Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
Utalii wa kiutamaduni bado ni nadharia changa katika nchi za
ulimwengu wa tatu ikiwemo Tanzania,kwa kuwa nchi hizo zimezoea kuona
utalii wa asili wa kutembelea mbuga za wanyama.
Siku za nyuma vivutio vya utalii wa kiutamduni
kama vile majengo ya kale,maeneo ya kihistoria na makumbusho hayakupewa
mtazamo wa kiuchumi zaidi.
Maeneo hayo yalipewa mtazamo wa kielimu zaidi na
kuundwa Idara ya Mambo ya Kale na Idara ya Makumbusho ambazo zote awali
zilikuwa katika wizara ya elimu na utamaduni ambavyo viliwekwa kama
vyanzo vya elimu zaidi kuliko vyanzo vya utalii.
Mabadiliko katika ulimwengu mzima ndiyo
yaliyosukuma kuwepo kwa utalii wa kiutamduni na nchi zilianza kutoa
kipaumbele katika utalii wa kiutamaduni ndiyo maana hapa nchini idara za
mambo ya kale na makumbusho zilihamishwa kutoka Wizara ya Elimu na
kuingia Wizara ya Utalii na Maliasili.
Hata hivyo ni vigumu kutenganisha utalii asili na
utalii wa kiutamduni kutokana na aina hizo mbili za utalii kuwa na
mahusiano ya karibu,Mtalii anapokwenda kutembelea utalii wa asili kama
mbuga za wanyama pia anaweza kupita katika maeneo yenye utalii wa
kiutamaduni na kununua bidhaa mbalimbali za kiutamaduni.
Wananchi, katika utalii wa utamaduni, wanaweza
kunufaika kuanzia kiwango cha familia, mtaa, kitongoji, kijiji, wilaya,
mkoa na kitaifa kwa hiyo utalii wa kiutamaduni unatoa fursa kubwa ya
ukuaji wa uchumi kuanzia kwa mtu binafsi hadi kwa taifa.Utafiti umebaini
kuwa utalii wa kiutamaduni unaweza kubadilisha kiwango cha maisha ya
watu kutokana na kupata kipato kinachoweza kuwaongezea kipato cha ziada
katika mapato yao.
Kwa mfano kabila la wamasai katika msimu wa utalii
wa kiutamaduni wanapata mapato karibu shilingi 30,000 kwa siku kutokana
na aina hiyo ya utalii.
Utafiti umebaini kuwa kofia inayotengenezwa kwa
ukindu inauzwa kati ya Sh3,500 hadi 5,000, mkanda unaotengenezwa kwa
ngozi yenye shanga unauzwa kati ya Sh5,000 hadi 10,000 na kinyago cha
kuchongwa kinauzwa kuanzia Sh20,000 hadi 500,000 kutegemea na ukubwa wa
kinyago hicho.
Utalii wa kiutamaduni una nafasi kubwa ya
kuchangia uchumi wa watu binafsi kwa sababu utalii unatengeneza ajira za
moja kwa moja na ajira ambazo sio za moja kwa moja na hivi sasa
Watanzania wengi wamejiajiri katika shughuli za utalii wa kiutamduni kwa
kufungua maduka ambayo wanauza vitu vya kitamaduni vyenye bei kubwa
zaidi katika soko la utalii.
Watu wanaonufaika katika sekta ya utalii wa
kiutamduni kutoka katika migongo ya watu wengine ni pamoja na watu wenye
hoteli, nyumba za kulala wageni, watu wanaouza maji na vyakula
mbalimbali.
Hivi sasa kuna nchi nyingi ambazo zimekuza uchumi
wake kwa haraka kupitia utalii wa kiutamaduni zikiwemo Australia,
Ujerumani, Uingereza pamoja na nchi nyingine nyingi za ulaya ambazo
kutokana na ukosefu wa mbuga za wanyama zimeamua kuendeleza utalii wa
kiutamaduni zaidi kuliko utalii wa asili na kupata maendeleo makubwa
kupitia aina hiyo ya utalii.
Sekta ya utalii nchini ni mhimili wa maendeleo ya
uchumi kwa kuwa ina mchango mkubwa katika pato la Taifa kwa kuchangia
wastani wa asilimia 17.
Endapo Sekta hii itasimamiwa vizuri na uendelea kupewa
kipaumbele na Serikali ni dhahiri kwamba uchumi wa Taifa utaimarika na
kupunguza tatizo la umaskini nchini.
Albano Midelo ni mwandishi mwandamizi anayeandikia masuala ya maendeleo,madini,mafuta na gesi
Chanzo:Mwananchi
Chanzo:Mwananchi
0 comments:
Post a Comment