Geita. Mwanamke aliyefahamika kwa jina la
Sambila Mihayo anayekadiriwa kuwa na umri kati ya miaka 20 hadi 22
ameuawa kinyama na wananchi wenye hasira baada ya kukamatwa akiiba
mahindi mabichi shambani katika Kitongoji cha Ilolanguli Kijiji cha
Mbabani Wilaya ya Geita mkoani hapa.
Tukio hilo lilitokea jana saa 9:00 usiku ikiwa ni siku moja baada ya sherehe za kuanza kwa mwaka mpya 2014.
Mwenyekiti wa kitongoji hicho, Abel Kidesheni
alisema alisikia mayowe ya wananchi na alipofika eneo la tukio alikuta
tayari mwanamke huyo akiwa ameuawa na wananchi hao huku mwili wake
wakitaka kuuteketeza kwa moto.
Kidesheni alisema mwanamke huyo alikutwa akikata
mahindi kisha kuyapakia kwenye mfuko wa sandarusi ndipo alipokamatwa na
wananchi ambao walimshambulia kwa mawe, marungu na fimbo hadi kupoteza
maisha yake.
Kamanda wa Polisi mkoani Geita, Leonard Paulo
alithibitisha kutokea kwa tukio hilo na kudai kwamba uchunguzi
unaendelea ikiwa ni pamoja na kuwabaini wote waliohusika na kwamba
hakuna mtu aliyeshikiliwa kuhusiana na tukio hilo.
Akizungumza na gazeti hili, mke wa mmiliki wa
shamba hilo Milika Migeka (41) alisema wakiwa wamelala walisikia mtu
akivunja mahindi awali walifikiri ng’ombe ndipo walipotoka taratibu na
kumkuta mwanamke huyo akiendelea kukata mahindi shambani mwao.
Alisema baada ya kuona hali hiyo walipiga mayowe ambayo yaliwaamsha majirani.
‘’Baada ya majirani hao kufika walianza kumpiga
kwa fimbo,mawe na marungu hadi kumuua na baadaye walitaka kumchoma moto
lakini mwenyekiti aliwazuia,’’alisema Migeka.
Ofisa Mtendaji wa kijiji hicho Petro Manyama
alidai kusikitishwa na uamuzi uliochukuliwa na wananchi hao na kukemea
vikali vitendo vya wananchi kujichukulia sheria mikononi.
Tukio hilo ni pili kutokea mkoani Geita katika
kipindi kisichozidi wiki moja baada ya wanaume watano kuuawa kwa kukatwa
kwa mapanga kisha miili yao kutoeketezwa kwa moto baada ya kuiba rambi
rambi msibani kitongoji cha Nyantorotoro A,mjini Geita.
Chanzo;Mwananchi
Chanzo;Mwananchi
0 comments:
Post a Comment