Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo (wa pili kushoto) na Waziri wa Nchi
anayeshughulikia Madini wa Uganda, Lokeris Peter (kushoto) wakitembelea mgodi
wa Dhahabu wa Blue Reef uliopo Rwamgasa. Wa pili kutoka kulia ni Mkuu wa Mkoa
wa Geita, Mhandisi Robert Lughumbi na kulia ni mmiliki wa mgodi huo, Christopher
Kadeo.
Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo (kulia) akiongozana na Waziri wa Nchi anayeshughulikia masuala ya Madini nchini Uganda, Lokeris Peter (kulia kwake) mara baada ya kuwasili kwenye Mgodi wa Dhahabu wa Busolwa Gold Mine Project uliopo Nyarugusu.
Mawaziri kutoka Uganda wakiwa pamoja na mwenyeji wao, Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo walipotembelea mgodi wa Dhahabu wa Blue Reef uliopo Rwamgasa ili kujionea shughuli zinavyoendeshwa mgodini hapo.
Mawaziri kutoka Uganda wakimsikiliza mmiliki wa Mgodi wa Dhahabu wa Blue Reef, Christopher Kadeo (hayupo pichani) baada ya kutembelea eneo (shimo) linalochimbwa Dhahabu. Kutoka kushoto ni Waziri wa Nchi- Mambo ya Ndani, Obiga Kania, Waziri wa Nchi- Masuala ya Uchumi, Dkt. Kasirivu Atwooki, Waziri wa Nchi- Madini, Lokeris Peter na Waziri wa Nchi- Mamlaka ya Mji Mkuu wa Kampala, Namugwanya Bugembe.
Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo (wa nne kutoka kulia) akiwa katika picha
ya pamoja na Mawaziri kutoka Uganda mara baada ya kuwasili kwenye Ofisi ya
Mkuu wa Mkoa wa Geita.
Mawaziri
Wanne kutoka Uganda wakiongozwa na mwenyeji wao Naibu Waziri wa Madini,
Stanslaus Nyongo Agosti 29, 2017 walitembelea migodi ya dhahabu ya
Mkoani Geita inayomilikiwa na Watanzania. Miongoni mwa migodi
iliyotembelewa ni Mgodi wa Dhahabu wa Blue Reef uliopo Rwamgasa, Mgodi
wa Dhahabu wa Busolwa Gold Mine Project uliopo Nyarugusu na Kituo cha
Mfano cha Uchimbaji Madini ya Dhahabu cha Tan Discovery kilichopo
Rwamgasa.
Mawaziri
hao waliwasili nchini Tanzania Agosti 27, 2017 kwa ajili ya zira ya
siku mbili ya kujifunza juu ya Usimamizi wa Sekta ya Madini hususan
suala la Uendelezaji wa Uchimbaji Mdogo wa Madini. Kwa mujibu wa Naibu
Waziri Nyongo, Mawaziri hao wametembelea migodi hiyo ili kuona namna
gani migodi hiyo inaendesha shughuli zake na namna ambavyo serikali
imekuwa ikiwasaidia kuhakikisha wanakuwa na uchimbaji madini wenye tija.
“Wamekuja kujifunza, kuangalia Sera zetu, Sheria zetu na mchango wa
Serikali katika kuwasaidia wachimbaji wadogo,” alisema.
Alisema
walipendekeza kutembelea migodi inayomilikiwa na Watanzania ili
kujionea namna ambavyo wazawa wanavyoendesha shughuli za uchimbaji
madini ikiwa na pamoja na kuzungumza nao ili kupata uzoefu wa uendeshaji
wa shughuli husika na kubaini ushirikiano uliopo baina yao na Serikali.
Akizungumza
kwa niaba ya Mawaziri wa Uganda, Waziri wa Nchi anayeshughulikia Madini
wa Uganda, Lokeris Peter alisema Tanzania ni miongoni mwa nchi Barani
Afrika zilizopiga hatua kwenye usimamizi wa Sekta ya Madini hususan eneo
la Uchimbaji Mdogo wa Madini ikilinganishwa na nchi zingine
walizotembelea.
"Uamuzi
wa kufanya ziara nchini humu unafuatia uzoefu wa muda mrefu wa Tanzania
kwenye masuala ya uchimbaji wa madini hususan namna ambavyo Tanzania
imeweza kurasimisha suala la uchimbaji mdogo," alisema Waziri Peter.
Awali
kabla ya kuwasili Mkoani Geita, ujumbe huo wa Mawaziri kutoka Uganda;
Agosti 28, 2017 ulikutana na Waziri wa Madini, Angellah Kairuki ambapo
ulielezwa masuala mbalimbali yanayohusu sekta husika ikiwemo Sera,
Sheria na Kanuni za Madini pamoja na masuala yanayohusu Wachimbaji
Wadogo wa madini.
Mawaziri
kutoka Uganda waliofanya ziara hiyo ni Waziri wa Nchi- Madini, Lokeris
Peter, Waziri wa Nchi- Mambo ya Ndani, Obiga Kania, Waziri wa Nchi-
Mamlaka ya Mji Mkuu wa Kampala, Namugwanya Bugembe na Waziri wa Nchi-
Masuala ya Uchumi, Dkt. Kasirivu Atwooki.
0 comments:
Post a Comment