Home » » Mashindano ya ulinzi shirikishi cup Geita yazinduliwa

Mashindano ya ulinzi shirikishi cup Geita yazinduliwa


Na David Azaria, Geita-Geita Yetu 
MAPEMA wiki hii Jeshi la Polisi mkoani Geita lilifanya Uzinduzi Mkubwa wa Mashindano ya Mpira wa Miguu  kwa vijana maarufu kwa jina la ‘ULINZI SHIRIKISHI CUP’,mashindano yanayotarajiwa kuanza wakati wowote Mkoani hapa. 
Uzinduzi huo ulifanywa na Kamanda wa Polisi Mkoani Geita Kamishna Msaidizi wa polisi Leonard Paul,kwanza kwa kuchagua kamati maalum itakayosimamia mashindano hayo kuanzia ngazi ya kata hadi Mkoa,lakini pili kwa kuandaa michezo ya ufunguzi kwa jumla ya vilabu sita vilivyorikisha vijana wenye umri wa chini ya miaka 14,17,na Vilabu vya watu wazima. 
Viongozi waliochaguliwa kuongoza kamati hiyo Kimkoa na Nafasi zao katika mabano ni Athanas Inyasi (Mwenyekiti-Mfanyabiashara),Paul Kasabago (Katibu Mkuu-Kaimu Kamanda wa polisi Mkoa wa Geita),Simon Kurwa (Mweka Hazina),na David Azaria (Katibu Mwenezi-Mwandishi wa Habari). 
Akizungumza na wadau wa Mpira wa Miguu katika mkoa wa Geita Kamanda Paul anasema Jeshi la polisi limekuwa katika kipindi cha Mpito katika harakati zake za kuwa karibu na wananchi (Jamii),ikiwa ni moja ya njia pekee na endelevu ya kupambana na uhalifu. 
Anasema harakati hizo zimepelekea kuanishwa kwa dhana ya polisi jamii ikiwa na maana ya kuishirikisha jamii katika ulinzi wao na mali zao ili hali polisi ikiwa ni mhimili katika kutoa utaalam wa namna ya kujilinda na kujihami na changamoto mbalimbali za kihalifu. 
Anasema moja kati ya vipengele vilivyomo ndani ya Polisi jamii ni uanzishwaji wa michezo kwa vijana kama njia ya kuwaondoa katika uhalifu (YOUTH SPORTS VS YOUTH CRIME) na kwamba hali hiyo inatokana na vijana kuwa kundi kubwa katika jamii kuliko kundi lolote na kwamba kutokana na tatizo la ukosefu wa ajira na utandawazi kama kundi hilo la vijana litaachwa linaweza kuwa janga kubwa katika jamii hapo baadaye. 
“Lengo la polisi kupitia dhana ya polisi jamii ni kuwezesha kushirikiana na jamii yote kwa ujumla kupitia michezo katika kuhakikisha kuwa vijana wengi iwezekanavyo wanashirikishwa ili kuwaondoa katika vijiwe vinavyopelekea wao kujiingiza katika masuala mbalimbali ya uhalifu……’’ anasema Kamanda Paul na kuongeza kuwa. 
“Uzoefu unaonyesha kuwa vijana ni wapenda michezo sana na hasa huu wa Mpira wa miguu hivyo ni wazi kabisa kwamba wakishirikishwa na kuwezeshwa ni wepesi na kuchukua hatua hivyo ni wazi kwamba itatusaidia sisi Jeshi la polisi katika kuzuia uhalifu…..’’. 
Anasema kwa kutumia michezo vijana watatumia muda mwingi katika michezo na kuwaondoa katika kutumia muda mwingi kwenye vijiwe jambo ambalo linapelekea wengi wao kujiingiza katika kuvuta Bangi, madawa ya kulevya na hata unyang’anyi ,jambo ambalo limekuwa likisababisha usumbufu katika jamii. 
Anabainisha kwamba kupitia michezo hiyo vijana walio wengi watakuwa katika makundi ya michezo badala ya kiuhalifu na kwamba vikundi hivyo vinaweza kutumika kama kama vikundi vya ushirika ambavyo vinaweza kupata misaada katika kuvifanya kuwa vya uzalishaji na hivyo kuwafanya kuondokana kabisa na uhalifu. 
Kwa mujibu wa Kamanda huyo dhana ya kuwaweka vijana na kuhakikisha kwamba wanakuwa pamoja kuna faida nyingi ikiwa ni pamoja na Kuwafanya vijana kujitambua kama sehemu ya jamii,kuwafanya vijana kuachana uhalifu,kuwafanya vijana kuwa katika vikundi vya uzalishaji badala ya uhalifu,na pia kuwafanya vijana kujipatia kipato kupitia vikundi vya uzalishaji. 
Anabainisha kuwa kazi kubwa ya kamati hiyo itakuwa ni kufanya maandalizi ya ligi hiyo kuanzia ngazi ya kata hadi fainali za mkoa,kutafuta zawadi pamoja na mahitaji mengine ya muhimu lengo kubwa ni kuhakikisha kwamba mashindano hayo yanatimiza malengo yaliyowekwa ambayo ni kupunguza kama si kuondoa kabisa vitendo vya uhalifu vinavyofanywa na vijana mitaani. 
“Ukichunguza kwa makini kule mitaani wale vijana wamekuwa wakijiingiza kwenye vitendo vya uhalifu kutokana na kutokuwa na kazi za kufanya, kuanzia asubuhi mpaka jioni utawakuta mitaani wakizurura tu, hawana kazi za kufanya na hili ni tatizo kubwa sana katika eneo hili, kuna tatizo la ukosefu wa ajira na hasa kwa vijana, hali hiyo ni lazima iwafanye washawishike kujiingiza katika vitendo vya uhalifu…..’’anasema Kamanda Paul. 
Kwa upande wake Mrakibu Mwandamizi wa Polisi Paul Kasabago anasema mashindano hayo yatawafanya vijana wengi ambao mara kwa mara wamekuwa wakijiingiza katika shughuli mbalimbali za kihalifu, kurejea katika michezo kwa sababu inaaminika kwamba michezo hutoa fursa kubwa kwa vijana katika kujiajiri na hivyo kupata mahitaji yao. 
Kasabago anasema mkoa wa Geita na hasa katika makao makuu ya Mkoa yaliyopo Mjinio Geita kwa sasa unakabiliwa na ongezeko la watoto wa mitaani, hali ambayo imekuwa ikisababisha kuwepo kwa ongezeko la vitendo vya uhalifu ambapo wengi wao wamekuwa vibaka katikati ya mji hali inayoletwa usumbufu kwa rai wema. 
Mkoa wa Geita unaundwa na jumla ya wilaya tano za Geita, Bukombe, Nyang’hwale, Mbogwe na Chato ambapo zaidi ya kata 100 zinatarajiwa kushiriki katika mashindano hayo ambayo yanatarajiwa kuanza mwishoni mwa mwezi huu. 
Wakizungumzia mashindano hayo wadau wanaounda kamati hiyo ya Mkoa wanasema yatasaidia kuwaondoa baadhi ya vijana walio wengi ambao tayari wamejiingiza katika matumizi mabaya ya dawa za kulevya hali ambayo imekuwa ikiwasababishia madhara mbalimbali. 

0 comments:

Post a Comment

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Geita Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa