MAUAJI ya kikatili dhidi ya vikongwe yanayodaiwa
kufanywa na kikundi cha Chinja Chinja yamezidi kuutikisa Mkoa wa Geita baada ya
kikongwe mwingine, Maua Ikoti (60) mkazi wa Kasang'hwa, wilayani Geita kuuawa
kwa kukatwa panga nyumbani kwake.
Kikundi cha Chinja Chinja kinadaiwa kuhusika na
mauaji ya vikongwe kwa imani za kishirikina katika mikoa ya Kanda ya Ziwa
ikiwamo Shinyanga, Mwanza, Simiyu, Geita na Mara.
Mauaji hayo yamekuja huku takwimu zikionesha kuwa
jumla ya vikongwe watatu wameuawa na kikundi hicho katika kipindi cha wiki nne.
Tukio la mauaji hayo limetokea saa 6 usiku wa
kuamkia juzi Jumapili baada ya wauaji hao kuvamia familia hiyo na kisha kuingia
ndani ya chumba alimolala kikongwe huyo.
Kwa mujibu wa Mwenyekiti wa Serikali ya Kijiji cha
Kasang’hwa, Maganiko Ndiomali, alisema wauaji hao walimkata kwa panga kikongwe
huyo sehemu za kichwani, mikono, shavuni na kwenye matiti na kumuua.
Alisema pamoja na mayowe yaliyopigwa na watoto wa
marehemu ya kuomba msaada, juhudi za wananchi kuwasaka wahusika wa tukio hilo
ili kuwatia nguvuni hazikuzaa matunda ambapo walitoweka kusikojulikana.
Mauaji ya vikongwe mkoani hapa yanadaiwa kuhusishwa
na imani za kishirikina ambapo kikundi kinachodaiwa kuhusika na mauaji hayo
hukodiwa na baadhi ya watu ili kulipiza kisasi baada ya kufiwa na ndugu zao
wakiamini kwamba wamerogwa.
Kikundi hicho kinadaiwa kuhusika na mauaji ya
kikatili dhidi ya mwanamke, Mondesta Nchambi (53) mkazi wa Kitongoji cha
Isabilo, Kijiji cha Nyakarango, wilayani Chato, mkoani Geita, kwa kumchinja
shingo kwa kutumia kitu chenye ncha kali kisha kutenganisha kichwa na
kiwiliwili chake.
Mauaji hayo yalitokea Septemba 26, mwaka huu na
kwamba katika kipindi kisichozidi wiki nne jumla ya vikongwe watatu wameuawa
kikatili katika vijiji vya Katoro, Nyakarango na Kasang’hwa mkoani Geita.
Hata hivyo kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi mkoani
Geita, Leonard Paulo, mbali na kuthibitisha kuwapo kwa matukio hayo hakuna mtu
wala watu waliokamatwa kuhusika na mauaji hayo.
Mauaji mengine yalifanywa Juni 17, 2013 ambapo
Jacob Simbakira (52) mkazi wa Kijiji cha Mwekako, Chato, Geita aliuawa na watu
wasiojulikana kwa kuchinjwa shingo na kutenganishwa kichwa na kiwiliwili chake.
Septemba 14, 2013, kikundi cha Chinja Chinja
kilimuua Ester Mashenene (61) mkazi wa Kitongoji cha Bugayambelele, Kijiji cha
Katoro, Geita.
Chanzo: Tanzania Daima
0 comments:
Post a Comment