Home » » MWENYEKITI, WAJUMBE WA SERIKALI YA KIJIJI LAMADI WASIMAMISHWA KAZI KUPISHA UCHUNGUZI

MWENYEKITI, WAJUMBE WA SERIKALI YA KIJIJI LAMADI WASIMAMISHWA KAZI KUPISHA UCHUNGUZI

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
Mkuu wa Mkoa wa Simiyu akizungumza na wananchi wa Kata ya Lamadi katika mkutano wa Hadhara uliofanyika Lamadi wiayani Busega.
Mwenyekiti wa Kijiji cha Lamadi Wilayani Busega, Mhe. Nzala Hezron akizungumza na wananchi katika Mkutano wa Hadhara ulioitishwa na Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe.Anthony Mtaka kwa lengo la kusikiliza kero mbalimbali za wananchi na kuzitolea ufumbuzi.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Simiyu, Boniventure Mushongi akitoa ufafanuzi wa masuala mbalimbali katika Mkutano wa hadhara uliofanyika katika Kata ya Lamadi wilayani Busega.


Na StellaKalinga, Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Simiyu

Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe.Anthony Mtaka amemsimamisha kazi kwa muda wa mwezi mmoja Mwenyekiti wa Kijiji cha Lamadi Wilayani Busega Mhe.Nzala Hezron pamoja na Wajumbe wa Serikali ya Kijiji hicho, ili kupisha uchunguzi kufuatia tuhuma mbalimbali zinazowakabili.



Uamuzi huo umekuja kufuatia malalamiko yaliyotolewa na wananchi wa Lamadi dhidi ya Mwenyeiti huyo kwa Mkuu Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe.Anthony Mtaka katika Mkutano wa hadhara uliofanyika jana Lamadi, kuhusu tuhuma mbalimbali ikiwemo matumizi mabaya ya fedha za michango ya wananchi katika Ujenzi wa Shule ya Sekondari Lukungu pamoja na kutosoma mapato na matumizi ya fedha za michango mbalimbali ya wananchi.



“Ili tuweze kutenda haki ya uchunguzi na ukaguzi tumeona ni busara Mwenyekiti asiwe Ofisini na wajumbe wanaounda Serikali ya Kijiji wasiwe ofisini ili uchunguzi na ukaguzi wa akaunti uweze kufanyika kwa haki” alisema Mtaka.

Mtaka amesema Mkaguzi wa Ndani kutoka katika Ofisi yake atakayeshirikiana na Mkaguzi wa ndani wa Wilaya ya Busega kufanya ukaguzi katika Akaunti ya Shule kujua namna fedha zilizochangwa na wananchi na zilizotolewa na Halmashauri zilivyofanya kazi ya Ujenzi wa Vyumba vya madarasa na matundu ya vyoo katika Shule ya Sekondari Lukungu.

Ameongeza kuwa kutokana na malalamilo ya baadhi ya wadau pamoja na wananchi uchunguzi na ukaguzi huo pia utahusisha pia Akaunti ya Kijiji cha Lamadi kwa kuwa Kijiji hicho kina hali nzuri kimapato na kimekuwa kikichangiwa na wadau mbalimbali wa maendeleo, hivyo ni vema ikabainishwa wadau wanaokichangia, wanachangia kitu gani na namna michango hiyo inavyotumika.

Aidha, Mtaka amesema ukaguzi huo pia utafanywa kwenye kamati iliyohusika katika upimaji viwanja katika Mji Mdogo wa Lamadi kwa sababu nayo imekuwa ikilalamikiwa na baadhi ya wananchi kuwa haikuwatendea haki.

Mkuu wa Mkoa huyo amesema uchunguzi na ukaguzi katika maeneo hayo matatu utaanza tarehe 10/01/2018 na taarifa rasmi ya zoezi hilo itatolewa tarehe 10/02/2018 kwa wananchi kupitia Mkutano wa hadhara, itakapobainika kuwa tuhuma zilizotolewa dhidi ya watu hao ni za kweli Serikali itachukua hatua.

Wakati huo huo Mtaka amemtaka Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Busega kumuondoa Afisa Mtendaji wa Kata ya Lamadi Bw.Furaha Magese Ng’onela na kuhakikisha kuwa ifikapo tarehe 10/01/2018 Kijiji cha Lamadi kinapata Mtendaji wa Kijiji kwa kuwa aliyepo sasa anakaimu na Kata ya Lamadi ipangiwe Afisa Mtendaji mwingine.

Vile vile Mtaka ameahidi kuchangia mifuko 100 ya saruji katika Ujenzi wa Shule ya Sekondari Lukungu ambayo sasa imepewe jina lake(Mtaka Sekondari) na wananchi hao, Mkuu wa Wilaya ya Busega,Mhe.Tano Mwera ameahidi kuchangia mifuko 40 na Mbunge wa Jimbo la Busega, Mhe.Dkt.Raphael Chegeni ameahidi kutoa vifaa vya ujenzi vyenye thamani ya shilingi milioni 10 kufanikisha ujenzi huo.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kijiji cha Lamadi, Mhe.Nzala Hezron amesema kuhusu suala la ujenzi wa Shule yeye pamoja na Serikali yake ya Kijiji haikushirikishwa kikamilifu na Kamati ya Maendeleo ya Kata(WADC).

Naye Mhe.Chegeni amemhakikishia Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe.Anthony Mtaka kuwa michango ya viongozi, wadau wa mendeleo na wananchi wa Lamadi inayotolewa sasa itatumika kama ilivyokusudiwa na ikiwa kuna atakayebainika kutumia tofauti na utararibu atachukuliwa hatua.

Mkuu wa Wilaya ya Busega, Mhe.Tano mwera ametoa wito kwa wananchi wa Lamadi kuunga mkono juhudi za Serikali kwa kuchangia shilingi 10,000 kwa kaya ili kufikia Februari 15, 2018 vyumba vinne vya madarasa viwe vimekamilika katika Shule ya Sekondari Lukungu(imebadilishiwa jina na wananchi na kuitwa Mtaka Sekondari), ambayo hadi sasa ina madarasa manne na matundu ya vyoo 16 yanayoendelea kukamilishwa ili wanafunzi waanze masomo.

Nao wananchi wa Vijiji vinavyounda Kata ya Lamadi wamesema wamejipanga kuhakikisha vyumba vya madarasa vinajengwa na kukamilika  katika shule hiyo kabla ya Februari 15, 2018 ambapo kila Kitongoji kimejipanga kuanza na ujenzi wa chumba kimoja cha darasa na vitongoji vyenye watu wachache vitaungana viwili kujenga chumba kimoja cha darasa, ambapo kamati za ujenzi zitachaguliwa na wananchi wenyewe.

0 comments:

Post a Comment

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Geita Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa