NA,MWANDISHI WETU GEITA
Jitihada za
jeshi la Polisi mkoani Geita,kuimarisha ulinzi ukiwemo ulinzi shirikishi jamii
zimezidi kugonga mwamba,kutokana na mkoa huo kuzidi kukumbwa na matukio ya
uharifu kama ujambazi,mauaji ya vikongwe na ubakaji.
Kushindwa kufanikiwa kwa ulinzi huo ni kutokana na mfululizo
wa matukio 8 yaliyotokea katika kipindi kisichozidi mwezi mmoja yakifuatiwa na
tukio lililotokea jana,Mtaa wa Shilabela kata ya Kalangalala mjini Geita baada
ya mlinzi wa Vibanda vya Biashara Juma Suguta(40) kuuawa na watu wasiojulikana.
Mlinzi huyo ambaye ni mkazi wa Mtaa jirani wa Moringe mjini
hapa,aliuawa usiku wa kumkia jana kwa kuchinjwa shingo kisha wauaji kufungua
kibanda kimoja wapo cha Mwalimu Jackson Mayunga wa shule ya Gold Valley ingawa hawakuchukua
kitu chochote.
Kamanda wa polisi mkoani Geita,Joseph Konyo alithibitisha
kutokea kwa tukio hilo na kusema kuwa juhudi za kuwasaka wauaji hao
zinaendelea.
‘’Tukio lipo na OCD(Mkuu wa Polisi wilaya),na OC-CID(Mkuu wa
Upelelezi),nimewapa maelekezo ya kuhakikisha
wahusika wa mauaji hayo wanatiwa mbaroni’’alisema Kamanda Konyo.
Aidha taarifa kutoka eneo la tukio hilo zilizothibitishwa na
ofisa mtendaji wa kata ya Kalangalala,Hamad Husein aliyefika eneo hilo mapema
ni kwamba mlinzi huyo amekutwa amekufa huku akiwa amelazwa kifudifudi na
walipomgeuza alionekana akiwa amechinjwa shingo huku akiwa amepingwa kitu
kizito kichwani.
‘’Huyu mlinzi nilikuwa namfahamu sana,ni rafiki yangu wa
karibu taarifa zake nimezipata asubuhi ya saa 12 nilipigiwa simu lakini
nilipofika eneo la tukio nimeona damu nyingi zikiwa zimetapakaa,Tulipomgeuza
alikuwa amechinjwa shingo na kwamba wauaji hawakuchukua kitu chochote’’alisema
Mtendaji Hamad.
Tukio hilo ni la pili kutokea katika kipindi kisichozidi
mwezi mmoja baada mlinzi wa Kampuni ya ulinzi ya Geita(GSG),Kulwa Kanuka(38)kuuawa
kikatili Aprili 4,mwaka huu kwa kuchinjwa shingo na watu wanaodaiwa kuwa ni
majambazi kisha kumnyofoa sehemu zake za siri na kumtoboa macho.
Mlinzi huyo aliuawa akiwa lindoni mtaa wa Mbugani na kwamba
wauaji walivunja kibanda cha M-pesa na kuchukua sh.45,000 pamoja na viti vine vya
Plastiki.
Mbali na tukio hilo mkoa wa Geita umezidi kukumbwa na
matukio ya mauaji ya vikongwe ambapo katika kipindi hicho vikongwe wane wameuawa
na majina ya vijiji katika mabano ni Kulwa
Kapalata(67)(Katoma),Joyce Dotto(70)(Butundwe)Yombo Petrol(50)(Kanyala),na
Kabula Yohana(60)(Kagu).
Hata hivyo matukio hayo yamefuatiwa na tukio la kusikitisha
lililotokea Mei 2,mwaka huu,baada ya mwanafunzi wa darasa la pili shule ya
msingi Kalangalala mjini Geita,kubakwa hadi kufa na mtu alimvamia ndani akiwa
amelala huku mama yake mzazi akiwa kazini kwenye uhudumu wa baa.
Kufuati kuwepo kwa mfululizo wa matukio hayo wakazi wa mji
wa Geita wameomba mkoa huo kuwa na kanda maalumu ya kipolisi ili kuthibiti
uharifu ambao umeleta hofu kwa wakazi hao.
0 comments:
Post a Comment