JESHI la Polisi mkoani Geita linamsaka Shija Hamisi (28), mkazi wa
Kijiji cha Ibamba kwa tuhuma za kumuua mtoto wake mwenye umri wa wiki
mbili kwa kumnyonga kwa wivu wa mapenzi.
Kamanda wa Polisi mkoani hapa, Kamishina Msaidizi Mwandamizi, Leonard
Paul, alisema kuwa mtuhumiwa huyo anaendelea kusakwa kwa kuwa
alitoweka baada ya tukio hilo.
Alisema tukio hilo lilitokea Jumatano iliyopita na kwamba chanzo ni
ugomvi wa kifamilia kati ya mtuhumiwa huyo na mkewe, Juliana Juma (20).
Inaelezwa Februari mwaka jana, Hamisi alikamatwa kwa tuhuma za wizi
wa mifugo wilayani Biharamulo, Kagera na alipotoka mahabusu alimkuta
mkewe akiwa mjamzito, hali iliyomtia shaka huenda mimba hiyo si yake.
Baada ya kujifungua Januari 22 mwaka huu, mtuhumiwa alidai mtoto
aliyezaliwa si wake na inadaiwa siku ya tukio, mkewe alikuwa akipika
jioni, na yeye alienda ndani alipokuwa amelala mtoto huyo na kumnyonga.
Taarifa hizo zinaeleza baada ya kumuua mtoto huyo kwa kumnyonga,
alichukua baiskeli kama anatoka kidogo huku mkewe akiendelea kupika,
lakini baada ya muda hakumsikia mtoto akilia ndipo alipoamua kwenda
ndani na kukuta mtoto amenyongwa na kutupwa chini.
Kamanda aliwataka wananchi wa Mkoa wa Geita kuendelea kutoa
ushirikiano ili kuwabaini watu wanaojihusisha na vitendo viovu, waweze
kukamatwa na kufikishwa mahakamani.
“Nawaonmba wananchi wasichukue sheria mkononi wawalete watuhumiwa nasi tutawafikisha mahakamani,” alisema Kamanda Paulo.
Chanzo;Tanzania Daima
0 comments:
Post a Comment