Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
Mjumbe wa Bunge la Katiba, James Mapalala ametoa siri ya
kutokujihusisha na suala la upigaji kura katika kamati yake namba moja
kwa kusema inapigia upatu serikali mbili.
Mapalala ambaye ni miongoni mwa waanzilishi wa
mfumo wa siasa wa vyama vingi nchini, alisema serikali mbili zimekuwa
zikimchefua, hivyo hawezi kushiriki usaliti huo. Katika kamati hiyo, pia
yupo Mbunge wa Nkasi Kaskazini (CCM), Ally Keissy aliyejipambanua kuwa
haungi mkono mfumo huo unaopigiwa upatu na chama chake.
“Mimi sikutoka bungeni kwa sababu niliamua
kupambana mle ndani... kusema kweli nimepambana nikiwa peke yangu na
mmoja wa wabunge wa CCM, lakini kila inapofikia hatua ya kupiga kura
katika vifungu vya Serikali mbili, mimi najitoa,” alisema Mapalala.
Kwa upande mwingine, mbunge huyo alikitaka Chama
Cha Mapinduzi na Serikali yake kumuomba radhi Jaji Joseph Warioba kwa
kumdhalilisha kuhusu masuala ya Rasimu ya Katiba.
Alisema Warioba anatakiwa kuombwa radhi kwa sababu
mambo mengi ambayo aliyapeleka katika Rasimu yalitoka kwa wananchi,
lakini yameachwa, jambo linaloonyesha kazi yake imekuwa ni ya bure.
Mapalala aliwaponda wajumbe wa Bunge Maalumu la
Katiba kwamba wanafanya kazi ya kutengeneza mfumo wa kugawana posho kwa
watu wa Tanzania Bara na Zanzibar.
“Hapa wanafanya mipango na ‘madili’ ya kugawana
posho, hatuna jambo jipya humo, tunachotaka sisi tulio wengi ni serikali
tatu na wanachokitaka wenzetu wachache ni serikali mbili na migao ya
madaraka na fedha, vitu ambavyo vimeshindwa kutuvusha kwa kipindi cha
miaka 50,” alisema Mapalala.
Kwa upande mwingine, mkongwe huyo alikituhumu chama hicho kwamba kinafanya mambo kwa kujiaminisha kuwa inaweza kutawala milele.
Hata hivyo, Mapalala amewataka vijana kuwa
wajasiri ili utakapofika wakati, waipinge katiba yenye mfumo wa serikali
mbili na waunge mkono serikali tatu
Chanzo;Mwananchi
0 comments:
Post a Comment