NDIVYO wanavyotania, eti ukitaka kushika wadhifa mkubwa katika
Serikali ya Kenya, basi oa mwalimu! Wanadai ndiyo `nyota’ mpya ya
madaraka ilikolalia.
Kisa? Kwa kuwa Margaret Kenyatta, mke wa Rais Uhuru Kenyatta
kitaaluma ni mwalimu, pia Rachel Ruto, mke wa Naibu Rais wa Kenya,
William Ruto ni mwalimu. Ukiachilia mbali hao, hata Ida Odinga, mke wa
Raila Odinga, Waziri Mkuu wa zamani wa Kenya ambaye mara mbili amemtoa
jasho Uhuru Kenyatta katika kuwania urais wa Kenya, naye ni mwalimu.
Margaret na Rachel walisomea ualimu katika Chuo Kikuu cha Kenyatta
wakati Ida alisoma katika Chuo Kikuu cha Nairobi. Hata Lucy Kibaki, mke
wa Rais wa Tatu wa Kenya, Mwai Kibaki naye alikuwa mwalimu kitaaluma.
Alifundisha katika Vyuo vya Ualimu Kamwenja na Kambui ambako alipanda
na kuwa Mkuu wa Chuo. Hata hivyo, baada ya kuolewa na Kibaki mwaka
1961, alifanya kazi kwa miaka miwili tu na baadaye kuachana na taaluma
hiyo.
Rais wa pili wa Kenya, Daniel Arap Moi ambaye wiki iliyopita, Agosti
22, alitimiza umri wa miaka 92, naye kitaaluma ni mwalimu. Mazingira ya
Kenya yanaonekana kutotofautiana sana na Tanzania, kwani chati ya walimu
katika kushika madaraka au kuwa wake wa viongozi wakuu imeonekana kuwa
juu.
Kuanzia Mkuu wa nchi, Rais Dk John Magufuli na Mkewe, Mama Janeth
Magufuli, kitaaluma ni walimu na wamefanya kazi ya ualimu. Vivyo hivyo
kwa Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa ni mwalimu kitaaluma kama ilivyo kwa
Mkewe, Mary Majaliwa.
Kwa Tanzania, Mama Magufuli si mke wa kwanza wa Rais kuwa mwenye
taaluma ya ualimu, kwani hata Rais wa Awamu ya Nne, Jakaya Kikwete,
mkewe Mama Salma Kikwete ni mwalimu kitaaluma.
Pia, hao si wa kwanza, kwani mjane wa Baba wa Taifa, Hayati Mwalimu
Julius Kambarage Nyerere, Mama Maria, naye kitaaluma ni mwalimu. Mama
Maria aliyezaliwa mwaka 1930 akiitwa Maria Waningu Gabriel Magige,
alisoma Shule ya Watawa Wakatoliki Nyegina, Musoma na Ukerewe mkoani
Mwanza.
Baadaye alijiunga na Chuo cha Ualimu Sumve. Alifundisha shule ya
Msingi Nyegina kabla ya kuolewa na Mwalimu Nyerere mwaka 1953. Aidha,
Rais wa Awamu ya Pili wa Tanzania, Ali Hassan Mwinyi aliyezaliwa miaka
92 iliyopita, alianzia ajira yake kwa kushika chaki katika Shule ya
Msingi Mangapwani ambako pia alisoma na kuhitimu elimu ya msingi.
Nchini Uganda, Rais wa nchi hiyo, Yoweri Museveni ingawa kitaaluma ni
mchumi na aliyebobea katika Sayansi ya Siasa, amewahi kufundisha Chuo
cha Ushirika Moshi, mkoani Kilimanjaro wakati Mkewe, Janeth Museveni, ni
mwalimu kitaaluma aliyesomea katika Chuo Kikuu cha Makerere. Kwa sasa
ndiye Waziri wa Elimu na Michezo wa Uganda.
CHANZO HABARI LEO
0 comments:
Post a Comment