NA MARCO KANANI, GEITA YETU BLOG
WALINZI wa mgodi wa dhahabu wa GGM wamemuua mwananchi Emanuel Mwita (32) kwa kumpiga hadi kufa walipomkuta ameingia mgodini humo kuokota mawe ya dhahabu katika vufusi vilivyomwagwa.
Tukio la kuuawa kwa mwananchi huyo lilitokea usiku wa kuamkia tarehe 16.12.2013 majira ya saa saba usiku ambapo baada ya walinzi hao kumkamata mtu huyo walianza kumshambulia kwa kipigo.
Kwa mujibu wa mmoja wa vijana waliokuwa na kijana huyo alisema baada ya walinzi hao kumkamata menzao walianza kumpiga sana bila huruma huku wao wakikimbia.
Kijana huyo aliendelea kusema kuwa kesho yake ya tarehe 16.12.2013 walienda kuulizia kituo cha Polisi Geita kujua kama kuna mtu alikamatwa jana mgodini lakini waliambiwa hakuna mtu wa aina hiyo aliyeletwa kituoni hapo.
Waliamua kwenda hospitali ndipo walipopewa taarifa na uongozi wa hospitali hiyo kuwa kuna mtu aliletwa na walinzi wa mgodi wa GGM na kutelekezwa hospitalini hapo akiwa na hali mbaya sana na alifariki muda mfupi akiwa anapatiwa matibabu.
Kaimu mganga mfawidhi wa hospitali wa wilaya ya Geita Adamu Sijaona alisema marehemu alikuwa na jeraha kubwa kichwani pia alikuwa akitokwa damu mdomoni na mkono wake wa kushoto ulikuwa umevunjika.
Kaimu kamanda wa Polisi mkoani Geita Amina Baturumili alisema hajapata taarifa za tukio hilo huku akilishukuru gazeti hili kwa kumpatia taarifa hizo akiahidi kuzifuatilia ambapo baadaye alithibitisha kutokea kwa tukio hilo.
0 comments:
Post a Comment