“Ukistaajabu
ya Musa utayaona na Firauni” ni maneno ambayo yamekuwa yakitumiwa na
watu mbalimbali hapa nchini, yenye lengo la kuikumbusha jamii fulani juu
ya yale yanayotokea kwa wakati huo.
Maneno
haya, nimelazimika kuyakumbuka katika makala haya kutokana na tukio
lililotokea wilayani Geita wiki iliyopita, ambapo gari la kubeba
wagonjwa lilikamatwa likiwa linatumika kubeba mafuta ya wizi katika
mgodi wa dhahabu wa Geita (GGM).
Kamanda
wa Polisi Mkoani Geita, Leonard Paulo, anazungumzia tukio hilo kuwa
lilitokea Septemba 5, mwaka huu saa saba usiku likiwa na lita 630 za
mafuta zenye thamani ya sh.mil 1.3.
Analitaja
kuwa ni lenye namba za usajili T.671 AKW aina ya Land Cruiser ambalo ni
la kituo cha afya cha Nzera katika Halmashauri ya Wilaya ya Geita.
Anasema
lilikuwa likiendeshwa na Bw.Amud Bihemo (28) ambapo lilikuwa
limefunikwa maandishi yanayotoa utambulisho wake kuwa ni gari la
wagonjwa kituo cha afya Nzera na mengineyo kama vile alama ya msalaba
mwekundu ili lisitambulike kwa urahisi.
“Limekamatwa
na polisi kwa kushirikiana na walinzi wa mgodi huo, likiwa mgodini
katika eneo la kufua umeme wa mgodi lijulikanalo kama Geita power, huku
maandishi yanayolitambulisha kama gari la wagonjwa Nzera yakiwa
yamefunikwa kwa karatasi za mng’ao na ile sehemu ya kubebea mizigo nayo
ikiwa imeng’olewa pamoja na kimulimuli chake ambapo pia waliweka
kitambaa cha kuakisi mwanga ili lifanane na yale ya mgodi huo,” anasema
Kamanda Paulo.
Anawataja
watuhumiwa wengine ambao walikamatwa eneo la tukio kuwa ni Bw.Malemo
Paul (38), Bw.Seleman Magoso (31), Bw.Julias Boas (28), Bw.Rashid
Hussein (27) na Ismail Zuberi(26) wote walinzi wa kampuni ya ulinzi ya
G4S.
Wengine
ni Bw.Christopher Kombo(26), mfanyakazi wa mgodi huo na Joseph
Christopher na kwamba watuhumiwa wengine walifanikiwa kutoroka.
Kwa
hakika tukio hili, linawagusa watu wengi si wilayani humo pekee bali
hata katika mikoa mingine hasa kwa wananchi waishio maeneo ya vijijini,
ambao wamekuwa wakitaabika kutokana na huduma duni za usafiri pindi
wanapokabiliwa na matatizo ya kiafya.
Gari
hili la kubeba wagonjwa ni msaada uliotolewa na mgodi wa dhahabu wa
Geita (GGM) mwezi Desemba mwaka jana, likiwa na thamani ya sh.mil. 40
ili kusaidia kuondoa kero ya wananchi wanaopata huduma ya matibabu
katika kituo cha afya cha Nzera.
Kituo
hiki cha afya ambacho kiko umbali wa zaidi ya kilomita 40 kufika ulipo
mgodi huu, kinategemewa na idadi kubwa ya wananchi wanaoishi katika
tarafa ya Bugando yenye kata sita ambazo ni Nzera, Senga, Nkome,
Muharamba, Fulwe pamoja na Ruenzela.
Kwa
mjibu wa sera ya afya, kituo hiki kimelenga kutoa huduma kwa wananchi
wapatao 34,812 ambao ni kutoka kata ya Nzera pekee na ndio walistahili
kuhudumiwa na gari hili lakini kutokana na upungufu wa magari ya
wagonjwa limekuwa likitoa huduma na maeneo mengine ndani ya tarafa hii.
Baadhi
ya familia zinazoishi katika maisha duni, zimekuwa zikilazimika kutumia
usafiri wa baiskeli na nyingine kutumia mikokoteni inayokokotwa kwa
punda ili kuwawezesha wagonjwa wao kuzifikia huduma za afya kama vile
zahanati, vituo vya afya ama hospitali za wilaya na zile za rufaa.
Usafiri
wa aina hii mara nyingi umekuwa ukisababisha vifo vya mara kwa mara
hasa kwa akina mama wajawazito wanapopatwa matatizo wakati wa kujifungua
pamoja na watoto ambao wamekuwa wakisumbuliwa na tatizo kubwa la
ugonjwa wa malaria.
Tukio
hili la gari la wagonjwa kutumika katika shughuli za wizi kinyume na
matarajio ya serikali na wananchi kwa ujumla, maoni tofauti yametolewa
huku mambo mapya yakijitokeza.
Wananchi
wa Nzera ndio hasa walioguswa na tukio hili kwa kile wanachokiona kuwa
hali ya afya zao iko shakani kutokana na hujuma kama hizi za matumizi
yasiyo sahihi ya magari ya kubeba wagonjwa.
“Taarifa
hizi binafsi zilinihuzunisha mno, tumekuwa katika mateso makubwa kabla
ya kuletwa katika kituo hiki, lilikuwa msaada kwetu kwani kuna familia
nyingine hazina fedha kwa ajili ya kukodi gari kutoka hapa Nzera hadi
hospitali ya wilaya ya Geita, hivyo lilikuwa linatusaidia kwa kweli hasa
sisi kina mama,” anaeleza kwa masikitiko Bi. Verediana Nestory mkazi wa
Nzera katika mazungumzo na mwandishi wa makala haya aliyetembelea
kijijini hapo.
“Tunapata
shida lisipokuwepo hili gari la wagonjwa, watu wengi watapoteza maisha
kwa sababu tu ya kushindwa kupata huduma mapema kutokana na kutokuwa na
fedha, mfano huko nyuma kabla halijaletwa hapa kuna jirani yangu
niliwahi kumshuhudia akiweka dhamana ya mbuzi ili apate gari ya kukodi
toka kwa mtu binafsi ili mgonjwa wake apelekwe hospitali ya Wilaya ya
Geita,” anaongeza.
Anasema,
jirani yake huyo aliyeweka dhamana ya mbuzi hakuwa na fedha kwa ajili
ya kulipa usafiri wa gari ili kumuokoa binti yake aliyekuwa na tatizo la
kujifungua, ambapo mumewe alimtelekeza na kukimbilia kusikojulikana.
Mwanamke
mwingine ambaye hakutaka kutaja jina lake gazetini, mfanyabiashara ya
duka jirani na ulipo mgahawa aliokuwa akipendelea dereva wa gari hilo la
wagonjwa kijijini hapo, anasema wao wanachotaka gari hilo lirejeshwe
katika kituo hicho cha afya.
“Kama
ni wizi amefanya dereva kwa tamaa zake sawa lakini tunachotaka sisi
wananchi wa Nzera, gari letu la wagonjwa waturudishie tu, kwani lilikuwa
likisaidia watu wengi katika maeneo haya ya tarafa nzima ya Bugando,
haiwezekani kosa afanye dereva halafu wananchi tuadhibiwe kwa kukosa
huduma,” anasema.
Baadhi
ya wananchi walisema kuwa licha ya kuwa gari hilo lilitakiwa kutoa
huduma hiyo bure, lakini baadhi yao walikuwa wakitozwa fedha kati ya
sh.10,000 hadi 30,000 kama gharama ya kuchangia mafuta, fedha ambazo
zinasadikika zilikuwa zikichukuliwa na dereva wa gari hilo.
Kwa
mujibu wa Mganga Mfawidhi wa kituo hicho cha afya Nzera, Dkt. Bahati
Nyamachaguri ni kuwa kabla ya tukio hilo la kukamatwa kwa gari hilo la
wagonjwa, kuna mgonjwa aliyemtaja kwa jina la Domicia Kabale (56)
alikuwa amelazwa kituoni hapo na alipatwa na tatizo la kupooza mdomo
ambapo alilazimika kupelekwa hospitali ya wilaya ya Geita kwa matibabu
na uchunguzi zaidi.
“Tulilazimika
kulitumia gari hili la wagonjwa mimi ndiye niliongoza msafara na ndani
ya gari tulikuwemo watu wanne akiwemo mgonjwa na ndugu yake, kwa kuwa
kesho yake nilitakiwa kuchukua dawa za kupunguza ugonjwa wa virusi vya
Ukimwi(VVU).”
“Tulifika
salama saa 11 hivi jioni ya siku hiyo, mgonjwa akapokelewa na wenzetu
wa hospitali ya wilaya na kwa mujibu wa sheria niliamini gari hilo
litabaki hapo hospitali hadi kesho yake,” anaongeza.
Anasema,
kesho yake asubuhi wakati anafika hospitalini hapo akijiandaa kwenda
kuchukua dawa hizo lili arudi kituoni kwake kwa kulitumia gari hilo,
alishangaa baadhi ya madereva waliokuwa wamekusanyika wote wakiwa
wameelekeza macho yao kwake na baadaye aliambiwa kuwa gari la kituo
chake cha Nzera liko kituo cha polisi baada ya kukamatwa likifanya
uhalifu mgodini.
“Nilienda
kituoni pamoja na mkurugenzi, tulikuta kweli gari liko hapo polisi,
likiwa limezibwa maandishi kwa stika, sehemu ya juu ya kubebea mizigo
imeng’olewa na imewekwa kitambaa cha mng’ao kama yale ya mgodini,
nilibaki kushangaa.” anasema.
Mganga
huyo Mfawidhi, anasema gari hilo huwa linawekewa mafuta kila siku ya
Jumatatu kutoka ofisi ya Halmashauri ya wilaya na kuwa tukio hilo
alilosema kuwa siyo zuri limemuumiza yeye binafsi.
“Kwa
kweli limenipatia fundisho kubwa wananchi walikuwa wamelizoea kutokana
na kuwa msaada wao mkubwa ingawa wapo baadhi ya viongozi wa kisiasa
walikuwa wakitoa vitisho kwa dereva pindi anapogoma kufanya yale
wanayotaka ikiwemo kubeba wagonjwa wao pasipo kupitia ngazi zinazohusika
za uongozi. Hii inatokana na baadhi ya watu kutojua utaratibu.
Mwandishi
wa makala haya akiwa kituoni hapo, alishuhudia mume na mke waliokuwa na
mtoto wao aliyekuwa na tatizo la kuishiwa damu kwa mjibu wa daktari,
wakibaki kuangua kilio kutokana na kushindwa gharama ya nauli ya
sh.4,000 ili kumfikisha mtoto huyo hospitali ya wilaya ya Geita kwa
matibabu.
Majira
iliweza kubaini kuwa katika kituo hicho, hapakuwepo na kitabu cha
makabidhiano kwa ajili ya kusaini pindi gari hilo linapoingia ama kutoka
ambapo dereva wake pia hakuwa mtumishi wa kudumu wa Halmashauri hiyo
bali alikuwa akifanya kazi kama kibarua (cassual) aliyekuwa akisaini
mkataba kila baada ya miezi mitatu.
Mmoja
wa dereva basi dogo la abiria maarufu kama Hiace linalofanya safari
zake kutoka mjini Geita kwenda Nkome kupitia kijijini hapo, ambaye
hakutaka kutaja jina lake kwa usalama wake, anasema mara nyingi gari
hilo la wagonjwa amekuwa akilikuta limeegeshwa porini jirani na eneo la
mgodi wakati wa usiku.
“Hawa
bwana watakuwa wamedhulumiana wao kwa wao tu ni mara nyingi pengine
limekuwa likitumika kwa shughuli kama hizi hasa usiku, nimekuwa
nikikutana nalo limeegeshwa hapa porini usiku, siku zimefika mwisho,
dogo amechezea kazi ningelikuwa na ndugu yangu huko wizarani
ningelimpigia nipate hiyo nafasi,” anasema.
Naye
mlinzi mmoja wa kampuni ya Intensive Security inayotoa huduma ya ulinzi
katika hospitali ya wilaya ya Geita(jina limehifadhiwa), anasema siku
ya tukio dereva huyo aliwaeleza kuwa yuko zamu ya usiku, hivyo gari lake
litakuwa na mizunguko ya mara kwa mara kutoka nje na kuingia lango kuu
la hospitali hiyo ya wilaya.
“Unajua
bwana yaani unaweza kudanganya sana lakini kama siku imefika imefika
tu, siku hiyo alikuja hapa getini na kutueleza yuko zamu na kama kawaida
tuna vitabu huwa tunaweka kumbukumbu yaani siku hiyo alianza kutoka saa
2 usiku na kuingia mara nyingi kweli hadi tukachoka kufungua geti
tukalazimika kuliacha wazi na mara ya mwisho alitoka saa 7
usiku,”anasema mlinzi huyo wa Kampuni ya Intensive Security na kuwa
kuruhusiwa kwa gari hilo kunatokana na magari ya wagonjwa wakati
mwingine kutumika kuwapeleka madaktari nyumbani kwao pindi wanapomaliza
kazi za kuhudumia wagonjwa.
Mkuu wa Mkoa na wilaya nao wanena
Mkuu
wa Mkoa wa Geita, Bw. Magalula Said Magalula, katika mazungumzo na
waandishi habari ofisini kwake, amewataka madereva na viongozi wa
serikali kuacha kutumia vibaya mali ya umma kwa kuwa ni aibu.
Mkuu
wa Wilaya ya Geita, Bw. Manzie Omary Mangochie, anasema tukio hilo
limemshtua mno na kwamba hakuwa na mawazo kuwa kuna siku ataliona gari
la wagonjwa likiwa linatumiwa katika vitendo vya wizi badala ya kufanya
kazi yake ya kubeba wagonjwa.
“Nimesikitika
sana, binafsi nimelazimika kufika kituoni mwenyewe kuona kitendo hiki
cha fedheha! Lazima hatua zichukuliwe kamwe hatutokubali vitendo vya
namna hii viendelee katika wilaya yetu, nimeagiza hatua kali zichukuliwe
mara moja,”anasema mkuu huyo wa wilaya kwa masikitiko makubwa.
Kauli ya uongozi wa Halmashauri
Kwa
upande wake Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Geita, Bw. Ali
Kidwaka, anakiri kuwa ni kweli dereva huyo alikuwa kibarua kwa muda wa
mwaka mmoja sasa.
“Niliunda
timu maalumu kufuatilia mara baada ya tukio hili na ilifahamika dereva
hakuwa mwajiriwa wa kudumu wa Halmashauri, lakini pia limetupatia
fundisho na angalizo kubwa,” anasema.
“Gari
la wagonjwa kutumika katika wizi kama huu bila shaka hata wewe
mwandishi hili wazo sidhani kama ulikuwa nalo kuwa inaweza kuwa, ndivyo
hivyo hata mimi lakini kuanzia sasa tunaanza kufanya ufuatiliaji magari
yote ya serikali katika Halmashauri, tutatoa waraka kama njia ya
kudhibiti na kweli tutafanya hata ziara za kushtukiza,” anaongeza.
Anasema,
kwa sasa Halmashauri hiyo yenye vituo vya afya vitano ambavyo ni
Katoro, Chikobe, Kashishi, Bukoli na Nzera inakabiliwa na upungufu
mkubwa wa magari ya kubeba wagonjwa ambayo yaliyopo sasa ni mawili
pekee.
Kwa
mjibu wa taarifa ya maombi maalumu yaliyopelekwa Wizara ya Fedha kwa
Halmashauri hiyo mwaka 2011, jumla ya sh.mil. 420 zilikuwa zimeombwa kwa
lengo la kununua magari matatu ya kubeba wagonjwa, maombi ambayo
hayakukubaliwa.
Maombi
hayo yalikuwa yamelenga kurahisisha utoaji wa huduma kwa haraka ikiwa
ni pamoja na kuokoa maisha ya wananchi wilayani humo.
Mwenyekiti
wa Halmashauri hiyo, Bw.Elisha Lupuga anasema “dereva huyu lazima
afukuzwe kazi mara moja na kutokana na tukio hili jana tumefanya kikao
na madereva wote wa Halmashauri, tumeonya kuwa endapo litajirudia
hatutawafumbia macho wale wote watakaopatikana wakijihusisha na vitendo
hivi,” anasema.
“Suala
la kwamba dereva alikuwa mwajiriwa wa muda si hoja bali hata kama
angelikuwa ameajiriwa angefanya hivyo kama ni tabia yake, hivyo lazima
hatua zichukuliwe kwa mujibu wa sheria,” anaongeza mwenyekiti huyo.
Viongozi wa vyama vya siasa wanazungumziaje tukio hili?
Katibu
wa Itikadi, Siasa na Uenezi wa Chama Cha Mapinduzi(CCM) mkoani Geita,
Bw.Said Kalidushi anasema kuwa tukio hilo ni sawa na hujuma kwa wagonjwa
ambao ndio wanaolitegemea zaidi.
“Ni
hujuma kwa wagonjwa, mfano endapo pangelikuwepo na mgonjwa ambaye
alitakiwa kutolewa kituoni hapo kwenda hospitali ya wilaya ya Geita kwa
matibabu zaidi ina maana angelipoteza maisha kutokana na hujuma kama
hizi.”
“Siamini
inakuwaje gari la wagonjwa liende mgodini kuiba mafuta badala ya
kuhudumia wagonjwa? CCM imekuwa ikilalamikiwa kwa matukio kama haya,
hizi ni tamaa zake na gari hili lilitolewa na mgodi na hilo hilo ndilo
limeenda kuiba humo ndani yaani hii ni sawa na mbwa anayemng’ata mfugaji
wake...” anasema na kuongeza kitendo hicho kisiwavunje wafadhili bali
waendelee kutoa misaada kwa jamii pale wanapoona inafaa kuwa hivyo.
Msemaji
wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) mkoani Geita, Ignas
Karashani, anasema kuwa serikali inatakiwa kufanya uchunguzi wa kina ili
kubaini endapo kitendo cha gari hilo kwenda kufanya wizi mgodini
kilikuwa na shinikizo toka kwa kiongozi yoyote ili hatua zichukuliwe
mara moja.
“Kazi
ya gari hili ni kubeba wagonjwa kwa dharura, huko nani aliamuru liende?
Pale Nzera kuna diwani ambaye ni Musukuma kama diwani naye alipaswa
kufuatilia kwa karibu kwa sababu linahudumia watu wake, lazima naye
ahojiwe huenda alishinikiza kwa maslahi yake,” anasema Diwani wa kata ya
Nzera ambaye pia ni Mwenyekiti wa CCM mkoani humo, Bw.Joseph Musukuma
yeye alitupia lawama Mganga Mfawidhi wa kituo hicho pamoja na dereva
kuwa wanastahili kuwajibika.
“Mganga
Mkuu na dereva wote wanatakiwa kwenda jela tu hao,” alimaliza kisha
kukata siku kwa kile alichoeleza alikuwa akiendelea na mkutano.
Uongozi wa mgodi
Kaimu
Mkurugenzi Mgodi wa Dhahabu wa Geita (GGM), Bw. Jasper Musadaidzwa,
katika taarifa yake kwa vyombo vya habari anasema kuwa mgodi huo
umeshtushwa na tukio hilo la wizi uliofanywa kwa kutumia gari la kubeba
wagonjwa.
Anasema,
mgodi huo ulitoa msaada wa gari hilo, kwa lengo la kusaidia kusafirisha
wagonjwa, watoto na akina mama wajawazito kwa kuzingatia moja ya sera
ya afya ya mgodi huo isemayo wananchi lazima wanufaike na uwepo wao.
“Tumeshtushwa
na wizi huu ambao umefanywa na watu wachache ambao wanatumia rasilimali
za umma kwa matumizi yao binafsi badala ya kuokoa maisha ya watu,”
anasema mkurugenzi huyo wa GGM.
Kukamatwa
kwa gari hilo la wagonjwa likiiba mafuta mgodini humo, kumeleta hofu
kubwa kuwa huenda pengine yapo baadhi yanatumika katika usafirishaji
dawa za kulevya kwa kuwa si rahisi kukaguliwa na polisi kwa kudhaniwa
yamebeba wagonjwa.
Takwimu
zinaonesha kuwa Tanzania inakabiliwa na uhaba mkubwa wa magari ya
kubeba wagonjwa katika vituo na hospitali mbalimbali, hali ambayo
ilisababisha Rais Jakaya Kikwete wakati wa kampeni za uchaguzi mkuu
2010, kuahidi kusambaza pikipiki za matairi matatu (bajaji) zipatazo
400,000 nchini.
Katika
ahadi hiyo, Rais Kikwete alisema lengo ni kusaidia wagonjwa hususani
wanawake wajawazito kuwahishwa hospitali wakati wa kujifungua.
Kwa
mujibu wa sera ya afya ya mwaka 2007, Serikali kwa kushirikiana na
wadau mbalimbali itahakikisha utoaji wa huduma bora za uzazi katika
vituo vya kutolea huduma za afya zinazowavutia wanawake, wanaume na
vijana hapa nchini
Majira
2 comments:
HAYA XAXA
geta yetu
Post a Comment