Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
Waziri wa Ujenzi, Dk. John Magufuli
Waziri
wa Ujenzi, Dk. John Magufuli, amewaaga rasmi wakazi wa Chato mkoani
Geita, akisema hatagombea tena ubunge katika jimbo hilo baada ya Chama
Cha Mapinduzi (CCM) kumteua kuwa mgombea wake wa urais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania katika Uchaguzi Mkuu utakaofanyika nchini Oktoba
25, mwaka huu.
Mbali na kuwaaga wakazi hao, Magufuli ameahidi kuendelea
kushirikiana na wananchi ili kuhakikisha Tanzania inapata maendeleo
haraka.
Aliwaambia wakazi hao kuwa atakapochaguliwa kuwa Rais katika
uchaguzi huo utakavishirikisha vyama vya siasa vya upinzani nchini,
atakuwa msikivu na mwenye kukubali kuelekezwa na marais waliotangulia.
"Ndugu zangu nawashukuru kwa kuniamini na kunipa nafasi ya
kuwatumikia kwa miaka 20 nikiwa mbunge wenu...tumefanya kazi nzuri
naamini kila mmoja wenu anajua hilo," alisema na kuongeza kuwa:
"Lakini pia nilipofika hapa kuomba udhamini wa nafasi ya kuteuliwa
na CCM kugombea urais mliniahidi na kuniombea sana ili nifanikiwe na
hatimaye imekuwa." alisema. Alisema anachoweza kuwaambia ni kuwashuri na
kusisitiza kuwa hatawaangusha atakapoingia Ikulu.
"Ninachoweza kusema kwenu asanteni sana, naahidi kutowaangusha
nitawatumika Watanzania wote pasipo kujali itikadi za vyama vyenu, dini,
kabila kwa kuwa maendeleo hayana chama. Kazi niliyokabidhiwa na chama
changu ni kubwa na nitakuwa msikivu kwa kuwa chama chetu kinao wazee
wengi wenye bussara ukianzia Mzee mkapa, Mwinyi, Kalume, Jakaya na
wengine wengi."
Wakati Dk Magufuli akiwaaga wakazi hao waliokuwa wamefurika kwenye
viwanja vya kituo cha zamani cha mabasi wilayani Chato, kumsikiliza
walisikika wakisema yeye ndiye mkombozi wa Tanzania.
AZUNGUMZIA UKANDA
Magufuli ambaye alipokelewa kwa mbwembwe katika jimbo hilo, awali
alisema kuwa wakazi wa Kanda ya Ziwa wasitegemee katika uongozi wake
atafanya upendeleo.
Alisema hatakuwa na upendeleo wa kikanda katika uongozi wake huku
akisisitiza kipaumbele kikubwa ni kuhakikisha ajira inapewa kipaumbele
kwa vijana.
“Nitahakikisha natenda haki sawa kwa wote bila kuangalia huyu ni
mwana CCM, Ukawa, ujimbo ama ukanda, lengo ni kuleta maendeleo kwa wote
na wala wananchi wasitegemee wapo nitakaowabeba,” alisema Dk. Magufuli.
Alisema maendeleo hayana chama fulani, bali yapo kwa wananchi wote
ambao ni wazawa wa nchi hii hivyo wale wanaoamini Rais kutoka kanda ya
ziwa ataonyesha upendeleo, amefilisika kimawazo.
"Magufuli ni wenu wenyewe mlimchagua kuwatumika Watanzania na kwa
kuwa hamkukosea kumchagua kuwa Mbunge wenu, pia serikali iliona kuwa
hili ni jembe na kumteua kuwa Waziri kwa kipindi chote cha utumishi
wake," alisema Nape na kusisitiza kuwa:
"Kana kwamba haitoshi CCM kimeendelea kuridhishwa na uwajibikaji wake na sasa kinampa ridhaa ya kugombea urais."
Baadhi ya wakazi wa jimbo hilo, waliliambia NIPASHE kuwa
wamefurahishwa na CCM kumteua Magufuli kuwa mgombea urais kinyume na
matarajio ya wengi.
SOURCE:
NIPASHE
0 comments:
Post a Comment