Home » » Ukatili wa kijinsia dhidi ya wanawake vikongwe wakithiri geita.

Ukatili wa kijinsia dhidi ya wanawake vikongwe wakithiri geita.

  MWANAMKE Tabu Shitunguru (55) mkazi wa Nyugwa Mkoani Geita ambaye ni mmoja wa wanawake waliofanyiwa ukatili wa kijinsia kwa kukatwa mapanga baada ya kutuhumiwa kuwa ni mchawi kutokana na macho yeke kuwa mekundu.


MMOJA wa Wanawake vikongwe ambao wamekuwa 
wakivamiwa na kuuawa kwa kukatwa mapanga kwa tuhuma za kuwa wachawi kutokana na macho yao kuwa mekundu,haya ndio maisha ya baadhi yao huko vijijini.(Picha zote na David Azaria)


Wauawa kwa kukatwa mapanga kwa tuhuma za uchawi
Kisa macho yao mekundu
Na David Azaria, Geita yetu
“Kilichoniponza ni haya macho yangu mekundu….nimekua nikisikia watu wakisema kwamba mimi ni mchawi, lakini naamini Mungu ni shahidi yangu mkuu kwamba siujui uchawi ukoje na katika maisha yangu sijawahi kujihusisha na vitendo hivyo, wamenikata mapanga kwa lengo la kuniua huu ni unyama usiovumilika’’ hayo ni maneno ya mmoja wa waathirika wa unyanyasaji na ukatili unaofanywa kwa vikongwe wenye macho mekundu Mkoani Geita. 
Vitendo vya ukatili dhidi ya wanawake kwa Imani za kishirikina Mkoani Geita bado vinaendelea kuchukua kasi baada ya mwanamke mmoja kuvamiwa nyumbani kwake na kujeruhiwa vibaya sehemu mbalimbali za mwili wake kwa kukatwakatwa mapanga. 
Tukio hilo ni mwendelezo wa mauaji ya wanawake ambapo wengine wanne wameuawa kisha miili yao pamoja na nyumba zao kuteketezwa kwa moto kwa imani za kishirikina. 
Katika tukio la kwanza lililotokea hivi karibuni katika kijiji cha Isonda kata ya Nyugwa wilayani Nyang’hwale, mwanamke mmoja Tabu Shitunguru (55) amelazwa katika hospitali ya wilaya ya Geita akiuguza majeraha yaliyotapakaa mwili mzima kutokana na kukatwakatwa kwa mapanga kwa tuhuma za kujihusisha na uchawi. 
Kama vile hiyo haitoshi siku chache baadaye huko katika kijiji cha Rwezera Tarafa ya Bugando wanawake wanne walishambuliwa mchana kweupe kwa vipigo, kukatwa mapanga, kuchomwa mishale na kisha miili yao kuteketezwa kwa moto hadi kuwa majivu.
Ni mauaji ya kusikitisha ambayo ni vigumu kuamini kwamba umetendwa na binadamu hawa ndani ya nchi ambayo inasifika kwa amani na utulivu, hapa ndipo tulipofikia watanzania, hatuheshimiani tena, na wala hakuna roho ya upendo na huruma!. 
Tukio hio la kuuawa kwa wanawake hao lilitokana na kifo cha mtoto mdogo mwenye umri wa miaka mitano Diana Salu ambaye alikamatwa kisha kutafunwa na Fisi hali iliyowapelekea wanakijiji wa eneo hilo kulihusisha tukio hilo na imani za kishirikina. 
Siku hiyo ya tukio mtoto huyo alikamatwa na kutafunwa na fisi majira ya saa moja usiku ambapo alikutwa na mkasa huo wakati akirudi nyumbani kwao akitokea dukani kununua biskuti ambapo baada ya kukamatwa alipiga kelele kuomba msaada lakini majirani walipofika mahali pa tukio walikuta tayari amekwishatafunwa baadhi ya viungo vyake ukiwemo mguu pamoja na sehemu za siri. 
Wananchi hao walianza kumkimbiza fisi huyo kwa lengo la kumuua ambapo alipotea katika mazingira ya kutatanisha baada ya kufika kwenye nyumba ya mmoja wa Bibi kizee aitwaye  Lolensia Bagili (70) ambapo wananchi hao walianza kumhoji na akasema kwamba fisi huyo alikuwa kwenye nyumba ya mwenzao. 
Kutokana na maelezo hayo wananchi hao wenye hasira walimuamuru kikongwe huyo kuwapeleka kwa mwenzake alipodai fisi huyo yupo, hata hivyo hawakuweza kumkuta na ndipo walipoanza kumshambulia kwa mapanga na marungu na kufa papo hapo, lakini kabla ya kifo chake kikongwe huyo aliamuriwa kuwataja wenzake ambao amekuwa akifanya nao shughuli za kichawi ambapo aliwataja vikongwe wengine watatu. 
Baada ya kumaliza mauaji dhidi ya kikongwe huyo waliendelea na msako mkali dhidi ya wengine ambapo nao waliwaua na kuwachoma moto na kama vile hiyo haitoshi wakateketeza nyumba zao kwa moto na kusababisha familia zao kukosa mahali pa kuishi.
Tabu Shitunguru (55) ambaye ni mwathirika wa vitendo hivyo vya kinyama akizungumza akiwa hospitali anasema amekuwa kilema kutokana na kunyofolewa vidole vyake sita kati ya kumi vya mikono yote miwili, kutokana na kukatwa mapanga, huku sehemu mbalimbali za mwili wake ikiwemo Shingo yake na Mgongoni ikiwa imecharangwa mapanga na kuharibika vibaya.
Akisimulia mkasa huo Mwanamke huyo anasema siku hiyo akiwa nyumbani kwake na mwanae wa kiume aliyemtaja kwa jina la Robert Mathias baada ya kumaliza kula nje ya nyumba yao majira ya saa 2 usiku, ghafla alishangaa akivamiwa na mtu asiyemfahamu na kuanza kumshambulia kwa kumkata mapanga shingoni. 
“Wakati tumekaa pale nje kijana wangu akiwa anakula mimi tayari nilikuwa nimemaliza kula chakula,nikashtukia mtu akinivamia na kuanza kunikata mapanga shingoni,a,alinikata panga la kwanza shingoni kisha mgongoni nikaanguka chini sikujua tena kilichoendelea hadi juzi nilipojikuta niko hapa hospitalini nikiwa nimefungiwa haya mabandeji mgongoni, kichwani,shingoni na mikononi…’’ anasema Mwanamke huyo. 
Tabu anasema wauaji hao wamempatia kilema cha maisha na sasa hawezi kufanya kazi ya aina yoyote kutokana na kutokuwa na vidole vya mikono, ambavyo siku za nyuma vilikuwa vikimsaidia kushika jemba na kwenda shambani na kulima,na hasa ikizingatiwa kwamba yeye ni mkulima anaendesha maisha yake kutokana na kilimo. 
“Kwa sasa siwezi hata kushika jembe,sijui nitakuwa mgeni wa nani?....kibaya zaidi hata huku mgongoni pamoja na shingoni wamenikata vibaya kiasi kwamba Daktari anasema siwezi kufanya kazi ngumu,ndiyo maana nasema kwa sasa mimi ni kilema,na hii inamaanisha kwamba nitazidi kuwa maskini zaidi kwa sababu sitakuwa na uwezo hata wa kujitafutia kipato. 
Hata hivyo mwanamke huyo anakanusha vikali tuhuma za uchawi dhidi yake zilizopelekea yeye kujeruhiwa kwa kukatwa mapanga na kueleza kwamba hajawahi kujihusisha na vitendo hivyo katika maisha yake ingawa kwa miaka mingi amekuwa akisikia akituhumiwa kwamba yeye ni mchawi kutokana na macho yake kuwa mekundu. 
Daktari anayemtibu mwanamke huyo Dk.Daniel Izengo akizungumzia hali hya mwanamke huyo anasema amejeruhiwa vibaya sehemu mbalimbali za mwili wake na hasa mgongoni, na shingoni hali ambayo imesababisha baadhi ya mishipa kukatika na hivyo kupoteza nguvu za kufanya kazi. 
“Kwa kweli ameumia vibaya sana, hana vidole sita kati ya 10 vya mikono yake yote miwili, na hata hivi vilivyobaki havina kazi yoyote kwa sababu vimepoteza nguvu kutokana na mishipa kukatwakatwa,na hata shingoni mwake na mgongoni ameumia vibaya kutokana na kukatwa mapanga….hali ambayo imesababisha baadhi ya mishipa kukatika……’’ anafafanua Dk.Izengo. 
Mkuu wa mkoa wa Geita Said Magalula Said anasema miongoni mwa mambo ambayo serikali ya mkoa imepanga mikakati ya kupambana nayo kwa kasi kubwa ni pamoja na ukatili huo wa kijinsia wanaofanyiwa wanawake kwa imani za ksihirikina ikiwa ni pamoja na kutoa elimu kwa jamii ili kutambua na kuachana na imani hizo potofu.
Alisema mkakati wa kutoa elimu zaidi katika jamii kuhusiana na Imani potofu zinazosababisha ukatili wa kijinsia kwa wanawake ikiwa ni pamoja na mauaji ya mapanga zinatiliwa mkazo. 
Taarifa za kiuchunguzi zinaonesha kuwa  tangu Mwezi Januari Mwaka 2011 hadi kufikia Mwishoni mwa Mwezi wa Mei  mwaka huu jumla ya wanawake 51 wamefanyiwa ukatili wa kijinsia kwa kukatwa kwa mapanga kwa kisingizio cha kuwa wachawi ambapo 24 kati yao wamepoteza maisha huku 27 wakipata kilema cha maisha  mkoani  Geita. 
Uchunguzi unaonesha kuwa wilaya ya Geita ambayo kabla ya kugawanywa na kupatikana wilaya nyingine ya Nyang’hwale katika kipindi hicho inaongoza kwa kuwa na wanawake 21 waliofanyiwa ukatili huo ambapo kumi na moja kati yao wamepoteza maisha na wengine 10 wamepata kilema cha maisha.
Geita inafuatiwa na wilaya za Bukombe na Mbogwe zilizokuwa zimeungana Kabla ya kugawanywa na kupatikana wilaya mbili zinazounda mkoa wa Geita yenye wanawake 16 ambapo 7 wamepoteza maisha, a Chato wanawake kumi na moja ambapo 5 wamepoteza maisha. 


0 comments:

Post a Comment

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Geita Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa