? ndiyo maana mimi nasema ni lazima tuwe na mkakati madhubuti katika kuwashirikisha wananchi wetu ili watambue umuhimu wao katika kulisaidia jeshi la polisi kuwanasa wahalifu,kama tukifanikiwa hilo ni wazi kwamba tutapunguza uhalifu kwa asilimia kubwa kama si kuutokomeza kabisa…..’’. anasema Kamanda Paul. 
Katika kuhakikisha kwamba wananchi wanatoa ushirikiano wa karibu kwa polisi Kamanda Paul anasema kwa sasa anapambana katika kuhakikisha kwamba kitengo cha polisi jamii kinaimarishwa ili kuwafanya wananchi kutambua haki zao ndani na nje ya jeshi la polisi,hali ambayo anaeleza kwamba itawafanya wananchi kujiamini zaidi. 
“Unajua kwa sasa bado kuna wananchi ambao ni waoga hawataki kusikia suala la jeshi la polisi,na sababu ziko wazi tu kwamba huko nyuma kidogo jeshi la polisi ilifika wakati Fulani likawa si rafiki tena wa wananchi,lilikuwa adui na hii ilisababishwa na askari wachache ambao hawakutaka kuzingatia maadili ya kazi zao,sheria na taratibu,lakini tangu mwaka 2006 kuna mabadiliko makubwa sana ndani ya jeshi letu….’’ anaeleza Kamanda Paul na kuongeza: 
 “Naomba wakazi wa mkoa wa Geita kwa ujumla wao wanipe ushirikiano,lakini ushirikiano huu usiwe kwa jeshi la polisi pekee,uwe ni kwa viongozi wote wa kiserikali katika ngazi zote,naamini wakifanya hivyo ni wazi kwamba kila kitu tutakiona rahisi tofauti na ambavyo wanafikiria na tutaujenga mkoa wetu kwa haraka…….’’. 
Viongozi wa serikali ya Mkoa wa Geita wanakabiliwa na changamoto nyingi katika kuhakikisha kwamba wanaujenga Mkoa huo mpya ambapo kwa upande wa jeshi la polisi ni wazi kwamba wanakabiliwa na mambo mbalimbali ikiwemo uhalifu wa kutumia silaha  jambo ambalo limewahi kutikisa wilaya zinazounda Mkoa huo miaka kadhaa iliyopita kabla ya kugawanywa kutoka katika mikoa yao ya zamani ya Kagera, Mwanza na Shinyanga. 
Karibu wilaya zote tano zinazounda Mkoa huo ikiwemo wilaya mbili mpya na tatu za zamani zinakabiliwa na changamoto kubwa ya uhalifu wa kutumia silaha, mauaji ya vikongwe kwa kutumia mapanga kwa Imani za kishirikina lakini pia mauaji ya watu wenye ulemavu wa Ngozi (Albino).        
Wilaya ya Geita ambayo ndipo yalipo makao makuu ya Mkoa ni wazi kwamba ndilo eneo ambalo linakbailiwa na changamoto nyingi,eneo ambalo hata kamanda Paul mwenyewe anakiri kwamba ni lazima iwekwe mikakati ya dhati katika kukabiliana na uhalifu wa kila aina uliopo katika wilaya hiyo. 
Ukiachilia mbali matukio ya ujambazi wa kutumia silaha ingawa kwa sasa hayatokei kwa sana, mauaji ya vikongwe kwa imani za kishirikina, vifo vya wachimbaji wadogo yanayotokana na kufukiwa ndani ya machimbo kutokana na uchimbaji holela lakini kuna suala la vibaka ambalo linaonekana kuenea kwa kasi katika mji wa Geita. 
Lakini pia kibaya zaidi kuna mauaji ya kuikitisha ya watu kuchomwa na Visu ambayo hata hivyo tangu kutangazwa kwa mkoa yameonekana kusimama, hata hivyo kutokana na mauaji hayo kufanyika katikati ya mji wa Geita ambapo ndipo yalipo makao makuu ya mkoa ambao kwa sasa umejaa utitiri wa askari polisi, huenda hilo likawa faraja katika kutokemeza vitendo  hivyo endapo lakini askari hao watawajibika ipasavyo kama ilivyo ndoto ya Kamanda Paul. 
Nyang’hwale ambayo ni wilaya iliyomegwa kutoka katika wilaya ya Geita hauna uhalifu wa lakini matukio ya wilaya ya Geita huenda yakaathiri ukuaji wa wa wilaya hiyo kama jeshi la polisi halitakuja na suluhisho na mikkati ya kuzuia vitendo hivyo kabla havijaanza kushamiri.
Wilaya ya Chato kumekuwepo na matukio ya utekaji wa magari ya abiria na wafanya biashara mara kwa mara ingawa kwa sasa matukio hayo yamepungua,hii inasababishwa na misitu mingi na mikubwa ukiwemo msitu unaotenganisha wilaya za Chato na Biharamulo ambapo ujambazi wa kutumia silaha nao umekuwa ukitoeka mara kwa mara. 
Wilaya ya Bukombe ni moja pia ya maeneo hatari ya uhalifu na hasa ujambazi wa kutumia silaha hali inayosababishwa na uwepo wa misitu na mapori mengi inayowafanya wahalifu kupata nafasi ya kujificha kabla na baada ya kufanya uhalifu.
Kwa upande wa wilaya Mbogwe iliyomegwa kutoka katika wilaya hiyo nayo kuna uhalifu kama huo ingawa si kwa asilimia kubwa,ingawa wilaya hiyo ndiyo inayoonekana kuwa na mauaji mengi ya watu wenye ulemavu wa ngozi (Albino) pamoja na mauaji ya vikongwe kwa imani za Kishirikina. 
Hakuna ubishi kwamba kwa sasa wananchi wamekua na imani kubwa sana na jeshi la polisi kutokana na utendaji wake wa kazi unaozingatia maadili na kwa wanaGeita wanapata matumaini mapya baada ya Geita kuwa mkoa na kupata viongozi wapya akiwamo Kamanda wa polisi Mkoa na Mkuu wa Mkoa huo.
Ni vyema askari wa Polisi wa kawaida wakazidisha imani kwa wananchi ili kuwafanya wakubwa wao kuaminika kwa jamii,kwa sababu ukiwasikia viongozi wa kipolisi ngazi ya Mkoa na hasa Kamanda Paul unapata imani kwamba jeshi hilo limejipanga katika kuhakikisha kwamba ulinzi na usalama wa raia na mali zao katika mkoa wa Geita uko salama salmini. 

0 comments:

Post a Comment

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Geita Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa