Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
Mjumbe wa Bunge Maalumu la Katiba kutoka Zanzibar, Juma Ali
Khatibu amesema kero za Muungano haziwezi kuwa sababu ya kuvunja
Muungano wa Tanganyika na Zanzibar uliozaliwa mwaka 1964.
“Dunia hivi sasa inaungana, nchi nyingi zinakuwa
wamoja. Jambo la kufanya hapa ni Bunge la Katiba kuangalia kero zetu ni
zipi katika Muungano halafu tukaziondoa,” alisema Khatibu.
Akizungumza mjini Dodoma jana, Khatibu alisema wajumbe wa Bunge hilo wanapaswa kuonyesha uzalendo katika kufikia uamuzi.
“Mimi ninachotaka kusema ni kuwa tumempata Rais
muungwana sana na kwa kweli nampongeza Rais Jakaya Kikwete kwa kuamua
kwamba kabla hajaondoka madarakani tupate Katiba Mpya,” alisema Khatibu.
Khatibu alisema kitendo hicho ni cha kihistoria na
kwamba Watanzania watamkumbuka kwa mwafaka wa kisiasa wa Zanzibar na
sasa Katiba Mpya.
Khatibu alisema baadhi ya viongozi wa nchi za
Afrika hawataki kuruhusu kuandikwa kwa Katiba Mpya mpaka kwanza waone
damu imemwagika lakini Tanzania inaandika Katiba yake ikiwa katika
mazingira ya amani.
Aliwasihi wajumbe wenzake waepuke kutazamana kwa
misingi ya Uzanzibari na Ubara na badala yake, washikamane kwa masilahi
ya taifa na wananchi kwa jumla.
“ Tanzania ni mfano wa kuigwa katika Afrika, nchi
nyingi sana zinajifunza kutoka kwetu kwa hiyo, Katiba isitufanye
tutengane. Kero za Muungano haziwezi kutufanya sisi tuvunje Muungano,”
alisema.
Malalamiko ya kero za Muungano yamekuwapo kwa
miaka mingi huku wanasiasa wakililia haja ya kuwapo kwa muundo mpya
utakaotoa fursa sawa kwa pande mbili za Muungano.
Hata hivyo, Rasimu ya Pili ya Katiba inapendekeza
muundo wa Muungano wa Serikali tatu jambo ambalo linatazamiwa kuzua
mvutano mkubwa wakati utakapofika muda wa kujadili Muungano kwenye Bunge
la Katiba.
Chanzo:Mwananchi
Chanzo:Mwananchi
0 comments:
Post a Comment