Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
Wiki iliyopita nilitoa mawazo yangu kuhusu wagombea urais na
kuwashauri vijana wajitokeze kwa wingi. Kwa kujenga hoja nilitoa mifano
ya viongozi watatu mashuhuri waliokuwa viongozi katika mataifa yao na
kuonyesha jinsi walivyofanya harakati za siasa na uongozi wangali bado
wabichi.
Nimepata maoni mengi, yapo yaliyounga mkono mawazo
yangu na yapo ambayo hayakuunga mkono na kutoa mifano ya viongozi na
marais walioingia madarakani wakiwa na umri mkubwa, ambao wameongoza
vizuri mataifa yao.
Sina ubishi juu ya hilo, lakini wazo langu
lilikuwa na dhamira ya kuwahamasisha vijana wajitokeze kugombea, haikuwa
dhamira yangu kuwavunja moyo wazee, wala hakuna sehemu niliyodadavua
kwa kusema kuwa wazee hawafai kuwa viongozi, bali nilishauri tu kwamba
ingefaa wao wabaki kama washauri.
Mjadala wa umri wa kuongoza ni mpana na kila mtu
anayo haki ya kutoa mawazo yake na kuamini anavyoamini. Lakini binafsi,
bado naamini kuwa kumpa kijana fursa ya kuongoza siyo jambo baya kwani
tumewaona vijana walioongoza na kufanya mambo makubwa tu na ukweli wa
fikra mpya, kasi mpya na ari mpya bado unabaki paleple, ingawa siyo
lazima kila kijana awe na fikra mpya kwani wapo vijana waliotawaliwa na
ukale na uhafidhina.
Ipo dhana inayojitokeza siku hizi kuwa ‘uongozi si
majaribio,’ wakati kina Julius Nyerere, Patrice Lumumba wa Kongo, Kwame
Nkrumah wa Ghana, Keneth Kaunda wa Zambia, Jomo Kenyatta wa Kenya na
wengineo waliposhika hatamu za uongozi, hawakuwa na uzoefu wowote zaidi
ya ule wa vitabuni na ule uchungu waliokuwa nao wa kunyonywa,
kunyanyaswa na kudhulumiwa.
Hawa walikuwa vijana na waliweza kuyahamisha
mataifa yao kutoka hatua moja kwenda nyingine. Kweli walifeli, walikwama
na walikosea kwa namna moja ama nyingine katika uongozi wao, lakini
yapo pia waliyoyafanya tena kwa ufanisi wa kupigiwa mfano.
Bila shaka ujana na fikra mpya siyo sifa pekee za
mtu kuwa kiongozi, ipo sifa moja ambayo imekuwa ikifanikisha zaidi
katika masuala ya kukusanya watu, kusikilizwa na kufuatwa; hii ni sifa
ya mvuto (Charsma). Kiongozi mzuri ni yule mwenye mvuto, anayependeka.
Kiongozi wa namna hii hata akikosea, hadhira huwa iko tayari kumsamehe.
Ipo mifano ya viongozi hao, mathalan Mwalimu Nyerere, Nelson Mandela,
Martin Luther King, Seif Sharif Hamad kwa kuwataja wachache.
Kadhalika, wapo viongozi waliokuwa na mvuto,
lakini kwa sababu moja au nyingine katika mchakato wa uongozi wakapoteza
mvuto wao, mathalan, Augustine Mrema, Christopher Mtikila na wengineo.
Vilevile wapo viongozi waliochaguliwa kutokana na haiba zao, mathalan
Jakaya Kikwete, Barack Obama, Andry Rajolina, Mfalme Mswati wa pili na
wengineo.
Wapo marais wanaopendwa na watu wao kutokana na
vituko vyao, mathalan Jacob Zuma, huyu kuna wakati alipata kupendwa sana
na jamii kubwa ya Afrika Kusini kutokana na kuendekeza mfumodume.
Wakati aliposhiriki ngono na dada anayedaiwa kuwa
alikuwa na Virusi Vya Ukimwi (VVU), bila kutumia kinga, Zuma alisema
kuwa alipomaliza tu kujamiiana alioga, hivyo haiwezekani kuwa
aliambukizwa virusi.
Sifa za rais ni nyingi, kwani hata Benjamin Mkapa
aliyekuwa mkali, makini na wakati mwingine mbabe, aliweza kuongoza kwa
kiasi chake mpaka hivi leo wapo wadadavuaji wanaoona kuwa alikuwa ni
rais mzuri kutokana na misimamo na umakini wake.
Ila ni wazi kuwa Watanzania wanahitaji rais mwenye
mawazo mapya, makini, mchapakazi, anayechukia rushwa, ambaye
atahakikisha kwamba inapungua kwa asilimia 90 au inatokomezwa kabisa.
Watanzania wanahitaji rais atakayelitoa taifa hapa lilipo na kulifikisha
katika hatua nyingine ya maendeleo.
Tunataka kiongozi mwenye visheni inayotekelezeka, anayeweza
kuyageuza mawazo kuwa vitendo. Tunataka kuiona Tanzania iking’ara kama
Singapore, Malaysia, Korea ya Kusini na nchi nyinginezo, ambazo katika
miaka ya 60 uchumi wake ulikuwa mdogo, lakini hivi sasa zina uchumi
mkubwa na maendeleo ya kuridhisha.
Mara nyingine hizi kelele tunazopiga (za kisiasa)
zinasababishwa na kutoridhika na uongozi uliopo. Uongozi wa wamba ngoma,
ngozi huvutia kwao. Wanataka viongozi wanaogawa majukumu na
kuyafuatilia, viongozi wasioridhika na maneno, viongozi wachapakazi,
viongozi wanaoufanya wizi kuwa ni mwiko kwao.
Rais aliye katika taswira ya Watanzania walio
wengi ni asiye mbinafsi, atakayelinda masilahi ya watu wa taifa hili,
rais asiyeyumbishwa na wabangaizaji, mapapa na manyangumi ya rushwa na
ufisadi. Rais atakayelinda mali na dhamana za Watanzania.
Rais mwenye pupa ya maendeleo, rais asiyelala
usingizi akikumbuka kuwa mamia kwa maelfu ya Watanzania hawana maji safi
na salama, maelfu umeme haujawafikia, hawapati huduma bora za afya na
mamilioni ya watoto na vijana hawapati elimu yenye manufaa.
Rais atakayeumwa na njaa inayowakabili Watanzania,
atakayetamani mkate anaokula yeye Ikulu wale watu wake wote, pengine
rais huyu ni wa kusadikika, lakini Waswahili husema:
“Fikra njema hujenga,” hivyo rais aliye katika
fikara za Watanzania ni rais mwenye sifa zote nzuri, lakini kubwa ni
kuwa aumwe na shida za Watanzania, awaondoe katika umaskini walio nao,
awatoe katika dhuluma zinazowakabili na awafutie ujinga uliotawala
vichwani mwao na kuwakinga na adui maradhi.
Hizo ni dhamira tulizokuwa nazo kabla ya uhuru na
hadi sasa zitaendelea kuwa ndizo vipaumbele vyetu kama taifa, rais
atakayeweza kutimiza hayo, ndiye atakayetufaa, awe kijana, mzee au
kikongwe. Rais Robert Mugabe ni kikongwe, lakini bado anaendelea
kupendwa na Wazimbabwe walio wengi kwa sababu moja tu kubwa; hajaacha
kutoa matumaini kwa wananchi wake iwe kuna jua ama mvua
Chanzo:Mwananchi
0 comments:
Post a Comment