SIKU chache baada ya watu watatu kufariki dunia katika eneo la
Kukuruma pit linalomilikiwa na mgodi wa dhahabu wa Geita Gold Mine (GGM)
kwa kuangukiwa na kifusi cha udongo, Ofisa Madini Mkazi wa Geita,
Injinia Sementa Haruna, amesema eneo hilo hawapaswi kuwepo wachimbaji
wadogo wadogo kwani lina leseni ya GGM ya mwaka 1999.
Sementa amewataka wachimbaji hao kwenda kwenye maeneo yao
waliyotengewa na serikali yaliyopo Isamilo na Lwenge kuliko kuendelea
kuwavamia wenye leseni.
Alitoa kauli hiyo alipozungumza na wachimbaji hao waliopo eneo
hilo, ambao walisema wapo hapo kwa sababu eneo hilo ni la serikali
baada ya mgodi wa GGM kumaliza kuchimba.
Mmoja wa wachimbaji hao, Joram Mtunga, alisema zaidi ya watu 1,000
waliopo hapo wanategemea kuendesha maisha yao na kusomesha watoto.
Alisema katika eneo hilo dhahabu inapatikana kirahisi tofauti na maeneo mengine kama ya Samina na Magema.
Mtunga alisema na kuongeza kuwa kitaalamu dhahabu ya Kukuruma ina
asilimia 100 yaani ni nzuri tofauti na kwingineko ndiyo maana watu huku
wapo wengi tofauti na kwingine.
Kuhusu suala la usalama wao maeneo hayo, walidai yanayotokea ni kwa
bahati mbaya, kwani kila sehemu penye machimbo hujitokeza matatizo
hayo, hivyo kuiomba serikali isiwaondoe.
Ofisa Mahusiano wa GGM, Tenga Tenga, alisema eneo hilo ni mali ya mgodi wao, hivyo ni vema liachiwe ili kazi ziendelee
Chanzo;Tanzania Daima
0 comments:
Post a Comment