Geita.Mwandishi wa habari wa Magazeti ya
Mwananchi Communications Ltd, mkoani Geita, Salum Maige amejeruhiwa
vibaya jichoni baada ya kushambuliwa na kundi la watu wanaodaiwa kuwa ni
askari wa Kituo cha Polisi Geita.
Akizungumza jana akiwa katika Hospitali ya Geita alikokuwa amelazwa, Maige alisema alikumbwa na mkasa huo wiki iliyopita.
Alidai kuwa alivamiwa na kundi la askari polisi
zaidi ya wanane Ijumaa iliyopita ambao walimpiga na kumjeruhi vibaya
kiasi cha kulazwa kwa siku mbili katika hospitali hiyo kabla ya
kuruhusiwa.
Alisema tukio la kupigwa kwake lilitokea mita 60 kutoka zilipo Ofisi za Polisi Mkoa wa Geita pamoja na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa.
Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Geita, Pudensiana
Protas alithibitisha kupewa taarifa juu ya kukamatwa kwa mwandishi huyo
lakini hakujulishwa juu ya kupigwa na kujeruhiwa. Hata hivyo, baada ya
kuonyeshwa picha za mwandishi huyo zikionyesha alivyojeruhiwa, aliahidi
kumtafuta ili kujua undani wa tukio hilo.
Akisimulia mkasa huo, alisema siku hiyo akiwa
anapita katika Mtaa wa Bomani kuelekea nyumbani kwake, alikutana na
kundi la askari polisi waliokuwa kwenye gari la jeshi hilo ambao baada
ya kumwona, alidai kuwa baadhi yao walishuka na kumfuata huku wakitoa
amri ya kusimama na kwamba yupo chini ya ulinzi.
Alisema aliwauliza sababu za kuwekwa chini ya
ulinzi lakini badala ya kumjibu walimshika na kumfunga pingu mikononi
kisha kumtupa ndani ya gari lao.
Alisema akiwa ndani ya gari hilo walianza kumshambulia kwa kumpiga na kumsababishia maumivu makali sehemu mbalimbali za mwili.
Katika kipigo hicho, alisema alipoteza kamera aina
ya Canon yenye thamani ya Sh350,000, kifaa cha kurekodia sauti chenye
thamani ya Sh150,000, kitambulisho cha kazi na fedha taslimu Sh16,000.
Chanzo;Mwananchi
Chanzo;Mwananchi
0 comments:
Post a Comment