Home » » UHAKIKI WA KUJA NA ORODHA SAHIHI YA WATUMISHI WA UMMA.

UHAKIKI WA KUJA NA ORODHA SAHIHI YA WATUMISHI WA UMMA.

NA HASSAN SILAYO-MAELEZO
Zoezi la uhakiki wa watumishi wa umma linaloendelea kwa sasa litasaidia kuja na orodha sahihi ya watumishi halali wa umma na kupunguza kabisa idadi ya watumishi hewa serikalini.

akiongea katika kipindi cha TUNATEKELEZA kinachoratibiwa na Idara ya Habari(MAELEZO) kwa ushirikiano na Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC) Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Dkt. Laurean Ndumbaro amesema kuwa zoezi hili limekuwa na mafanikio makubwa kwani litasaidia kubaini watumishi hewa na kuwatoa katika mfumo wa ajira kutokana na kuiingizia serikali hasara.

"Zoezi hili tunaloliratibu kwa sasa kwa ushirikiano na NIDA litasaidia kuwaondoa watumishi hewa serikalini ambao kwa takwimu imeonesha serikali ilikuwa ikilipa mabilioni ya fedha kwa waajiriwa hewa kutokana na kutokuwa na taarifa sahihi za watumishi wa serikali jambo ambalo litakoma siku chache zijazo kwa uwepo wa orodha sahihi ya watumishi wa umma" Alisema Dkt. Ndumbaro.

Dkt. Ndumbaro alisema kuwa baada ya kuliendesha kwa mafanikio zoezi hili linatarajiwa kumalizika ndani ya mwezi huu hivyo kuziwezesha taasisi za serikali kuwa na orodha sahihi ya watumishi wa umma hivyo zoezi la kuajiri litaendelea kama kawaida pia kuwaingiza katika mfumo waajiriwa wapya ambao ajira zao zilisitishwa kwa muda.

Aidha Dkt. Ndumbaro alisema kuwa baada ya zoezi hili serikali itajaza nafasi zote zilizowazi baada ya watumishi hewa kuondolewa katika mfumo wa ajira serikalini

Wakati Huohuo Dkt. Ndumbaro amesema kuwa upandishaji vyeo kwa watumishi wote wa umma utazingatia utendaji kazi wa mhusika katika eneo lake na kazi.

Naye Naibu Katibu Mkuu wa Ofisi hiyo Bi. Suzan Mlay amewataka viongozi wa serikali kutumia lugha nzuri kwa waliochini yao ikiwamo kufuata kanuni sheria na taratibu za kiutumishi katika kutekeleza majukumu yao.

0 comments:

Post a Comment

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Geita Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa