ASKOFU wa Kanisa la Habari Njema mjini hapa, Tryphone John,
amenusurika kwenda jela baada ya kulipa faini ya sh 30,000 baada ya
kupatikana na hatia ya gari lake kumgonga mwendesha pikipiki, Mandikilo
Baluhya (42) na kumsababishia ulemavu wa kudumu.
Hukumu hiyo ilitolewa juzi katika Mahakama ya Wilaya ya Geita baada
ya kumtia hatiani na kumtaka kulipa faini hiyo ama kwenda jela miezi
sita.
Awali akisoma maelezo ya kesi hiyo, Mwendesha Mashitaka, Janet
Kisibo, alidai Aprili 29, mwaka jana akiwa mjini eneo la Shell ya
Gedeco, Baluhya aliyekuwa akiendesha pikipiki T 272 BQT aligongwa na
gari T 448 AGY Toyota Hilux lililokuwa likiendeshwa na dereva George
John ambaye ni mfanyakazi wa askofu huyo ambaye alikimbia baada ya
ajali hiyo na mpaka sasa anaendelea kutafutwa.
Mwendesha mashitaka alidai tuhuma zilizomfikisha mahakamani askofu huyo ni kutotunza kumbukumbu za mtumishi wake.
Baluhya ambaye ni mkazi wa Mkolani mjini hapa, ambaye sasa amekatwa
mguu kutokana na ajali hiyo, alisema amekuwa akihitaji msaada wa
kumuuguza tangu alipokuwa Hospitali ya Bugando, lakini askofu huyo
hakumsikiliza zaidi ya kumpatia sh 300,000, kiasi ambacho hakikidhi
mahitaji ya matibabu na kuhudumia familia. Alisema ana familia na mke
mmoja na watoto tisa wanaomtegemea.
“Nikimpigia simu anakuwa mkali hataki kunisikiliza, anasema niende
popote pale yeye ameshamaliza nisimsumbue,” alisema Mandikilo kwa
uchungu huku akiomba wasamaria wema wamsaidie walichonacho ili anusuru
afya yake na familia.
Chanzo;Tanzania Daima
0 comments:
Post a Comment