Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
SERIKALI imetenga jumla ya Sh bilioni 811 zitakazotumika kutekeleza
ahadi ya Rais John Magufuli ya kukipatia kila kijiji Sh milioni 50 kwa
ajili ya shughuli za maendeleo. Imeelezwa kwamba serikali imeshaanza
kushirikisha wadau mbalimbali kupata maoni ya jinsi ya kuendesha mpango
huo kwa ufanisi na tija.
Katibu Mtendaji wa Baraza la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi (NEEC)
alisema serikali itaanza kutoa fedha hizo kuanzia mwaka wa fedha ujao.
Alikuwa akizungumza na waandishi wa habari mwishoni mwa wiki baada ya
mkutano wa wadau waliokuwa wanajadili rasimu ya mpango huo wa utoaji
fedha kwa ajili ya maendeleo.
Mkutano huo ulihudhuriwa na wawakilishi wa halmashauri za wilaya,
Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF),
mabenki, mifuko ya hifadhi ya jamii na vikundi mbalimbali. “Kwa kuanzia,
fedha hizo zitatolewa kwa awamu tatu katika kipindi cha miaka mitano,”
alisema.
Alisema fedha hizo zitatolewa kupitia benki kabla ya kutolewa kwa
vikundi mbalimbali kama Vicoba, Saccos na vikundi vingine kulingana na
taratibu zitakazowekwa. Alisema mpango utaanza na mikoa 10 iliyo nyuma
katika kutumia huduma za kifedha kwa kuzingatia taarifa ya utafiti ya
Finscope ya mwaka 2013.
Mikoa hiyo ni Singida, Lindi, Mtwara, Mbeya, Shinyanga, Geita,
Kagera, Dodoma, Rukwa na Ruvuma. Akifungua mkutano huo, Waziri wa Nchi,
Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Uhusiano ya Bunge, Kazi, Ajira, Vijana na
Walemavu, Jenista Mhagama, alisema mkutano huo ulilenga kupata maoni ya
wataalamu ya namna bora ya kuutekeleza.
Akizungumza kwa niaba ya Waziri, Kaimu Mkurugenzi, Maendeleo ya Sekta
Binafsi, Uwekezaji na Uwezeshaji, Ofisi ya Waziri Mkuu, Victor
Mwainyekule alisema mawazo yaliyopatikana yatazingatiwa kuboresha mpango
huo unaolenga kupambana na umaskini.
Mkuu wa Uendeshaji, Benki ya Wanawake (TwB), Zablon Yebete alisema
mpango huo ni uwekezaji mkubwa kwa Watanzania unaopaswa kuungwa mkono na
vyombo vya fedha na wadau wengine nchini.
“Tunatakiwa kuunga mkono mpango huu unaohusisha vyombo vya fedha
katika utekelezaji wake kwa faida ya taifa,” alisema. Kwa mujibu wa
mpango huo, walengwa watapatiwa mafunzo ya ujasiriamali kabla ya
kupatiwa fedha hizo.
Chanzo Gazeti la habari leo
0 comments:
Post a Comment