Home » » HOT NEWS: NAULI ZA MABASI YA MIKOANI ZASHUKA , VIWANGO VYAWEKWA WAZI

HOT NEWS: NAULI ZA MABASI YA MIKOANI ZASHUKA , VIWANGO VYAWEKWA WAZI


Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Udhibiti Usafiri wa Nchi Kavu na Majini Nchini (Sumatra), Gilliard Ngewe.
Serikali imetangaza viwango vipya vya nauli za mabasi zitakazoanza kutumika kuanzia Aprili 30, mwaka huu, huku nauli za magari hayo yanayokwenda mikoani zikishushwa na zile za daladala zinazotoa huduma maeneo ya mijini zikiendelea kubaki kama zilivyo.
 
Nauli hizo mpya zilitangazwa jana na Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Udhibiti Usafiri wa Nchi Kavu na Majini Nchini (Sumatra), Gilliard Ngewe.
 
Alisema punguzo la nauli hizo ni asilimia 7.8 kwa daraja la kawaida la chini na asilimia 5.81 daraja la kati.
 
Ngewe alisema viwango hivyo vimebadilika kutokana na kushuka kwa kwa bei ya mafuta mwishoni mwa mwaka jana.
 
Alisema kutokana na kushuka kwa bei ya mafuta, Sumatra imekuwa ikipokea wito wa kupitia upya viwango vya juu vya nauli vilivyowekwa na mamlaka hiyo Aprili, 2013.
 
Pia alisema wamefanya mabadiliko hayo baada ya kukusanya maoni kutoka kwa wadau na wamiliki wa usafirishaji katika mikutano mbalimbali iliyofanyika jijini Mwanza, Dar es Salaam na Arusha.
 
Alisema Machi 9, mwaka huu, Baraza la Ushauri la Watumiaji wa Huduma Zinazodhibitiwa na Sumatra (SCCC) liliwasilisha kwa Sumatra maombi ya kushusha nauli za mabasi ya masafa marefu na mijini.
 
Ngewe alisema katika maombi hayo baraza liliainisha sababu za kuomba punguzo hilo kuwa ni kushuka kwa bei za mafuta na kodi ya forodha kwa mabasi mapya kutoka asilimia 25 hadi 10.
 
 Alisema baraza hilo liliomba nauli ya masafa marefu kwa kilomita moja ya basi la abiria la kawaida kutoka Sh. 36.89 hadi 28.05 sawa na asilimia 23.96, nauli ya basi la hadhi ya juu ishuke kutoka Sh. 58.47 hadi 47.19 (asilimia 19.29).
 
Ngewe alisema katika usafiri wa mijini, maombi yalikuwa ni kupunguza nauli kwa asilimia 23 kwa njia yenye umbali wa kilomita 10 kutoka Sh. 400 ya sasa hadi Sh. 300.
 
Alisema baada ya kutafakari taarifa iliyowasilishwa na baraza hilo, bodi iliridhia viwango vipya vya juu vya nauli kwa mabasi ya masafa marefu kwamba, daraja la kawaida la chini kupitia njia ya lami, ipungue kutoka Sh. 36.89 hadi Sh. 34.00 (asilimia 7.8). 
 
Ngewe alisema pia daraja la kawaida la chini njia ya vumbi, ipungue kutoka Sh. 46.11 hadi Sh. 42.50 (asilimia 7.8), daraja la kawaida la juu ipungue kutoka Sh. 46.22 hadi Sh. 44.96 (asilimia 7.8),  huku daraja la kati nauli ipungue kutoka  Sh.53.22 hadi 50.13 (asilimia 5.81).
 
Alisema kutokana na maombi hayo, bodi iliamua nauli za mabasi ya hadhi ya juu (luxury) hazitawekewa kiwango maalumu isipokuwa Sumatra itawaacha wasafirishaji kupanga bei ya nauli inayoendana na huduma ya mabasi hayo.
 
Ngewe alisema pamoja na kuwaachia uhuru huo, Sumatra itasimamia na kujiridhisha kuona endapo nauli wanazotoa zinaendana na huduma wanayotoa na kwamba, hiyo imetokana na uchache wa magari ya kiwango hicho yanayotoa huduma kwa sasa.
 
Pia alisema itasaidia  kuchochea ubunifu katika utoaji huduma kwa ushindani kati ya huduma za barabarani na njia nyingine za usafiri.
 
Ngewe alisema baada ya ukokotoaji kufanyika na kwa kuzingatia masuala muhimu yaliyoainishwa, bodi iliridhia viwango vya sasa vya nauli za daladala viendelee kutumika kutokana na punguzo lililokokotolewa kuwa dogo ikilinganishwa na viwango vinavyotumika.
 
Alisema viwango vilivyokokotolewa iwapo vingepitishwa vingesababisha usumbufu wa malipo kwa abiria pamoja na watoa huduma.
 
Ngewe alisema katika kukokotoa kwa urefu wa kilomita 0-10,  ambayo nauli yake kwa sasa ni Sh. 400, ilitakiwa kushuka hadi Sh. 376.77 (asilimia 5.8), kilomita 11-15 ilitakiwa kushuka kutoka Sh. 450 hadi Sh. 448.62 (asilimia 0.3).
 
Alisema kilomita 16-20 ilitakiwa kushuka kutoka Sh. 500 hadi Sh. 485.34 (asilimia 2.9),  kilomita 21-25 ishuke kutoka Sh. 600 hadi Sh. 583.34 (asilimia 2.8), kilomita 26-30 ilitakiwa kushuka kutoka Sh. 750 hadi Sh. 742.74 (asilimia 1).
 
Hata hivyo, Ngewe alisema bodi ilibaini kuwa bei ya mafuta ilikuwa imeshuka ikilinganishwa na bei iliyokuwapo wakati viwango vya sasa vilipoanza kutumika Aprili 2013.
 
Alisema bei hizo mpya za nauli kwa mabasi yaendayo mikoani zitabandikwa na pia  mtu yeyote atazipata kupitia simu yake ya mkononi na kwenye tovuti ya Sumatra, ambazo pamoja na mambo mengine, itakuwa inabainisha madaraja ya basi husika.
 
Ngewe alisema Dar es Salaam hadi Arusha nauli ya sasa ni Sh. 22,700 ipungue kufikia 21,000, Dar-Babati Sh. 29,00 ipungue hadi 27,00, Dar-Mbeya Sh. 30,700 ipungue kufika Sh. 28,500.
 
Dar-Mwanza Sh.42,600 ipungue hadi Sh. 36,500, Dar -Sumbawanga Sh. 45,100 iwe Sh. 42,00 , Dar -Songea Sh. 35,000 iwe Sh. 32,500, Dar-Dodoma Sh. 16,700 iwe Sh. 15,500.
CHANZO: NIPASHE
Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.

0 comments:

Post a Comment

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Geita Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa