Waziri Mkuu Mstaafu, Frederick Sumaye, amesema deni la taifa halihimiliki na kuna hatari litaliingiza taifa kwenye wakati mgumu.Akizungumza na NIPASHE katika mahojiano maalum wiki iliyopita, Sumaye alisema kukosekana kwa nidhamu ya fedha ndiko kumesababisha deni la taifa kuongezeka siku hadi siku.
“(Hili) linanipa shida… kama fedha zinakusanywa halafu hazionekani ni lazima kujua zinakwenda wapi, ni lazima tusimamie mapato ya serikali, kwa sasa tunakusanya Shilingi trilioni moja kwa mwezi, mimi nashangaa hizo fedha zinakwenda wapi kama haziwezi kutatua matatizo ya nchi?” alihoji.
“Kuna wakati nilisoma taarifa zao, kwa mwezi walivuka trilioni moja, nashangaa hizo fedha zinakwenda wapi… wakisimamia matumizi sawa sawa hili tatizo litapungua sana,” alisema.
Alisema iwapo matumizi yatasimamiwa vizuri ni wazi kuwa fedha inayokusanywa itaweza kutatua matatizo mbalimbali.
Alisema hali ni mbaya kwenye hospitali kutokana na Bohari Kuu ya Dawa (MSD) kugoma kupeleka dawa kutokana na deni kubwa la zaidi ya bilioni 102 na tayari baadhi ya hospitali zimefungiwa kupelekewa dawa, ikiwamo Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH).
Hivi karibuni MSD ilisema hadi kufikia Septemba 2014 deni linalodaiwa kwenye vituo vya serikali limekuwa na kufikia kiasi cha Sh. bilioni 102 na mwishoni mwa mwaka 2013 lilikuwa Sh. bilioni 76.4.
“Kwa nini serikali hailipi? Hatujui… ukienda kwenye mifuko ya hifadhi ya jamii wanaidai serikali pia, sasa inataka kubadili mfumo wa kulipa pensheni na kwa taarifa nilizopewa na walimu inakata mafao kwa zaidi ya nusu. Huwezi kufanya kitu cha namna hiyo, hizo ni fedha za watumishi, wanawekeza ili watakapostaafu waweze kumudu maisha,” alisisitiza.
Alisema serikali inapaswa kusimamia matumizi kwa kuwa mapato ni makubwa, lakini haijulikani yanakwenda wapi.
Sumaye alisema haamini kama deni la taifa la zaidi ya Sh. trilioni 30 linahimilika kwa kuwa wakati wa uongozi wao wa awamu ya tatu, walikuta deni la Sh. trilioni 14, lakini walilipunguza hadi kufikia trilioni 6 hadi 7, pamoja na jitihada zao hizo deni hilo bado lilikuwa tatizo kwa taifa.
“Deni hilo bado lilikuwa tatizo, ukiniuliza hili la sasa, (ni wazi) litaumiza uchumi sana. Hata mkikusanya mapato, sehemu kubwa italipa deni… sijui itakuwaje, lakini wanaosimamia uchumi wanajua, tunawaombea,” alisema.
Alisema rais wa awamu ya tano atapaswa kulibeba deni hilo kwa kuweka nidhamu katika fedha kwa kuondoa mambo ambayo siyo ya msingi.
Alisema madeni ya ndani kwa wakandarasi na wazabuni mbalimbali ni mzigo mkubwa kwani wakiamua kudai fedha zao, ni tatizo kubwa kwani ni mzigo ambao haubebeki
Hivi karibuni, Naibu Waziri wa Fedha, Mwigulu Nchemba, alisema kiasi cha fedha kilichotengwa katika mwaka wa fedha 2013/14 kwa ajili ya ununuzi wa dawa zilikuwa ni Sh. bilioni 47, lakini serikali ilitoa Sh bilioni 7 tu kwa matumizi hayo.
AKIBA YA FEDHA
Akikumbushia enzi za utawala wa awamu ya tatu wa Rais Mkapa, Sumaye alisema wakati wanaingia madarakani hali ya maisha ilikuwa ngumu, lakini walijibana na hadi wanaondoka, akiba ya fedha za kigeni ilikuwa kubwa kiasi cha kuweza kulipia bidhaa na huduma kutoka nje kwa miezi minane; hadi Benki ya Dunia wakawashauri kupunguza akiba iliyokuwapo kwani ilikuwa kubwa kuliko wastani.
“Ni matokea ya nidhamu na usimamiaji wa shughuli za serikali kwa nguvu zote… hata fedha za matumizi ya kawaida za serikali kwenda ngazi za chini zilikuwa za kutosha. Hatukuwa na upungufu wa dawa, wala wanafunzi kurudi nyumbani kwa kukosa ada na elimu iliboreka. Wengi waliokuwa wanasomesha watoto Kenya na Uganda walibadilika na kuwarudisha nchini,” alisema.
“Usimamizi ni muhimu kuliko ukusanyaji. Unaweza , lakini kama huna nidhamu ni kazi bure,” alisema.Alisema kwa kipindi cha uongozi wao hawakuchapisha fedha na walisimamia uchumi na kuingia katika mpango wa kusamehewa madeni chini ya mpango wa Benki ya Dunia kwa nchi masikini zenye madeni makubwa (HIPC) ikiwa ni kati ya nchi nne.
UTAWALA BORA
Sumaye alisema haki ndiyo msingi wa utawala bora na kwamba kila zama na kitabu chake na kwamba hata leo, Baba wa Taifa angefufuka asingeweza kutawala kama enzi zake kwa kuwa kuna changamoto tofauti kulinganisha na kipindi alichokuwa akiongoza.
Alisema serikali zote zina mambo ambayo waliyafanya vizuri na mengine walikosea na kwamba ni vyema serikali yoyote inayotawala ikahakikisha kuwa na mambo mengi mazuri.
UCHUMI
Alisema yanahitajika marekebisho katika mfumo wa uchumi, kwa kuwa unakuwa kwa asilimia 7, lakini ni vyema kila mwananchi afaidi na siyo fedha kugawanywa kwa watu, bali kuwe na fursa za kutosha za kujiendeleza kiuchumi.
“Tuwe na uchumi mpana, unaojumuisha watu wengi na usiwe wenye kulenga watu fulani. Zipo nchi ambazo uchumi wake umekuwa kwa zaidi ya asilimia kumi, lakini umeshikwa na familia moja, kitaifa unakuwa, lakini uko kwa wachache tu,” alisema
Alisema kwa hapa nchini, uchumi haujakaa vizuri kwa kuwa haujaenea kwa watu wengi bali umebaki kwa wachache na hilo linapaswa kuangaliwa kwa kina na kurekebishwa.
Alisema namna pekee ya kuhakikisha uchumi unawanufaisha wote ni lazima fedha zitokanazo na rasilimali kama madini au gesi asilia zikatumika kunyanyua uchumi unaohusu watu wengi.
Alitolea mfano eneo la madini, akisema fedha kutoka huko zielekezwe katika sekta ya kilimo ambayo inakuwa kwa asilimia 4 huku kukiwa na ongezeko la watu kwa asilimia 3 na kwamba kutofanya hivyo, matokeo yake ni haya yanayoonekana sasa ambapo watu wengi wanakimbia kilimo kwa kuwa ukuaji wake bado ni mdogo.
Alisema iwapo kilimo kingekuwa kwa asilimia walau nane au tisa, maisha ya Watanzania wengi yangebadilika kwani watu wangejitosheleza kwa chakula na mahitaji ya msingi.
“Tunataka kuona uchumi unakua zaidi katika eneo lenye watu wengi, eneo la madini linabeba watu wachache… wale wanaofanya kazi migodini na wafanyabiashara tu, lakini tungeboresha sekta ya viwanda na kilimo, badala ya kuuza sufi unatengeneza nguo na kahawa badala ya kuuza punje unauza kahawa iliyosagwa,” alisema.
Sumaye alisema Nigeria ina utajiri wa mafuta, lakini haijaweza kunufaika na utajiri huo kwa sababu ya usimamizi usiokuwa makini, jambo ambalo Tanzania inapaswa kujifunza kwa kuhakikisha kwamba inakuwa na watalaamu kwenye maeneo hayo na wanatumika ipasavyo kwa manufaa ya taifa.
“Maeneo mengine kama misitu hatuhitaji kuwa na wataalam bali ni sera ya serikali kuwa sasa magogo hayasafiri nje… anayetaka aje kuwekeza kwenye kiwanda nchini. Lakini kwa rushwa, (magogo) yataendelea kusafirishwa.
Alisema Tanzania siyo nchi yenye misitu mingi na sasa inakaribia kwisha kama hatua za haraka zisipochukuliwa.
GESI
Alisema wakati wa utawala wa Baba wa Taifa, Mwalimu Nyerere, nguzo kuu za uchumi zilishikwa na dola, lakini sasa hali ni tofauti kwani sekta binafsi imetwaa nafasi na kampuni nyingi za kigeni zimewekeza nchini.
“Tatizo siyo kuruhusu kampuni binafsi, bali ni namna gani tunadhibiti kampuni hizo. Tangu zilipoingia hatujaweza kuwa na uwezo (wataalamu) wa kudhibiti, wanatupiga chenga (sana), tumefanya tathmini, tumeunda tume, kasoro zimebainishwa na kurekebishwa, lakini bado serikali inapigwa chenga,” alisema na kuongeza:
“(Suala la) kuchimba (gesi) halinisumbui… lipo mikononi mwa watu wengine, bali mikataba iwe yenye kupendelea nchi na wananchi wake, mikataba ambayo sote tunanufaika na sisi lazima tufaidike zaidi.”
Alisema muhimu ni kuwa na mikataba makini, kwa kuzingatia mapendekezo yaliyotolewa na tume mbalimbali zilizowahi kuundwa na kubaini kasoro zilizopo kuhusiana na madini ikiwamo ya Jaji Bomani.
Alisema eneo la gesi lisipoangaliwa vyema, taifa litaambulia patupu licha ya taarifa za wataalamu kueleza kuwa rasilimali hiyo ina faida kubwa.
“Usipokuwa makini, nao (wawekezaji) wanajua ni mahali pa kuchota kwa haraka … kuna fedha nyingi.Kama hatuna uwezo wa kuona mikataba vizuri na kuisimamia, tunaweza kupata hasara kubwa kwenye gesi,” alisema.
Alisema yeye hana tatizo kwa Watanzania kumiliki vitalu vya gesi na anaamini hakuna anayeweza kumiliki mwenyewe na kwamba siyo vyema kwa kiongozi au wafanyabiashara kushika vitalu kwa ajili ya kuviuza, bali waviendeleze kwa manufaa yao na taifa .
Alisema ni muhimu kwa Watanzania kuwa na hisa katika maeneo ya uchimbaji na ni vyema ikawepo sheria, iseme ili umiliki kitalu eneo fulani lazima Watanzania wawe na hisa, kwa kufanya hivyo Watanzania watanufaika na watakuwa jicho la serikali katika eneo hilo kuliko kuwaachia wageni peke yao.
“Eneo la gesi ni muhimu sana… mkilikosea mtakuwa maskini, mkipatia hali ya maisha itabadilika… naiomba serikali yangu isifanye makosa katika hilo,” alisema.
SOURCE: NIPASHE
Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
0 comments:
Post a Comment