Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
TUHUMA za ubadhirifu na uporaji wa ardhi zinazowakabili baadhi ya
watendaji wa halmashauri na kijiji, zimewasukuma wananchi wa Kijiji cha
Bugulula, Kata ya Bugulula wilayani Geita kufunga ofisi ya serikali ya
kijiji hicho.
Baadhi ya tuhuma zilizowafanya wanakijiji hao kufunga ofisi yao ni
pamoja na ujenzi mbovu wa msingi wa zahanati ya huduma ya mama na mtoto
uliogharimu kiasi cha sh milioni 36, wakati tayari ukiwa umeweka
nyufa.
Wananchi hao zaidi ya 250 walisema viongozi wa serikali ya kijiji
hicho wameshirikiana na baadhi ya watendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya
Geita kuhujumu kiasi hicho cha fedha kwa kumpa kazi ya ujenzi wa jengo
hilo mkandarasi ambaye ujenzi wake uko chini ya kiwango.
Mmoja wa wananchi hao aliyeomba jina lake lihifadhiwe, alisema ujenzi
mbovu wa msingi wa jengo hilo ni aina nyingine ya kielelezo cha
kukithiri kwa ufisadi unaofanywa na baadhi ya watendaji wa serikali na
halmashauri ya wilaya hiyo.
Mmoja wa kina mama wa kijiji hicho ambaye pia aliomba jina lake
lisitajwe gazetini, akizungumza kwa uchungu alisema: “Tunapata shida
sana kina mama wakati wa kujifungua, ukipatwa na uchungu inabidi uende
Geita ambako ni mbali, hivyo tulijua jingo hilo ndiyo mkombozi wetu.”
Hata hivyo, viongozi na watendaji kadhaa wa serikali ya kijiji na
halmashauri wametupiana mpira, kila mmoja akielekeza lawama kwa
mwingine.
Wakati Diwani wa Kata hiyo, Elisha Lupuga ambaye pia ni Mwenyekiti wa
Halmahauri ya Wilaya ya Geita akipuuza malalamiko ya wananchi hao na
kudai kuwa hakuna malalamiko yoyote ya msingi, bali kundi la vijana
vijana wachache waliopandikizwa kufanya fujo katika kijiji hiki,
Mwenyekiti wa Serikali ya Kijiji, Bahati Matitu, alikiri ujenzi duni wa
msingi wa jengo.
“Ni kweli msingi una ufa na tayari mkandarasi tulimwambia na anakuja kuurekebisha ili atukabidhi,” alisema Matiku.
Hata hivyo, taarifa ya halmashauri iliyosomwa katika kikao cha baraza
la madiwani mapema mwaka huu, imeonyesha kuwa ujenzi wa msingi huo
umekamilika kwa asilimia mia moja na tayari umekabidhiwa.
Mkandarasi aliyejenga msingi huo, Kenedy Kubuka kutoka Kampuni ya
J.V.K alipoulizwa kuhusiana na tuhuma hizo, alikiri kuwepo na dosari
katika ujenzi.
“Ni kweli sisi ndio tunajenga jingo hilo, lakini ujenzi unaendelea na
bado sijamaliza na kuanzia wiki ijayo nitakamilisha pale palipobaki na
ndiyo maana sijakabidhi rasmi,” alisema Kubuka.
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Geita, Ali Kidwaka alipohojiwa
sababu za kulipwa kwa fedha hizo wakati ujenzi umefanyika chini ya
kiwango, alijibu kwa kifupi: “Sijui kama kuna msingi unajengwa katika
kijiji hicho na kama upo nitafuatilia ili nijue zaidi.”’
Hata hivyo, uchunguzi umebaini kwamba mkandarasi huyo amelipwa tu nusu ya sh mil 36.
Chanzo:Tanzania Daima
0 comments:
Post a Comment