Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
WAKATI taifa likiwa kwenye sintofahamu juu ya mchakato wa katiba
mpya, wanawake wilayani Geita mkoani hapa wameitaka katiba ijayo kuweka
sheria za kujali wanawake, wajane na walemavu.
Wito huo ulitolewa jana na washiriki kwenye mdahalo uliofanyika
katika ukumbi wa Kanisa la Katoliki ambao uliandaliwa Geita Network
Platfom, ambapo walisema katiba iweke mambo ya kuwajali na kuwalinda
wanawake.
Washiriki hao walisema masuala ya wanawake yanapotambulika kikatiba
ni rahisi kutungiwa sheria na hivyo matatizo yoyote yanayowakabili
hutatuliwa kisheria badala ya kufanyiwa hisani.
Walibainisha kuwa miongoni mwa mambo yanayowakabili ni matukio ya
unyanyasaji na udhalilishaji, ikiwemo kubakwa huku kesi zao zikichukua
muda mrefu na hivyo ushahidi kupotea.
Joyce Juma, alisema kuwa kumekuwa na vitendo viovu ambavyo
wanafanyiwa wanawake bila serikali kuchukua hatua, kwa hiyo akaomba
kwenye katiba ijayo yawepo mambo ya kuwalinda na kuwatetea wanawake kwa
nguvu zote.
Katibu wa asasi hiyo, Isaka Kubini, alisema wataendelea kuandaa
makongamano kama hayo kila wakati ili wananchi waweze kuelewa na
kuipigia kura katiba inayopendekezwa baada ya kupitishwa bungeni.
“Tutazidi kuweka makongamano kama haya ili wananchi wawe na uelewa
wa wanachokipigia kura ya kukubali au kukataa katiba inayopendekezwa
wakati wa upigaji wa kura za maoni,” alisema.
Chanzo;Tanzania Daima
0 comments:
Post a Comment