· Pampu yadaiwa kupelekwa Morogoro, yeye asema iko kijijini
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amemsimamisha kazi Mhandisi wa
Maji wa Wilaya ya Chato, Bw. Peter Ngunura kwa kosa la kumdanganya mbele
za watu na kumpa taarifa za uongo juu ya pampu ya maji iliyodaiwa
kupelekwa Morogoro.
Waziri Mkuu alitoa agizo hilo jana jioni (Jumatano, Machi
16, 2016) alipokuwa akiwahutubia mamia ya wakazi wa mji wa Chato
waliojitokeza kumsikiliza kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye
uwanja wa michezo wilayani Chato, mkoani Geita.
Waziri Mkuu ambaye amewasili mkoani Geita kwa ziara ya siku
mbili akitokea mkoani Kagera, alisimamishwa na wakazi wa kijiji cha
Kalebezo, kata ya Nyamirembe, wilayani Chato na kukuta mabango
yaliyokuwa yakidai maji safi na kuelezea uharibifu wa pampu ya maji.
Katika maelezo yao, wakazi hao walimweleza Waziri Mkuu
kwamba mradi wa maji kwenye kata hiyo ulishakamilika lakini pampu yao
imechukuliwa na kupelekwa Morogoro jambo lililosababisha wakose maji kwa
muda mrefu.
Kwa
sababu alikuwa hajafika Chato mjini na hakuwa na
taarifa sahihi za mradi huo wa maji, Waziri Mkuu aliwaeleza wakazi hao
kwamba analibeba jambo hilo na atafuatilia hadi aelezwe ni kwa nini
pampu hiyo imepelekwa Morogoro. Akiwa kwenye mkutano wa hadhara, ndipo
suala la maji likaibuka tena na Waziri Mkuu kuamua kuchukua hatua hiyo.
“It’s unethical (ni kinyume cha maadili) kumdanganya
kiongozi wako. Nimekuuliza mara mbili mbili kama una uhakika kuwa pampu
hiyo ipo ukasema una uhakika kuwa ipo. Nimemtuma diwani na vijana wangu
wakacheki wakasema hakuna pampu,” alisema Waziri Mkuu na kumwita Diwani
huyo jukwaani ili atoe majibu.
“Pale
kulikuwa na pampu mbili; moja ni ya kuvuta maji kutoka kwenye kina
kirefu na kuyapeleka kwenye pump house na nyingine ni ya kuvuta maji
kutoka kwenye pump house
na kuyapeleka kwenye tenki kubwa la kuhifadhia maji. Ile ya kutoa maji
kwenye kina kirefu ndiyo haipo, wataalamu wanajua wameipeleka wapi,”
alisema Bw. Charles Manoni ambaye ni diwani wa kata ya Nyamirembe ambayo
kijiji cha Kalebezo kimo.
Waziri Mkuu alisema ahadi ya Serikali ya awamu ya Tano ni
kuwatumikia wananchi kwa uadilifu. “Lazima watumishi wa umma wabadilike
na kuanza kuwatumikia wananchi kwa dhati. Hatuwezi kuwa na watumishi
waongo ambao wanamdanganya hata Waziri Mkuu.”
“Kuanzia sasa, Engineer atakaa pembeni, polisi na TAKUKURU
wamchunguze. Asitoke Chato hadi uchunguzi ukamilike. Nataka kujua nani
alichukua hiyo pampu na kwa kibali gani. Tukijiridhisha atarudi lakini
kwa sasa hivi akae kando,” alisema.
Mapema jana mchana, akizungumza na viongozi
mbalimbali wa mkoa wa Geita na wilaya ya Chato mara baada ya kupokea
taarifa zao kwenye ukumbi wa Halmashauri, Waziri Mkuu alimpa fursa
Mhandisi huyo aeleze nini kimetokea kuhusu pampu inayodaiwa kupelekwa
Morogoro lakini akakanusha na kudai kuwa ipo palepale kijijini.
“Una uhakika na hayo unayoyasema? Hiyo pampu ipo kweli
kijijini? Nikienda nitaiona?” alihoji Waziri Mkuu na kujibiwa mara mbili
na mhandisi huyo kwamba ana uhakika asilimia 100 kwamba pampu ipo na
wala haijaenda Morogoro.
Alipotaka kujua ni kwa wananchi wa kijiji kile hawana maji
kutokana na ubovu wa pampu hiyo, alijibiwa kwamba mradi ule ulikuwa
chini ya mamlaka ya maji ya mji wa Bukoba (MBUWASA) ambako wilaya hiyo
ilikuwepo zamani kabla ya kuhamishiwa kwenye mkoa mpya wa Geita mwaka
2012.
Mhandishi huyo alisema amekuwa akifuatilia fedha za
matengenezo kutoka kwa Mkurugenzi wa MBUWASA bila mafanikio, ndipo
Waziri Mkuu akamuagiza aende nje ya ukumbi huo akapige simu na kumletea
majibu ni lini fedha hizo zitapatikana ili wananchi wa kijiji kile
waendelee kupata maji.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU
ALHAMISI, MACHI 17, 2016.
0 comments:
Post a Comment