Home » » MAJAMBAZI WAUA POLISI WAWILI KITUONI

MAJAMBAZI WAUA POLISI WAWILI KITUONI

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
  Wajeruhi wawili, wamelazwa hoi Bugando
  Wapora bunduki, mabomu usiku wa manane
IGP Ernest Mangu
Kundi la majambazi usiku wa kuamkia jana wakiwa na bunduki na mabomu, walivamia kituo cha Polisi cha Wilaya ya Bukombe mjini Ushirombo na kuua askari wawili na kujeruhi wengine wawili, kisha kupora silaha kadhaa zikiwamo bunduki, mabomu na risasi.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Geita, Joseph Konyo jana alithibitisha kutokea kwa tukio hilo, lakini akasisitiza kuwa habari zaidi zitatolewa baadaye baada ya uchunguzi wa awali kukamilika.

Mganga Mkuu wa Wilaya ya Bukombe, Dk. Honoratha Rutanisibwa, jana alithibitisha kupokea maiti mbili za askari hao na kuwataja kuwa ni WP 7106 Uria Mwandiga na PC Danstan Kimati mwenye namba G2615 ambao walikufa papo hapo katika shambulio hilo baada ya kujeruhiwa kwa risasi kichwani.

Dk. Rutanisibwa aliwataja majeruhi wawili kuwa ni Koplo David Ngutama (44) na PC Mohamed Hassan Kilomo (25).

Alisema Koplo Ngupama amejeruhiwa kichwani na inadaiwa ameng’olewa meno mawili, wakati PC Kilomo amejeruhiwa kifuani na amevunjika mguu wa kulia.
Kutokana na majeruhi hao kuwa katika hali mbaya, Dk. Rutanisibwa alisema wamehamishiwa hospitali ya Rufaa ya Bugando kwa matibabu zaidi.

Tukio hilo linalofanana na lingine lililotokea wilayani Mkuranga saa 7:00 usiku Juni 11, mwaka huu katika kituo kidogo cha polisi cha Mkamba ambako polisi mmoja aliuawa na majambazi waliokivamia na kupora bunduki tano na risasi kadhaa, habari kutoka eneo la tukio zinasema kuwa majambazi hayo yalitenda uhalifu huu saa 9:40 usiku.

Habari kutoka eneo la tukio zinasema kuwa majambazi hayo ambao idadi yao haijajulikana, wanadaiwa kukizingira kituo hicho na kuvunja dirisha kwa bomu, kisha kumimina risasi kadhaa eneo la mapokezi na kuua askari hao, kujeruhi wengine, na kupora silaha kadhaa na risasi.

Jana majira ya saa 8 mchana Inspekta Jenerali wa Polisi, Ernest Mangu, aliwasili mjini Ushirombo kufuatia tukio hilo ambalo limezidi kuzua maswali mengi juu ya usalama wa vituo vya polisi na utayari wao kukabili mashambulizi dhidi yao.
IGP Mangu alikuwa na kikao na kamati ya ulinzi na usalama ya mkoa wa Geita ofisini kwa Mkuu wa Wilaya ya Bukombe, Amani Mwenegoha.

Kikao hicho kilihudhuriwa na Mwenyekiti wa Kamati ya ulinzi na usalama ya mkoa, Mkuu wa mkoa wa Geita, Saidi Magalula, maafisa usalama wa taifa wa mkoa, afisa uhamiaji wa mkoa, Kamanda wa polisi wa mkoa na Mkuu wa wilaya Mwenegoha.

Baada ya kikao hicho alizungumza na waandishi wa habari na kuthibitisha kuhusu tukio hilo ambalo alisema kuwa kilichowaua polisi hao wawili ni bomu la kivita.
IGP Mangu hata hivyo hakutaka kusema kama majambazi hao ni wa kutoka Tanzania au nchi ya jirani, kwa kile alichosema uchunguzi bado unaendelea.

Alisema idadi ya bunduki na risasi vilivyoporwa haijajulikana kwa kuwa silaha hizo hazikuwa kwenye ghala kuu bali la muda ambalo hupokea silaha zilizo kwenye operesheni.

Hata hivyo, alithibitisha miongoni mwa silaha zilizoporwa kuwa ni aina ya SMG na mabomu na kuahidi dau la Sh. milioni 10 kwa mtu yeyote atakayefanikisha kukamatwa kwa majambazi hayo.

IGP Mangu alisema kwamba Mkurugenzi wa Upelelezi (DCI), Isaya Mungulu, atawasili Bukombe kwa ajili ya upelelezi wa tukio hilo.

MAJERUHI WANENA
Kilomo ambaye anapata matibabu Bugando katika mahojiano maalumu na NIPASHE alisimulia tukio hilo kuwa majambazi hao ambao idadi yao haijajulikana walivamia kituo hicho majira ya saa 8.45 usiku wa kuamkia jana wakiwa na bunduki na mabomu.

Alisema majambazi hao walishambulia kituo kwa kulipua bomu moja na kumimina risasi kadhaa kituoni, huku polisi watano waliokuwa kituoni wakijibizana nao kwa risasi.

Alisema walizidiwa nguvu na majambazi hao, alipoteza fahamu na alipojitambua alijikutana Bugando. Kilomo alisema kuwa amejeruhiwa ubavuni, mguu wa kulia na mkono wa kushoto.

NIPASHE ilishuhudia mguu wa Kilomo ukiwa umefungwa bandeji ngumu (PoP) na ubavu wa kulia ukiwa umefungwa bandeji, pia mkono wa kushoto umefungwa bandeji.

Mwenzake, Ngutama hali yake ni mbaya na amepoteza fahamu. NIPASHE ilishuhudia Ngutama akiwa amefungwa bandeji kichwani na mkono wa kushoto.

Afisa Muuguzi Msaidizi wa Bugando, Elizabeth Edward, alisema kuwa majeruhi hao walipokelewa jana saa 7 mchana wakitokea Bukombe na hali ya Ngutama ilikuwa siyo nzuri. Alisema Kilomo hali yake inaendelea vizuri.

UVAMIZI MKURANGA
Juni 11, mwaka huu majambazi sita walivamia kituo kidogo cha Polisi cha Mkamba kilichoko katika Wilaya ya Mkuranga mkoani Pwani na kumuua askari polisi, kuwajeruhi wanamgambo wawili, kupora bunduki tano, mbili aina ya SMG zenye risasi 60 na bunduki tatu aina ya shotgun zilizokuwa zimehifadhiwa ghalani.
Majambazi hao wakiwa na mapanga walimuua askari na kuwajeruhi wanamgambo hao usiku.

Polisi walidai kuwa silaha zilizoporwa zilikuwa zikisubiri kupelekwa katika kituo kikubwa cha polisi chenye ghala kuu kwa ajili ya hifadhi.
CHANZO: NIPASHE

0 comments:

Post a Comment

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Geita Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa