Kiongozi wa familia hiyo, Albert Michael, alipozungumza na waandishi wa habari mjini Geita.
---
Na Rashid Zahor, Geita.
FAMILIA
ya mgombea urais wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. John Magufuli
imesema Watanzania watakuwa na bahati ya kumpata kiongozi mchapakazi,
mwenye msimamo na anayependa maendeleo.
Imesema
iwapo Dk. Magufuli atachaguliwa kuwa rais, katika uchaguzi mkuu
unaotarajiwa kufanyika Jumapili wiki hii, atawaletea maendeleo makubwa
kwa kuwa ni mtu mwenye msimamo, asiyeyumba na anayependa maendeleo.
Kauli hiyo ilitolewa jana na kiongozi wa familia hiyo, Albert Michael, alipozungumza na waandishi wa habari mjini Geita.
Mzee
Albert hakuwepo Katoma juzi wakati msafara wa Dk. Magufuli uliposimama
kwa muda nyumbani kwa babu yake, ambako alipata nafasi ya kuzuru kaburi
lake na la bibi yake mzaa wa baba na kuwaombea dua.
"Watanzania
wasiwe na wasiwasi, Magufuli ni mtu anayependa watu na maendeleo na ni
mchapakazi,"alisema Mzee Albert, alipokuwa akijibu swali kuhusu sifa za
mgombea huyo tangu alipokuwa mtoto.
Aidha,
Mzee Albert alisema Dk. Magufuli si mpole, sio mkali sana, lakini ni
mtu mwenye msimamo na asiyeyumba katika jambo analotaka kulifanya.
Mzee
Albert, ambaye ndiye aliyeachiwa mji wa Katoma kwa sasa, liliko
chimbuko la ukoo wa Dk Magufuli, akiwa miongoni mwa wadogo zake marehemu
baba mzazi wa mgombea huyo, alisema familia yao ipo pamoja naye na
inamuombea Mungu aweze kutimiza dhamira yake ya kuwa rais wa awamu ya
tano ya serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
"Ninachowahakikishia
Watanzania ni kwamba Oktoba 25, watampata kiongozi bora, asiye na
ubaguzi wa aina yoyote,"'alisema mzee huyo.
Akizungumzia
majina ya mgombea huyo, alisema jina la Pombe alipewa na bibi yake siku
alipozaliwa, kwa kuwa siku hiyo alikuwa akipika pombe. Alisema jina la
Magufuli lilitokana na kupenda kwake michezo.
"Siku
John alipozaliwa, bibi yake alipopelekewa taarifa, alisema 'huyo mume
ni mume wangu aitwe pombe'," alisema mzee huyo, ambaye alifika Geita
juzi usiku akitokea Chato.
Juzi,
Dk. Magufuli alitembelea kwenye makaburi ya babu na bibi yake mzaa wa
baba, eneo la Katoma, wilayani Geita Vijijini na kufanya ibada ndogo ya
kuwaombea dua.
Dk.
Magufuli alifika nyumbani kwa babu yake saa 6.30 mchana na kupokewa na
baba yake mdogo, Sylvestr Magufuli, kabla ya kupelekwa kwenye makaburi
hayo, ambako aliongoza ibada ndogo ya kuwaombea dua.
Akizungumza
kwenye eneo hilo, baba huyo alisema makaburi hayo ni ya babu na bibi wa
mgombea huyo pamoja na ndugu zake wengine, waliofariki dunia miaka
mingi iliyopita.
Alisema asili ya ukoo wa Dk. Magufuli ni Katoma, ambako ndiko baba yake alikozaliwa kabla ya kuhamishia makazi yake Chato.
"Tumezoea
kumuona ndugu yetu kwenye tv na kumsikiliza kwenye redio, leo
tumefurahi kumuona yeye mwenyewe,"alisema na kuongeza kuwa wanamuombea
dua kwa Mungu ili aweze kuchaguliwa kuwa rais.
Kwa
upande wake, Dk. Magufuli alisema alifarijika kufika tena katika eneo
hilo kwa sababu ndiko alikozaliwa na kukulia na pia ndiko ukoo wake
ulikoanzia.
Dk.
Magufuli alitumia fursa hiyo kuwatambulisha ndugu zake kwa wanahabari
kabla ya kuingia kwenye nyumba ya familia, iliyoko umbali wa mita 30
kutoka barabara itokayo Kamanga kwenda Sengerema.
Mgombea huyo alisema jina la Pombe alipewa na bibi yake, aliyemtaja kwa jina la Anastazia, siku alipoivisha pombe yake.
Alisema
babu yake, marehemu Michael, alifariki dunia akiwa na umri wa miaka 103
baada ya kumuuguza kwa muda mrefu akiwa Dar es Salaam na baadaye
kumrejesha Katoma.
"Kwangu
siku hii ni ya pekee. Nilipojua kwamba nitasafiri kwa kutumia njia hii,
niliona ni lazima nipite hapa kwa sababu ndiko maisha yangu
yalikoanzia,"alisema Dk. Magufuli na kusifu maendeleo yaliyopatikana
katika kijiji hicho, ikiwemo nishati ya umeme.
Aliwaomba
wakazi wa kijiji hicho wamuombee dua kwa Mungu ili aweze kushinda kiti
cha urais, katika uchaguzi mkuu wa rais, wabunge na madiwani,
unaotarajiwa kufanyika nchi nzima Jumapili.
0 comments:
Post a Comment