Home » » MAJAMBAZI YATIKISA MJI , YAUAWWA

MAJAMBAZI YATIKISA MJI , YAUAWWA

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 
  Yalipora maduka, kisha kufyatua risasi ovyo
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Geita, Joseph Konyo
Majambazi yamemvamia mfanyabiashara wa maduka ya M-Pesa mkoani Geita na kumuua kwa kumpiga risasi kisha kumpora fedha.Hata hivyo, majambazi wawili waliohusika katika tukio hilo waliuawa na polisi kwa kushirikiana na wananchi baada ya tukio hilo.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Geita, Joseph Konyo, alithibitisha kutokea kwa mauaji hayo pamoja na mfanyabiashara huyo kuporwa kiasi cha fedha ambacho hata hivyo, hakijajulikana.

Kamanda Konyo alisema tukio hilo lilitokea juzi jioni saa 11.30 jioni, katika kata ya Kalangalala mjini Geita.

Alimtaja mfanyabiashara aliyeuawa na majambazi hao kuwa ni Gosbert Walwa (54), ambaye alipigwa risasi kadhaa maeneo ya tumboni na kwamba alifariki dunia muda mfupi baada ya kufikishwa katika Hospitali ya Wilaya ya Geita kwa ajili ya matibabu.

Kamanda Konyo alisema majambazi hao walikuwa na bunduki moja aina ya SMG ambayo waliitumia katika uporaji na mauaji hayo.

Pia majambazi hao walifanya uporaji kwa wakala mkuu wa bia mjini humo na kupora Sh. milioni 1.8 pamoja na bastola.

“Kabla ya mauaji haya ya mfanyabiashara Walwa, wakiwa kwenye pikipiki, majambazi hao walivamia kwa wakala wa  kusambaza bia, Ignas Inyasi na kupora fedha na bastola yenye namba HO478Y ikiwa na risasi 15 inayomilikiwa kihalali na mfanyabisahara huyo (Inyasi),” alifafanua Kamanda Konyo.

Kamanda huyo alisema kuwa wakati polisi wakielekea katika eneo la tukio, majambazi hayo tayari yalikuwa yameshatoroka kwa kutumia pikipiki hiyo.

Alisema walitoroka baada ya kumteka wakala wa maduka ya M-pesa, marehemu Walwa, na kumpiga risasi tumboni na baadaye waliendelea  kujihami kwa kufyatua risasi kadhaa hewani.

“Polisi walizidi kupambana nao kwa umbali wa kilomita kadhaa karibu na Shule ya Sekondari Nyangh’wale, ndipo gari la polisi lilifanikiwa kumgonga jambazi aliyekuwa na silaha akijiandaa kufyatua risasi,” alifafanua Kamanda Konyo.

Alisema mara baada ya jambazi huyo kugongwa kwa gari na kufa papo hapo, mwenzake alizidi kusonga mbele kwa pikipiki, lakini mbele yake kulikuwa na wanafunzi wa shule ya sekondari waliosaidia kumzingira na kumshambulia hadi kufa.

Alisema kutokana na tukio hilo, wananchi kadhaa mjini Geita walielezea kufurahishwa na juhudi hizo za Jeshi la Polisi na kuahidi kununua pikipiki 12 pamoja na kuchangia gharama za mafuta kila mwezi, ili kuongeza juhudi za mapambano dhidi ya ujambazi mkoani humo.

Mmoja wa mashuhuda wa tukio hilo, Paschal Peter, ambaye ni muuzaji katika duka la bia, alisema majambazi hao wakati wanaingia dukani hapo walijifanya wateja na baada ya muda mfupi waliwaweka wateja chini ya ulinzi.

Alisema kuwa baada ya kuwekwa chini ya ulinzi, majambazi hao walipora kiasi hicho cha fedha za mauzo ya siku hiyo na kutokomea nazo.

Kamanda Konyo alisema majambazi hao vilevile walipora bastola iliyokuwa katika droo, mali ya Inyasi ambaye wakati wa tukio hilo hakuwamo.

Katika hatua nyingine, kundi kubwa la wananchi juzi usiku walikusanyika katika hospitali ya wilaya hiyo, baada ya kusikia taarifa za kuuawa kwa majambazi hayo, huku wakisukuma gari la polisi lililokuwa limebeba miili ya majambazi hao.
 
CHANZO: NIPASHE

0 comments:

Post a Comment

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Geita Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa