Na David Azaria, Chato-Geita Yetu
TATIZO la kukatika kwa umeme linalowakabili wakazi wa wilaya za Chato mkoani Geita na Biharamulo mkoani Kagera juzi lilizua balaa katika halmashauri ya wilaya ya Chato kufuatia madiwani kususia kikao cha baraza la madiwani baada ya kupinga kusomewa taarifa ya mapato na matumizi gizani kutokana na kukatika kwa huduma ya umeme kwenye wilaya hiyo
Hatua hiyo ilijitokeza majira ya saa 1:55 usiku muda mfupi baada ya Kaimu mweka hazina wa halmashauri hiyo Fulunence Kishenyi kuwasilisha taarifa ya mapato na matumizi ya mwaka 2011/012 inayoishia Mei 31, mwaka huu kwa kutumia mwanga wa tochi ya simu ya nokia.
Baada ya mweka hazina kuwasilisha taarifa hiyo huku giza likiwa limetanda ndani ya ukumbi, mwenyekiti wa baraza hilo Charles Maisha aliwataka madiwani kuijadili taarifa hiyo kwa kutumia mwanga wa tochi za simu zao za mikononi, hatua iliyopingwa vikali na madiwani wa kambi ya upinzani (Chadema) wakiongozwa na mwenyekiti wao Chrispine Kagoma ambaye ni diwani wa kata ya Buseresere.
“Mheshimiwa mwenyekiti hatuwezi..kuendelea na kikao hiki sisi kambi ya upinzani,kwanza tunamashaka na taarifa ya mweka hazina,kutokana na mashaka haya na umeme umekatika tochi za simu hazitasaidia,kwa sababu hii taarifa inakasoro nyingi kwa hiyo hatuungi mkono kujadili gizani wengine hatuna simu zenye tochi’’alisema mwenyekiti huyo wa kambi ya upinzani.
Kagoma alisema hawawezi kujadili taarifa hiyo kwa tochi za simu na hivyo madiwani watano wa chadema na baadhi ya madiwani wa chama cha CCM kuungana na kambi ya upinzani na kujiondoa kwenye kikao hicho kwa kupinga agizo la mwenyekiti wao la kuwataka watumie tochi za simu Mkononi.
Aidha madiwani hao waliikataa taarifa ya mweka hazina kufuatia kutofautiana mapato ya ndani na matumizi,kutokana na Taarifa hiyo ya fedha kuonyesha kuwa fedha iliyokusanywa katika kipindi cha mwaka wa fedha 2011/12 kuwa ni shilingi Milioni 524 huku matumizi yakiwa shilingi Bilioni.1.2 hatua iliyopelekea madiwani hao kuhoji sababu ya mapato na matumizi kutofautiana.
Pamoja na madiwani hao kujiondoa kwenye kikao, madiwani wengine waliendelea kuijadili taarifa hiyo ambapo madiwani ambao hawakuwa na simu zenye tochi walilazimika kusogea kwa wenzao wenye tochi ingawa hawakuvumilia na hivyo ilipofika saa 2:30 usiku walianza kuondoka ukumbini mmoja baada ya mwingine akiwemo mkuu wa wilaya hiyo Rodrick Mpogolo kitendo kilichopelekea kikao hicho kuvunjika.
Kutokana na kikao hicho kuvunjika baadhi ya ajenda hazikujadiliwa ikiwemo taarifa ya ukimwi,kikao cha kamati ya maadili cha kujadili nidhamu ya watumishi na kufunga kikao kitendo ambacho kilimlazimu na mwenyekiti wa baraza hilo kunyanyuka na kuondoka bila kufunga kikao hicho.
Mwili wa mtuhumiwa wa ujambazi waharibikia chumba cha kuhifadhia maiti
Na David Azaria, Geita-Geita Yetu
MWILI mtu anayedaiwa kuwa ni Jambazi uliokuwa umehifadhiwa katika chumba cha kuhifadhia maiti katika hospitali ya wilaya ya Geita baada ya kuuawa na Polisi,unadaiwa kuharibika vibaya na hivyo kusababisha harufu mbaya katika chumba hicho na maeneo mengine yaliyo karibu na chumba hicho.
Kufuatia hali hiyo Jeshi la polisi Mkoani Geita limetoa wito kwa ndugu jamaa na marafiki kufika katika hospitali hiyo kwa lengo la kuuchukua mwili wa ili kuuzika, hata hivyo ikiwa ni siku ya tano sasa tangu mwili huo marehemu kuwasili katika chumba hicho hakuna ndugu wala rafiki ambaye amewasili kwa ajili ya kwenda kuutambua.
Kamanda wa Polisi Mkoani Geita Kamishna Msaidizi wa Polisi Leonard Paul alisema jeshi la polisi limelazimika kutoa wito kwa ngudu ama marafiki kujitokeza ili kuuchukua mwili huo na kwenda kuusitiri na kwamba endapo jambo hilo litashindika serikali italazimika kuuzika kama ambavyo imekua ikifanya kwa miili mingine inayokosa ndugu,jamaa na marafiki.
“Natoa wito kwa wananchi wa mkoa wa Geita huyu ni mkazi wa Geita anmbaye alikuwa akiishi pale Katoro,watu wanamfahamu na tunaamini kwamba anao ndugu,basi wajitokeze waje wauchukuwe mwili huu wakausitiri,lakini wakishindwa kwa sababu unaendfelea kuharibika hapa hospitalini,basi tutatoa amri ya kuuzika….sasa hapo wasije wakalalamika……’’alisema Kamanda Paul.
Kamanda Paul alitaja jina la Mwili wa mtu huyo anayedaiwa kuwa ni jambazi sugu kuwa ni Leonard Nana (30) ambaye ni mkazi wa Mji Mdogo wa Katoro ambaye anaelezwa kuhusika katika matukio kadhaa ya ujambazi wa kutumia silaha katika wilaya za Geita, Bukombe, Sengerema, Chato pamoja na maeneo ya visiwa mbalimbali vilivyoko ndani ya Ziwa Victoria.
Polisi walilazimika kumpiga risasi mtuhumiwa huyo ambaye alitaka kumpora Bunduki Mmoja wa Askari polisi waliokuwa wamekwenda kuwakamata ndani ya nyumba moja ya kulala wageni wakati wakigawana fedha pamoja na kupanga mikakati ya kufanya ujambazi.
Majambazi hao wanaodaiwa kufanya shambulizi la kutaka kumuua aliyekuwa Mkuu wa Kituo cha Polisi Katoro Thomas Mboya kwenye Baa Mkoani Geita, walitiwa mbaroni na Polisi huku Leonard akiuuawa kwa kupigwa Risasi baada ya kumrukia polisi kwa lengo la kutaka kumpora silaha.
Watuhumiwa hao walikamatwa Mwishoni mwa wiki iliyo katika mji Mdogo wa Buselesele wilayani Chato Mji ulioko mpakani kati ya wilaya za Geita na Chato umbali wa mita 100 kutoka katika Mji wa Katoro ambapo walifanya shambulio la kutaka kumuua Mkuu wa Kituo cha Katoro.
Kamanda Paul alisema siku ya tukio polisi wa kituo kidogo cha Buselesele wilayani Chato walipata taarifa kutoka kwa raia wema kwamba watuhumiwa hao waliokuwa katika Nyumba ya kulala wageni ya Nyamigogo walikuwa wakipanga njama za kwenda kufanya uhalifu.
“Baadhi ya raia wema waliopata kusikia mazungumzo ya watuhumiwa hao waliokuwa ndani ya nyumba hiyo walikwenda kutoa taarifa katika kituo cha polisi cha Buselesele ambao baadaye walifanya mawasiliano na wenzao wa kituo kidogo cha Katoro kwa kuwa viko karibu, ambapo jumla ya askari watano wakiwa na silaha walifika katika eneo hilo……’’ alisema Kamanda Paul nakuongeza.
“Walipofika walifanikiwa kuwakuta watuhumiwa ambao kwa wakati huo hawakuwa na silaha ya aina yoyote ambapo waliwaweka chini ya ulinzi na kuwakamata,hata hivyo mmoja wa watuhumiwa hao(Marehemu),aliamua kupamba na mmoja wa maaskari polisi kwa lengo la kumpora Bunduki hali iliyosababisha apigwe risasi kwenye mguu wa kushoto…….’’.
Alisema watuhumiwa hao walichukuliwa hadi kituo kikuu cha polisi cha wilaya ya Geita na kuwekwa ndani huku majeruhiwa aliyepigwa risasi akikimbizwa hospitali ya wilaya kwa matibabu, lakini alifariki Dunia baadaye.
Baada ya kuhojiwa na kupekuliwa iligundulika kuwa watuhumiwa hao ni raia kutoka nchini Burundi ambao aliwataja kwa majina ya Nsengiyumvua Elira (25), Eliye Habyarimana (28) wote wakazi wa Mkoa wa Ruyigi nchini Burundi pamoja na Mabula Lawrent ((29) mkazi wa kijiji cha Runzewe wilayani Bukombe Mkoani Geita.
Aidha uchunguzi wa kina uliofanywa na mwandishi wa Gazeti hili umebaini kuwa ngudu, jamaa na marafiki wa Marehemu wamekuwa waoga kujitokeza na kuuchukua mwili wa marehemu kwa kuhofia kukamatwa na polisi, kwa kuwa imebainika kuwa marehemu alikuwa ni jambazi sugu na kwamba alikuwa akimiliki Bunduki tano aina ya SMG ambazo kwa sasa zinasakwa na Polisi.
0 comments:
Post a Comment