MKUU wa Mkoa wa Geita Said Magalula Said akihutubia Baraza la Madiwani wa halmashauri ya wilaya ya Geita.Picha na David Azaria
Na David Azaria, Geita yetu
Mvutano Mkubwa uliibuka jana katika kikao cha Baraza la Madiwani juu ya ununuzi wa vifaa vya ujenzi wa Barabara, ambapo baadhi ya madiwani walipinga zoezi hilo huku wengine wakipigana kufa na kupona katika kuhakikisha kwamba vifaa hivyo vinanunuliwa.
Hali hiyo iliibuka baada ya Ofisa Mipango wa Halmashauri ya wilaya hiyo Andrew Chikwanda kuwasilisha taarifa yua ununuzi wa vifaa hivyo baada ya kukamilisha taratibu za ununuzi kupitia Benki ya CRDB ambao walikubali kutoa mkopo wa asilimia 100 katika ununuzi wa vifaa hivyo.
Alitaja vifaa vilivyokusudiwa kunuliwa na halmashauri ya wilaya hiyo vikiwa na lengo la kurahisisha shughuli za ukandarasi na hasa ujenzi wa barabara za wilaya hiyo, kuwa ni pamoja na Greda moja, Skaveta, Katapila, na Rola vyote vikiwa na tahamani ya shilingi Bilioni 1.4.
Hata hivyo baada ya kuwasilisha taarifa hiyo mbele ya Madiwani baadhi ya madiwani waliibua hoja ya kupinga ununuzi wa vifaa hivyo kwa madai kuwa vitasababisha mgongano wa kiutendaji,na hasa ikizingatiwa kwamba kwa sasa kuna mgawanyo wa halmashauri tatu katika wilaya ya Geita.
“Binafsi sioni umuhimu wa ununuzi wa vifaa hivi kwa sababu kesho na kesho na keshokutwa halmashauri hizi kila moja inajitegemea,sasa hivi hatuoni kwamba kwa mgawanyo huo kutasababisha vurugu kwa kila mmoja kutaka kubaki na vifaa hivyo,kwa sababu leo tunanunua kama halmashauri ya Geita lakini baada ya siku chache kutakuwa na halmashauri ya Mji,Halmashauri ya Geita Vijijini na Halmashauri ya wilaya ya nyang’hwale……’’ alisema Diwai wa Kata ya Nzera Joseph Musukuma na kuongeza.
“Kwa sasa naona hakuna sababu za kufanya hivyo kwa sababu kwanza hili suala tulikuwa hatujaambiwa katika siku za nyuma sasa iweje liibukie hapa kwenye kikao….’’ Alisema na kuhoji Diwani huyo ambaye alikuwa Mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya hiyo kabla ya kung’olewa mwaka jana kwa madai ya kushindwa kuongoza vikao kwamujibu Sheria, kanuni na taratibu.
Kwa upande wake Diwani wa Kata ya Mtakuja Hilarius Buchuma Alionesha mashaka katika suala la ulipaji wa fedha hizo zinazotolewa kwa mkopo na Benki, huku akibainisha kwamba thamani yote ya upatikanaji na ulipaji wa fedha hizo umejumlisha halmashauri nzima ya wilaya ambayo inatarajiwa kujitenga siku chache zijazo.
“Leo katika taarifa mmeeleza kwamba ulipaji utahusu mapato yatakayotokana na shughuli zitakazofanywa na vifaa hivyo katika halmashauri ya wilaya ya Geita ambayo kwa sasa inajumuisha wilaya ya Nyang’hwale, Geita Vijijini pamoja na Halmashauri ya Mji…sasa tunategemea nini kama hali hiyo itajitokeza, hatuoni kwamba tutakuja kuchanganyana…??...’’ alisema na kuhoji Diwani huyo.
Hata hivyo Diwani wa Kata ya Butobela Leonard Bugomola alipingana na madiwani hao na kukifafanulia kikao hicho cha madiwani kwamba suala la ununuzi wa vifaa hivyo ni ajenda ya muda mrefu ambayo imewasumbua kwa muda mrefu,na kwamba suala hilo lilikwishapitishwa katika vikao vya baraza vilivyopita na suala lililokuwa limebaki ni utekelezsaji wake.
“Hili suala si la kutusumbua leo hii na kuanza kulijadili upya,limetusumbua kwa muda mrefu wakati tukiangalia ni namna gani tujaribu kupunguza gharama zinazotumika katika utengenezaji wa barabara za halmashauri na hasa zile za vijijini na ndiyo maana tumefikia hatua hii,kwa hiyo kuanza kulijadili tena leo ni kujichanganya sisi wenyewe…….’’ alisema Diwani Bugomola.
Kufuatilia mabishano makali yaliyodumu kwa muda wa nusu saa huku mkurugenzi a Halmashauri ya wilaya hiyo Bensoni Tatala akisimama kila mara kutoa ufafanuzi juu ya faida ya ununuzi wa vifaa hivyo, Mkuu wa mkoa wa Geita Said Magalula Said alisimama na kuwataka madiwani hao kukubali ununuzi wa vifaa hivyo.
“Hili suala inavyoonekana ni kwamba mlikwishalijadili na kulipatia maamuzi katika vikao vyenu vilivyopita, hilo ni moja lakini la pili, hata kama mtavinunua vifaa hivyo suala la mgawanyo wake halina tatizo,hili ni suala ambalo liko wazi na muda wa kufanya hivyo ukifika basi mtakaa na kulijadili tena…..’’ alisema Mkuu huyo wa Mkoa na kuwafanya Madiwani waliokuwa mstari wa mbele katika kupinga ununuzi wake kukaa kimya.
0 comments:
Post a Comment