Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399
KATIKA hali isiyokuwa ya kawaida na kushangaza wanafunzi wa shule
ya Sekondari Kivukoni katika halmashauri ya mji wa Geita Mkoani hapa
wamepewa adhabu ya viboko wakilazimishwa kuchangia sherehe ya kuhitimu
elimu ya Sekondari.
Wakizungumza na Tanzania Daima, wanafunzi hao ambao waliomba
kuhifadhiwa majina yao kwa sababu ya usalama wao shuleni hapo walisema
uongozi wa shule hiyo umetoa agizo la kila mwanafunzi kulipa shilingi
elfu tano kila mmoja kwa ajili ya mahafali hayo.
Wanafuzi wanaosoma kidato cha kwanza hadi cha tatu walishangazwa pia
wao kulazimishwa kuchangia sherehe hiyo kwa nguvu wakati ilipaswa kuwa
hiari.
"Juzi sisi wanafunzi wa kidato cha tatu tuliitwa na walimu wale ambao
tulikuwa hatujalipa tulichapwa viboko vitano kila mmoja tukiambiwa
tumegoma kutoa mchango huo," alisema mwanafunzi mmoja na kuongeza.
"Sasa hivi kila mwalimu anapoingia darasani tunaitwa majina wale
ambao hatujachanga tunapigwa viboko bila huruma tunawaaambia hatuna
pesa tunaongezewa adhabu ya viboko vingine," alisema.
Pia walisema pamoja na kuchapwa viboko walitakiwa kuandika barua za
kujieleza kisha kupelekwa kwa mkuu wa shule huku wakitishiwa
kufukuzwa.
Alipotafutwa kuelezea juu ya tuhuma hizo kaimu mkuu wa shule hiyo
ambaye alikataa kata kata kutaja jina lake alisema hajui suala hilo
wala kuwepo kwa mchango wa aina hiyo shuleni.
Alipoulizwa kuhusu wanafunzi kupewa adhabu wakikataa kutoa michango
alikubali kwa kusema aliyetoa idhini hiyo ni mkuu wa shule.
Ofisa Elimu wa Halmashauri ya mji wa Geita, Cosmas Kibiti, alisema
kisheria inatakiwa michango iwe imekubaliwa na vikao halali kisha
kuwepo na muhtasari wa vikao tofauti na hapo ni kosa
Chanzo:Tanzania Daima
0 comments:
Post a Comment