WANANCHI wa eneo la soko la chakula la mji mdogo wa Ushirombo,
wilayani Bukombe, Geita, wapo hatarini kukumbwa na magonjwa ya mlipuko
kutokana na dampo la taka kufurika.
Diwani wa mji mdogo wa Ushirombo, Soud Ntanyagala (CHADEMA),
alibainisha hayo alipozungumza na waandishi wa habari muda mfupi baada
ya kumalizika kikao cha baraza la madiwani cha Halmashauri ya Wilaya ya
Bukombe.
Alisema kutokana na hali hiyo anakusudia kuhamasisha mgomo kwa
wananchi wa mjini huo ili kushinikiza halmashauri kuzoa taka hizo.
“Kwa sasa soko hili limejaa uchafu mwingi, halmashauri imekuwa
ikichelewa kuzoa taka na sasa imefikia hatua mbaya, wapo
wafanyabiashara wa mboga mboga na vyakula kwa maana nyingine kuna
uwezekano wa wafanyabiashara na wateja wao kupatwa na magonjwa ya
mlipuko kama vile kipindupindu.
“Nimepiga kelele nimeshindwa, kilichobaki kwa sasa ni kuhakikisha
nashawishi maandamano kwa ajili ya kushinikiza halmashauri ifanye
haraka kuondoa taka hizo,” alieleza diwani huyo.
Mbali na hilo, alisema atahakikisha anapinga tabia ya kubadilisha
matumizi ya fedha ambazo zimekusudiwa kufanya miradi mbalimbali lakini
zinabadilishiwa matumizi.
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Bukombe, Lilian Matinga,
alisema atasimamia uamuzi wa madiwani wenye masilahi kwa wananchi wa
wilaya hiyo.
“Nipo kwa ajili ya kusimamia maendeleo ya wananchi na sitakubaliana
na kiongozi yeyote ambaye anataka kufanya halmashauri kama mali yake au
kuisababishia hasara halmashauri kwa kushindwa kutumia fedha ambazo
zimekusudiwa kutumika katika miradi mbalimbali,” alisema mkurugenzi huyo
Chanzo:Tanzania Daima
0 comments:
Post a Comment