Home » » Hatua inadaiwa itamaliza migogoro inayosababishwa na uvamizi unaofanywa na wachimbaji wadogo

Hatua inadaiwa itamaliza migogoro inayosababishwa na uvamizi unaofanywa na wachimbaji wadogo

Bukombe. Serikali imeanza kupitia upya leseni za wawekezaji wakubwa wa madini ambazo hazijatumika  kwa muda mrefu, ili  maeneo hayo  yatolewe kwa wachimbaji wadogowadogo.
Akihutubia mikutano ya hadhara maeneo ya Lunzewe na Ushirombo, Wilaya ya Bukombe juzi,  Rais Jakaya Kikwete alisema hawawezi kuvumilia watu wanaochukua leseni na kukaa nazo bila kufanya kazi.
Rais Kikwete alisema Serikali inatambua uwapo wa wachimbaji wadogowagodo, hivyo imeanza kupitia leseni za wachimbaji wakubwa ili maeneo ambayo hawajayatumia yatolewe kwa wachimbaji wadogo.
Alisema wakati kazi hiyo ikikamilishwa na Serikali, wachimbaji wanapaswa kuungana kuunda ushirika, ili iwe rahisi kwa Serikali kuwasaidia kwa kuwapatia zana za kuwarahisishia uchimbaji.
 Awali, Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Stephen Masele alisema hivi sasa wizara yake imeanza zoezi la kupitia leseni hizo na kwamba, karibu wanakamilisha kazi hiyo na watasimamia kuhakikisha mafunzo yanatolewa kwa wachimbaji hao.
“Nataka kukuhakikishia (Rais Jakaya Kikwete) kuwa, wizara yetu itakapokamilisha zoezi la upitiaji leseni za wachimbaji hao wakubwa, maeneo haya tutayatoa kwa wachimbaji wadogo,” alisema Masele.
Alisema hivi sasa wachimbaji wamekuwa wakisaidiwa kuungana kwenye vikundi kujenga ushurika, ili iwe rahisi kusaidiwa kwa pamoja badala ya  mchimbaji mmojammoja.
Masele alisema kitendo cha wawekezaji kuchukua maeneo na kukaa nayo muda mrefu, kimekuwa kikisababisha wananchi kuamua kwenda kupora maeneo hayo na kuanza uchimbaji.
Alisema hali hiyo imesababisha migogoro baina yao  na wawekezaji wakubwa na wadogo.

Chanzo;Mwananchi

0 comments:

Post a Comment

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Geita Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa