Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
KATIBU Tawala wa Mkoa wa Geita, Seveline Kahitwa, amejeruhiwa
vibaya na kulazimika kukimbizwa katika Hospitali Teule ya Wilaya ya
Sengerema mkoani Mwanza, katika ajali iliyotokea juzi Kijiji cha
Bugulula.
Katika ajali hiyo, Mkuu wa Mkoa wa Geita (RC), Said Magalula, alipata majeraha madogo miguuni na mkono wake wa kushoto.
Viongozi hao walipata ajali hiyo walipokuwa katika msafara wakielekea
katika Hifadhi ya Taifa ya Msitu wa Rwande katika Halmshauri ya Wilaya
ya Geita, unaodaiwa kuvamiwa na wakulima na wafugaji.
Imedaiwa kuwa chanzo cha ajali hiyo, ni kusimama ghafla kwa gari la
Mkuu wa Polisi Wilaya ya Geita, Busee Bwire, lenye namba PT 1998
kumkwepa mtoto John Haule (4) aliyekatisha ghafla barabarani.
Kitendo hicho kilifanya magari yaliyokuwa katika msafara huo, likiwemo
la mkuu wa mkoa, katibu tawala mkoa, kamanda wa polisi mkoa na mkuu wa
wilaya ya Geita kugongana ovyo na kusababisha majeruhi kwa baadhi ya
viongozi hao.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Geita, Joseph Konyo, alisema chanzo cha
ajali hiyo ni uzembe wa wazazi wa mtoto huyo ambao walimwachia kuvuka
barabara, na kwamba kama sio uhodari wa dereva maisha ya mtoto huyo
yangepotea.
Mganga Mfawidhi wa Hospitali Teule ya Wilaya ya Sengerema,
aliyetambulika kwa jina moja la Dk. Charles, alikiri kupokea majeruhi
wa ajali hiyo kutoka Geita, lakini hakuwa na taarifa kama ni katibu
tawala wa mkoa.
Kutokana na ajali hiyo, Magalula alilazimika kusitisha ziara hadi hapo itakapopangwa tena.
Msitu wa Rwande wenye ukubwa wa ekari 16,000, umevamiwa na wakulima na
wafugaji tangu mwaka jana, huku wakitetewa na baadhi ya wanasiasa
wanaotaka waruhusiwe kuendesha shughuli za kilimo na ufugaji katika
msitu huo.
Chanzo:Tanzania Daima
0 comments:
Post a Comment