Home » » RC Geita awataka watumishi wazembe idara ya misitu kuachia ngazi

RC Geita awataka watumishi wazembe idara ya misitu kuachia ngazi


MKUU wa Mkoa wa Geita Said Magalula Said akihutubia Baraza la Madiwani wa halmashauri ya wilaya ya Geita.Picha na David Azaria

Na David Azaria, Geita yetu

SERIKALI mkoani Geita imewataka Maofisa Misitu Wilaya ya Geita kuachia ngazi mara moja, kama wameshindwa kudhibiti uharibifu mkubwa wa Misitu unaondelea kufanyika katika misitu mbalimbali ya hifadhi iliyoko katika wilaya na Mkoa huo. 
  
Agizo hilo limetolewa na Mkuu wa Mkoa wa Geita Said Magalula Said,wakati akizungumza na Madiwani pamoja na watendaji mbalimbali wa halmashauri ya Wilaya ya Geita, katika kikao cha Baraza la Madiwani kilichofanyika katika ukumbi wa halmashauri ya wilaya hiyo. 
  
Kwa mujibu wa Mkuu huyo wa Mkoa Misitu ya hifadhi inayozunguka wilaya ya Geita imeharibika vibaya, hali ambayo inatishia usalama wa mazingira ya wilaya hiyo, lakini katika hali isiyokuwa ya kawaida watumishi wa idara hiyo wamekaa wakishuhudia huku wakiwa hawana mikakati ya aina yoyote katika kukabiliana na hali hiyo. 
  
“Misitu imeharibiwa, Misitu imepotea na inaendelea kupotea kila kunapokucha, lakini Idara ya misitu ipo, wakuu wa Idara wapo, madiwani wapo, B araza la madiwani Lipo lakini misitu inaangamia hawa woote wanaangalia, hili halikubaliki hata kidogo ni lazima hatua zichukuliwe….’’ Alisema Magagula na kuongeza: 
  
“Lakini kwa sababu kuna watendaji wa idara hii na wanalipwa mishahara na serikali, nataka niseme kwamba ni lazima wawajike katika hili, na kama kweli wameshindwa kudhibiti uharibifu wa misitu yetu ni bora wakaachia ngazi ili tuwapate watu watakaokuwa na uwezo wa kutunza na kulinda misitu yetu…..’’ alibainisha Magalula. 
  
Alisema Serikali haiko tayari kuona Misitu ikiangamia wakati kuna watumishi wa idara husika ambao wamewekwa mahsusi kwa ajili ya kusimamia ulinzi na ustawi wa Hifadhi ya misitu,na kwamba ni lazima mkakati wa serikali wa kutunza na kuhifadhi misitu ulioko kwa mujibu wa sheria na taratibu. 
  
Magalula alimuagiza Mkurugenzi Mtandaji wa halmashauri ya wilaya ya Geita, Mwenyekiti na wakuu wa idara kuchukua hatua za haraka ili kunusuru ukataji na uchomaji mikaa ili sehemu ambayo inamiti ya asili isendelee kuwepo bila kuathiriwa na watu wachache wenye uchu wa kujipatia kipato. 
  
Akizungumzia hali ya misitu, Mkuu wa Mkoa Ofisa Misitu wa wilaya ya Geita Kasika Gamba Kasika alikiri kuwepo kwa uharibifu mkubwa wa misitu katika wilaya ya Geita na sababu kubwa ambayo imepelekea kuwepo kwa hali hiyo ni upungufu wa watumishi katika idara hiyo ambao wanapaswa kukabiliana na majangili wanaovamia na kuharibu misitu. 
  
“Tatizo kubwa ni upungufu wa watumishi tulionao kattika idara hii ambao hawakidhi mahitaji,lakini kibaya zaidi ni kwamba pamoja na upungufu huo wa watumishi lakini hata hao walipo hawajapangwa katika maeneo maalum yanayohusiana na misitu,wamewekwa mijini wanakaa kwenye lami hawana kazi za kufanya huku msitu ukiharibiwa…..’’ alisema Ofisa Misitu huyo wa wilaya. 
  
Aliongeza kuwa tatizo lingine ni ukosefu wa vifaa kama vile magari maalum kwa ajili ya Doria ambapo kwa sasa idara hiyo inalo gari moja ambalo halikidhi mahitaji,kwani misitu iliyopo katika wilaya hiyo ina ukubwa wa jumla ya Hekta 87,820,hivyo gari moja halitoshi kufanya doria. 
  
Misitu ya hifadhi iliyoko katika wilaya ya Geita ni pamoja na Msitu wa hifadhi wa Geita wenye jumla ya Hekta 47,700 ambao umezunguka eneo la Mji wa Geita, Lwamgasa hekta 15,500 ulioko katika Tarafa ya Busanda, Lwande Hekta 15,500 ulioko katika Tarafa ya Bugando na Miyenze Hekta 9,170 ulioko kaatika Tarafa ya Nyang’hwale. 
  



0 comments:

Post a Comment

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Geita Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa