na Sitta Tumma, Geita
SHIRIKA la Plan International Tanzania limezindua mradi maalumu wa kupambana na kutokomeza ajira hatarishi kwa watoto wilayani Geita, mkoa mpya wa Geita.
Uzinduzi wa mradi huo uliofanyika hivi karibuni wilayani hapa umeonekana kuleta matumaini mapya ya makuzi mema na maendeleo kwa watoto walio katika hatari ya kutumikishwa migodini, viwandani, mashambani na maeneo mengine hatarishi.
Mkuu wa kitengo cha uchumi katika Jumuiya ya Ulaya (EU) nchini, Stefan Schleuning, alisema mradi huo unatarajiwa kuwashirikisha wadau mbalimbali kwa ajili ya kutokomeza tatizo la ajira hatarishi kwa watoto wilayani hapa.
Schleuning ambaye alimwakilisha Balozi wa EU, Filiberto Ceriani Sebregondi, alielezea kusikitishwa na takwimu za sasa zinazoonyesha kwamba kati ya watoto 100 duniani 16 wameajiriwa na wengine 12 wako katika hatari ya kufanyishwa kazi ngumu na hatarishi.
“Takwimu zilizopo zinaonyesha watoto wengi hawapelekwi shule kabisa na katika kila watoto 100 zaidi ya nusu ya watoto hao hawahitimu masomo yao shuleni,” alisema Schleuning.
Alisema tatizo la ajira kwa watoto ni kubwa hapa Tanzania ambapo asilimia 70.4 ya watoto wenye umri kati ya miaka mitano na 17 wamejiingiza katika kazi hatarishi za kiuchumi maeneo ya migodini, mashambani, viwandani na ukahaba jambo ambalo ni hatari kwa maisha yao.
Schleuning alisema EU inaamini kuwa elimu ndiyo haki muhimu na ufunguo unaomwepusha mtoto kutumikishwa katika kazi hatarishi.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Plan International Tanzania, David Muthungu, alisema shirika hilo linashughulikia maendeleo ya jamii yanayomlenga mtoto na kwamba ili kutimiza njozi hiyo limejipanga kutumia maeneo makuu matano kuzuia ajira hatarishi kwa watoto.
Mkurugenzi huyo wa Plan hapa nchini Tanzania, alizitaja nyanja hizo kuwa ni pamoja na mazingira salama kwa watoto na vijana, elimu, kujikimu, afya ya jamii, maji na usafi wa mazingira, sauti ya watoto na vijana.
Naye Mkuu wa Mkoa mpya wa Geita, Magalula Saidi Magalula, alisema kuwa serikali inatambua uwepo wa tatizo la ajira hatarishi kwa watoto nchini, hivyo inaendelea kufanya jitihada mbalimbali kukabiliana nalo kwa kushirikiana na sekta binafsi.
“Serikali itaendelea kushirikiana na shirika hili la Plan International bega kwa bega katika juhudi za kutokomeza ajira hatarishi kwa watoto na kuleta maendeleo kwa jamii na taifa kwa ujumla
Chanzo: Tanzania Daima
0 comments:
Post a Comment