Home » » Marafiki, maadui waishio pamoja mgodini Geita

Marafiki, maadui waishio pamoja mgodini Geita

Uchimbaji wa madini ya dhahabu katika Mgodi wa Dhahabu Geita (GGM) ulianza rasmi mwaka 1930 na kati ya mwaka 1936 hadi 1966 mgodi huo ulifungwa na kuanza tena kuchimbwa baada ya miaka mingi.
  • Mgodi huo kwa sasa unatajwa kuwa mkubwa nchini ukilinganisha na ile mingine inayopatikana katika maeneo mbalimbali nchini.
Migodi mingine ya dhahabu ni Bulyanhulu ulioko Kahama mkoani Shinyanga, Tulawaka ulioko Biharamulo, Kagera na ile ya North Mara na Buhemba , mkoani Mara.
Kwa mujibu wa aliyekuwa Waziri wa Nishati na Madini, William Ngeleja kati ya mwaka 2000 hadi 2006, mgodi huo wa Geita uliilipa serikali kodi ya Dola za Marekani 85,784,706.
Meneja Mwezeshaji mgodi huo, Rebecca Stephen anasema mapato yaliyotokana na mauzo ya madini kwa mwaka 1999 hadi 2012 ni Dola 4,206 milioni na mgodi huo ulitumia Dola 783 milioni kwa ajili shughuli mbalimbali za uendeshaji zikiwamo za kulipia huduma na mishahara.
Kutokana na mapato hayo, GGM imelipa kodi ya Sh327 bilioni kwa Serikali pamoja na kutumia sehemu ya mapato hayo kuanzisha na kuendeleza huduma za jamii ambazo ni pamoja na uchimbaji wa visima vya maji, ujenzi wa Shule ya Wasichana ya Nyankumbu iliyoko mjini Geita.
“Mwaka 2000 hadi 2012, GGM imeilipa serikali Sh167 bilioni ikiwa ni kodi itokanayo na mishahara ya wafanyakazi. Tunafanya vizuri, tumeajiri wafanyakazi 3,600 wakiwamo wa kudumu na vibarua,” amesema meneja huyo.
Mradi wa maji safi na salama umegharimu Sh7 bilioni na utatosheleza mahitaji ya zaidi ya wakazi 120,000 wanaoishi mjini Geita wakati shule ya wasichana iliojengwa na GGM imegharimu Sh4 bilioni.
Mwalimu Mkuu wa Shule ya Nyankumbu, Scholastica Manyahi anasema mradi wa ujenzi wa shule hiyo ulibuniwa na wananchi kutokana na kutokuwapo kwa shule ya wasichana katika mkoa huo mpya wa Geita.
Manyahi anasema shule hiyo ina vyumba 21 vya madarasa, nyumba 36 za walimu, maabara na mabweni sita yamekamilika na matatu yako kwenye ujenzi.
Anabainisha kwamba changamoto mbalimbali zinazowakwamisha wanafunzi wa kike kufanya vizuri shuleni ni umbali wa kilometa 15 kufika shuleni, wanafunzi kulea watoto, bibi na babu zao na baadhi yao kubeba mimba.
“Baadhi ya wanafunzi wa kike wanakwenda kusafisha dhahabu na wengine wamekuwa wakirubuniwa na wachimbaji wadogo na kisha kupewa mimba,” anasema.

CHANZO;MWANANCHIA

0 comments:

Post a Comment

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Geita Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa