Geita. Askofu wa Kanisa Katoliki Jimbo la
Geita, Damian Dallu amesema viongozi wengi wamekuwa wakijidanganya kwa
kuwa wabinafsi na wenye kujirundikia mali na kutojali watu maskini kwa
kuamini kufanya hivyo watajitengenezea mazingira ya kufurahisha nafsi
zao.
Akihutubia kwenye ibada ya Krismasi
iliyoadhimishwa kitaifa mkoani Geita, askofu huyo aliwataka Watanzania
kuacha ubinafsi na kupendana huku akisisitiza kuwa;“Ukiona mwenye
madaraka anajifirikia mwenyewe na kusahau shida zinazowakabili watu
maskini basi huyo siyo kiongozi wa watu.”
Askofu Dallu alisema siku zote kiongozi ni mtu wa
kuwajali watu na anapaswa kuwajibika kwao, lakini kama inatokea kiongozi
anaweka masilahi yake mbele huyo kiongozi hafai,” alisema Askofu Dallu.
“Mali haitawaletea furaha kamwe. Hata ikitokea
mahali kuna mali mfano hapa Geita tuna dhahabu, Mtwara wana gesi na watu
wanatumia madaraka yao kuwataka watu wa Mtwara watenganishwe na
Watanzania wenzao kwa ajili ya gesi,” alionya.
Alisema kuwa na ubinafsi wa kujirundikia mali
kamwe hauwezi kumletea furaha binadamu mbali ya kuwa chanzo cha vurugu
na mitafaruku.
Alitolea mfano nchi za Uarabuni namna
zilivyobarikiwa kuwa na mali ya asili kama mafuta lakini hata hivyo
pamoja na neema hizo bado nchi hizo zinakabiliwa changamoto ya ukosefu
wa amani.
Askofu Dallu alisema kuwa viongozi waliopewa
dhamana ya kuongaza watu wanatumia vibaya nafasi zao ikiwa ni pamoja na
kuharibu rasilimali za nchi kwa kushiriki kuhamasisha watu kuwa na
utengano.
Alisema viongozi wengi wanatumia mamlaka ili
wapate kutawala rasilimali za nchi kwa manufaa yao binafsi bila
kuwahurumia Watanzania wenzake.
Pia alikemea vitendo vya baadhi ya viongozi na
jamii nzima kuharibu na kutumia vibaya rasilimali za nchi kwa kuua tembo
na kuangamiza vivutio vya nchi kwa masilahi binafsi.
Chanzo;mwananchi
Chanzo;mwananchi
0 comments:
Post a Comment