Home » » Polisi wamshambulia mwandishi wa RFA

Polisi wamshambulia mwandishi wa RFA

MWANDISHI wa Habari wa Redio Free Afrika mkoani Geita, Salum Maige, amelazwa katika Hospitali ya Wilaya ya Geita, baada ya kujeruhiwa vibaya kutokana na kushambuliwa na askari polisi zaidi ya wanane. Akizungumza na RAI, Maige ambaye amelazwa katika chumba namba 4 wodi namba 2, alisema alishambuliwa juzi saa 1:45 usiku na kundi la askari polisi zaidi ya wanane umbali wa mita 60 kutoka zilipo ofisi za polisi mkoa.
Alisema siku ya tukio alikuwa akielekea nyumbani kwake mtaa wa Bomani, alikutana na kundi la polisi waliokuwa na gari lenye namba za usajili PT 1998 OCD GEITA, ambapo baadhi yao walishuka na kumwambia yuko chini ya ulinzi.

Alisema baada ya kuwekwa chini ya ulinzi, aliwahoji sababu ya kukamatwa kwake, ghafla alijikuta akifungwa pingu mikononi kisha kuingizwa kwenye gari huku akishambuliwa kwa kipigo kikali.

Katika tukio hilo, Maige alipoteza kamera aina ya Canon ya thamani ya Sh 350,000, kinasa sauti Sh 16,000 alizokuwa nazo.

Maige amejeruhiwa vibaya upande wa jicho na inaelezwa kwamba damu nyingi zilivujia ndani.

Alisema katika siku za hivi karibuni, amekuwa na mgogoro wa kifamilia na mkewe, Mariam Msigwa (25) ambaye katika siku za hivi karibuni wamekuwa hawaelewani.

Kamanda wa Polisi Mkoa Geita, Leonard Paul hakupatikana jana kuzungumzia tukio hilo, ingawa Kaimu wake, Pudensiana Protas alithibitisha kupokea taarifa za tukio hilo.

Chanzo;Mtanzania

0 comments:

Post a Comment

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Geita Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa